Walikutana katika tamasha la
muziki, alikuwa anacheza peke yake kipweke akasikia sauti ikipasua anga katika
himaya ya masikio yake.. ‘tunaweza kucheza wote’ hakujibu kwa maneno akamgeukia
wakaanza kucheza, angeweza vipi kumkatalia msichana Yule mtulivu wa umbo na
mwepesi kutabasamu. Baada ya kucheza sana, msichana akataka kuaga, mwanaume
naye akasema yu njiani kuondoka. Wakatoka wote nje, mwanaume akiwa na pensi
chakavu na fulana inayokaribia kufubaa…
Mwanaume hakutegemea kama
msichana Yule alikuwa na usafiri wake lakini ilikuwa hivyo.
Alimpatia lifti katika gari lake.
Wakafahamiana na huo ukawa mwanzo wa kuwasiliana kiukaribu zaidi.
Msichana yule akajitambulisha kwa
jina la Caroline Mduma, naye mvulana hakusita kujitambulisha kwa jina lake la
kuzaliwa Benard Ngayoma ama alivyozoeleka Ben.
Kituo cha Magomeni Mikumi ndipo
Ben alipoishia, Caro akaagana naye huku akijitambulisha mahali anapoishi
‘Naishi Mbezi ya kimara’
“Asante sana kwa lifti….” Ben
alimalizia huku akishuka garini.
Milango ikafungwa gari ikaikamata
barabara na kutoweka.
Akiwa katrika kibanda chake cha
chumba kimoja alichoishi na rafiki yake, usiku majira ya saa nne simu yake
ikaita. Ilikuwa namba ngeni. Akaogopa kupokea akihofia wadeni wake huenda
wanamtafuta. Ile hali ya kushindwa kupokea simu ikamfadhaisha sana na
kujitambua kuwa alikuwa masikini wa kutupwa.
“Pokea simu kaka…unadhani
ukiipotezea nd’o mwisho wa matatizo.” Rapha alimsihi Ben. Alipotaka kuipokea
ikawa imekatika.
Alipotaka kuitazama namba kwa
makini mara simu ikaita tena.
Ben akapokea.
Sauti ya kike ikamlaki kwa
bashasha la aina yake.
“Mh unawahi kulala jamani au nd’o
namba mpya hupokei mwenzetu.”
“Aaah…si unajua tena…aah” akajibu
kipumbavu bila kujua anataka kusema nini.
“Caro hapa usije ukadhani kidemu
chako cha kule Temeke.”
“Caro….Caro…” alijaribu
kulitafakari jina.
“Caroline Mduma….tumekutana
tamashani.” Alimalizia utambulisho wake.
Ben akakaa kitako hakutegemea
kabisa kupokea simu kutoka kwa mrembo yule ambaye alionekana dhahiri kuwa
hakuwa na shida ndogondogo.
Mazungumzo
yakaendelea…walizungumza kwa takribani dakika hamsini. Wakayazungumzia maisha
ya Dar kidogo, wakapitia na adha ya usafiri wa Dar wakikumbushiana foleni kubwa
kutoka maeneo ya ‘Faya’ hadi mataa ya Magomeni mapipa. Maongezi yakapaa zaidi
na kuufikia ubinafsi. Hapa wakaombana wao kwa wao wasiongee sana wapeane miadi
wataongea ana kwa ana.
Wakakubaliana na kuagana.
Benard akamsimulia Rapha.
Wakalala wakiwa na tafakari hiyo kichwani. Caro.
*****
LICHA ya kuishi Magomeni, Ben
hakuwahi kula wala kunywa katika hoteli ya Travertine iliyopo mkabala na
barabara ya Morogoro. Siku hiyo alikuwa anakula kwa bili ya Caroline Mduma.
Caroline alimtazama Ben kwa macho
ya kuibia akagundua kuwa kuna mambo kadhaa Ben alikuwa hayajui. Kwanza ni
uvaaji, Ben alikuwa amevaa mavazi ambayo huenda kwake yalikuwa stahiki kutokana
na uchumi lakini machoni alionekana kama mshamba, shati kubwa kumzidi viatu vya
ngozi ngumu visivyong’ara na suruali nayo ilimpwaya laiti kama zisingekuwa
jitihada za mkanda wake kiunoni ingeweza kumwadhiri wakati wowote.
Hilo Caro alilimezea…..akaliona
jingine wakati wa kula. Ben hakuwa akifahamu kutumia Uma na kisu katika kula
chakula, alihangaika sana kula nyama laiti kama asingekuwa Caro huenda angenawa
na kutumia mikono. Kama hiyo haitoshi kila Ben alivyotupia tonge mdomoni
alikumbwa na ugonjwa unaowakabili waswahili wengi.
Ugonjwa wa kutafuna chakula huku
mdomo ukiwa wazi….
Ben hakuwa na staha hiyo…..
Walizungumza mengi baada ya
chakula. Caro akasema hili na Ben akaongezea lile. Mara wagonge viganja vya
mikono yao mara wacheke vicheko vilivyojaa staha.
Ilikuwa saa kumi hatimaye
ikatimia saa tatu usiku.
Kila mmoja alikuwa kimya
wakitazamana. Kuna jambo Caro alikuwa ameliweka mezani. Jambo ambalo Ben
hakulitarajia….
Mapenzi!! …..Caro alijielezea
kuwa anampenda Ben.
Ben hakutaraji…hakika hakutarajia
jambo hilo hata kidogo.
Kupendwa na msichana mrembo wa
haja muhitimu wa chuo kikuu nchini Uganda. Mwenye kazi yake……
Hakika ilikuwa ngumu kuamini…..
Akatamani kusema ‘nakupenda pia’
akahofia kuonekana mwepesi kulaghaika….
Akataka aseme ‘nitakufikiria’
hili akaona ni jibu la kike kike…akalipuuzia.
“Ben…” Caro akaita kwa sauti
tulivu.
“Caro…” Ben akaitika….
“Nisamehe kama nimekukwaza…”
“Hapana Caro hujanikwaza
ila….ila….ni kama siamini yaani….”
“Kwanini Ben sifananii ama.”
“Mimi ni masikini ujue, na
nimekueleza maisha yangu. Usidhani nimekutania hata jambo moja, yaani maisha
yangu ni magumu wewe…acha tu Caro yaani hata chakula na….”
“Pliiz Ben…hayo ni mengineyo.
Nakupenda ndo jambo ambalo nimelileta mezani.” Caro akamkatisha.
“Caro sidhani kama nina hoja ya
kupingana nawe…sikuwa na mpenzi kwa muda mrefu…sikuwa na wazo la kuingia katika
mahusiano, nikisema nipo tayari namaanisha hayupo atakayeumia hakuna
nitakayemsaliti…..NIPO TAYARI CARO.” Hatimaye Ben akajitia ujasiri akazungumza.
Sauti yake ya upole ilivutia kuisikiliza japo ilihuzunisha.
Usiku huu ukawa wa aina yake.
Wakaongozana hadi nyumba anayoishi Ben. Licha ya Ben kumzuia sana Caro asifike
‘geto’ kwake, binti yule aligoma kabisa.
Walimkuta Raphael akiwa
amejilaza. Chumba kilikuwa na giza na mbu walishindana kupiga miluzi. Caro
hakujali. Aliingia. Taa ikawashwa. Rapha akawakaribisha.
“Rapha mambo…” Caro akawahi
kujipa uenyeji. Rapha akatabasamu.
“Poa shem..” akajibu. Ben akaona
aibu akainama. Mazungumzo ya hapa na pale, kisha Caro akaaga.
Usiku huu ulikuwa wa mwisho kwa
Ben kulala kwa shida.
Caro akamkaribisha nyumbani kwake
maeneo ya Mbezi ya kimara.
Rapha akapatiwa pesa kwa ajili ya
kupanga chumba kingine ama kukiboresha chumba alichokuwa anaishi.
Ben akaanza maisha mapya akiwa na
Caro kama mpenzi wake.
Mambo yalienda upesi upesi. Ben
akanunuliwa nguo zilizoendana na mwili wake, akalipiwa ada katika kituo cha
kufanyia mazoezi ya viungo. Kila baada ya kutoka katika mazoezi ya viungo
alikuwa anaingia kujifunza kuendesha gari.
Mazoezi yakamkubali kifua
kikatanuka, mikono ikajaa nguo nazo zikamkubali. Caro akakiri kuwa Ben alikuwa
mtanashati haswa. Jambo hili lilimpa furaha kubwa maana alipolenga ndipo
penyewe haswaa.
Ben hakuachwa awe baba wa
nyumbani ndani ya miezi miwili ya mapenzi motomoto alikuwa amefunguliwa duka la
kuuza spea za magari, mitaa ya Msimbazi Kariakoo. Biashara ambayo aliimudu
vyema.
Haikupita siku bila Ben
kuzungumza na mpenzi wake kuhusu biashara inavyokwenda…..alikuwa mkarimu na
mwenye maadili.
Ni jumapili pekee ambayo hakuwa
akienda kazini. Siku hii waliitumia kuhudhuria ibada kanisani na kutoka kidogo
kwa ajili ya kujiburudisha. Walipendeza kuwatazama.
Wakati huo alikuwa anaendesha
gari yake aliyopewa na Caro lakini kadi haikubadilishwa jina ilibaki kuwa mali
ya Caro na hakuna aliyejali.
Ben akawa jamali wa sura kutokana
na chakula kizuri na upungufu wa mawazo kichwani.
MWEZI WA NNE tangu waanze kuishi
pamoja Ben aliyekuwa na pesa za kutosha katika akaunti yake akaanza visa, mara
achelewe kurudi nyumbani. Mara alalae kwa rafiki zake ambao Caro hakuwajua.
Caro alipouliza majibu yakawa ya mkato.
“Mpenzi leo ni siku ya ibada…”
“Wewe ndo Yesu ama?” Ben alijibu
bila kujali lolote.
Zamani simu ya Ben ilikuwa simu
ya Caro lakini sasa aliweka ‘password’ na hakutaka kujibu kwanini amefanya
hivyo. Zamani simu zilizopigwa alizipokea bila shaka lakini sasa akawa
anachagua simu za kupokea.
“Mbona simu inaita unakata.” Caro
alihoji.
“Simu yako imekushinda unahamia
kwenye simu yangu.” Alijibu kwa jeuri. Kisha akatoweka sebuleni
Caro aliugundua mchezo ule jinsi
ulivyokuwa unaenda lakini alijiweka katika upande wa mwanamke mstaarabu
hakutaka shari. Akauliza kistaarabu sana na hata alipojibiwa kwa shari hakuacha
kumwekea mpenzi wake maji bafuni.
Siku moja alihoji……
“Baba Caro….kuna jambo nahitaji
kuzungumza nawe.”
“Nakusikiliza.”
“Ni kuhusu kuoana…” Caro alisema.
Ben akashtuka hakutegemea hoja ile...
“Bado mapema Caro….yaani hata
mwaka hatujafikisha aisee.”
“Umeniitaje?” Caro alishtuka kwa
mara ya kwanza katika uhusiano wao Ben anamuita kwa jina lake la kuzaliwa
wakati walizoea kuitana, ‘mama Ben’ na ‘baba Caro’.
“Nimepitiwa tu…” alijibu bila
hofu. Caro akakaa kimya.
Caro akajikunyata kama kuku
aliyemwagiwa maji ya baridi. Lakini kichwani akitafakari mengi, alikuwa
akimtafakari Ben huku akitafakari na swali alilotoka nalo Uganda. Aliona kama
jibu linakaribia.
“Maana nina mimba kwa sasa…” Caro
alimweleza baada ya kunyanyua kichwa.
“Car…aah mama Ben,,una
mimba…mimba ya nini kwa sasa, unataka tupate mtoto nje ya ndoa….” Aling’aka
Ben. Caro hakusema neno kwanza akatulia.
“Mara yetu ya mwisho kutumia
kinga ni lini unakumbuka.” Caro aliweka msumari. Ben akagundua kuwa tangu
wapime na kujikuta hawana virusi hawajawahi kutumia kinga. Soni ikamshika.
KITENDO cha Ben kusikia Caro ana
mimba ndo kilimuhamisha kabisa nyumbani. Akawa hakosi kuhudhuria kwa Zulfa,
msichana kigoli aliyekuwa amemdatisha. Kila alichokuwa anasema Ben alitii,
karibia kila siku alipomtembelea alimwachia shilingi lakini moja hadi moja na
nusu. Pesa ilikuwepo kwa nini asimwachie. Alifanya yote haya kwa jeuri ya pesa.
Pesa ambayo amesahau chanzo chake.
MWEZI WA TANO wa mahusiano hali
ilizidi kuwa tete. Ben akawa na sauti kuu zaidi katika nyumba, Caro akakosa
amani, kila mara alikuwa anagombezwa bila kujalisha ni katika simu ama ana kwa
ana. Ben alikuwa kama kichaa. Mara akagundulika kuanza kutumia pombe, akawa
muhudhuriaji mzuri wa kumbi za starehe zinazosadikika kuwakamua watu wengi pesa
hapa mjini. Huko kwenye hizo kumbi Ben akawa mpenda sifa aliwatuza wacheza shoo
na waimbaji. Kibaya zaidi Ben akakumbwa na tamaa ya kutembea na wasichana
warembo, hakuwakosa kwa sababu alikuwa na pesa wakajikosha akafanya nao
mapenzi. Maisha yakaendelea.
Caro alipogundua hili akaamua
kuwa makini. Hakuna mapenzi bila kinga la sivyo hakuna kufanya kabisa. Hali hii
ikamkera Ben akazidi kujikita kwa kimada wake. Hilo nalo Caro aliligundua
kupitia kwa marafiki wa Ben wenye tabia za kishakunaku. Ilimuuma sana lakini
alifurahi kwa sababu alikuwa analipata jibu.
MWEZI WA SITA alimbadilikia Ben,
akaanza kuwa mkali na muulizaji wa kila kitu kinavyoendelea. Ben hakutaka kutoa
ushirikiano alikuwa jeuri na asiyeshaurika. Hata Rapha alikuwa amegombana naye
tayari na Ben hakujali lolote kwa sababu alikuwa na pesa. Aliamini kuwa pesa ni
kila kitu kwake…
Caro alipohoji juu ya ugomvi wake
na Rapha kwa mara ya kwanza akajikuta akipokea kipigo kutoka kwa Ben, kipigo
kitakatifu. Masikio yake yalisikia akiitwa jina baya ‘MALAYA’, Caro amekuwa
Malaya?
Hakika aliumia lakini bado
alitabasamu moyoni maana alikuwa anazidi kulipamba jibu lake…
Zilikuwa zimebaki siku kadhaa
mkataba wake wa mkiezi sita katika nyumba ile uweze kumalizika na hakuwa na
mpango wowote wa kuongeza muda wa kuishi pale na mwenye nyumba alitambua hilo.
Kila kitu ndani ya nyumba ile kilikuwa mali ya mwenye nyumba. Ni nguo pekee na
vitu vingine vidogo vya ziada ndo vilikuwa vya wapangaji.
Hizo ni aina ya nyumba za kupanga
jijini ambazo malipo yake huwa makubwa sana na mara nyingi familia za kitajiri
humudu…..
Ni nyumba ambazo huna haja ya
kuhangaika kuhamisha mizigo mingi wakati wa kuhamia na kuhama.
CARO alijikusanyia kilicho chake.
Kwa sababu lilikuwa jambo la kawaida sana Ben kuacha kurudi nyumbani hata kwa
siku tatu bila taarifa….Caro hakuhangaika. Alifurahi kuyakuta magari yote
mawili yakiwa uani. Ben hakuondoka na gari siku hiyo….
Caro akapiga simu kwa watu
aliofahamiana nao. Wakayaondosha magari na mizigo yake kidogo pamoja na nguo
nyingi za Ben. Akamuaga mwenye nyumba na kumkabidhi funguo zake.
SIKU iliyofuata ndege ikatua
katika uwanja wa kimataifa nchini Uganda.
Caro akapokelewa na marafiki zake
waliokuwa na shauku ya kuonana naye tena. Wote walingoja majibu kutoka kwa
binti huyu.
Caro hakuwa na papara. Walipofika
mahali tulivu alianza kuwasimulia. Walianza wao kumkumbusha swali aliloondoka
nalo.
“UTAITAMBUA VIPI TABIA HALISI YA
MWANADAMU?”
Caro Mduma akatabasamu. Kisha
akatoa majibu kwa utaratibu.
“Ukitaka kumjua vyema mwanadamu
tabia zake mpe pesa, pesa za kutosha utamfahamu vyema. Mngemuona huyo Ben
wallah msingeweza kumdhania kama anaweza kubadilika…alikuwa mshamba hajui kuvaa
na mtaratibu tena mnyenyekevu mno. Sijui nilivutika nini kuamua kumtumia katika
kulijibu swali langu lakini niliamua kuwa naye. Mwanzoni alikuwa ana mapenzi ya
kweli hauwezi amini kidogo mwenzenu nishawishike kuwa awe mpenzi wangu wa
maisha kwa jinsi alivyonicare, yaani alikuwa ni husband kweli lakini mambo
yakabadilika baadaye. Akageuka mbogo baada ya pesa kumzoea…mshenzi sana kumbe.
Nilimzuga nina mimba akaonekana kama anataka kuikataa…..nikamdanganya tuoane
yote hayo akakataa, nilikuwa namfuatilia sana viwanja zake. Hakuna mtu anapenda
sifa kwa wasichana kama Ben, Ben alinyanyua mikono akanibamiza baada ya
kumuuliza kwanini amegombana na rafiki yake…, hakuna mwanaume limbukeni kama
yule, alitekwa na manzi mmoja hata Yule msichana alikuwa mbaya class kwetu
anamzidi. Akawa anampatia pesa kila leo….eti akagombana na rafiki yake
aliyekuwa anamuhifadhi kwa room yake. Akadhani mimi mjinga kumbe nipo katika
kutafuta jibu. Nimemwacha solemba. Sijui atachanganyikiwaje tu….amebaki na
biashara yake hiyo ndo zawadi kwa kunisaidia kupata jibu. Yaani ningekuwa
nimempenda kweli sijui nini kingehappen….” Caro alimaliza. Kila mmoja alikuwa akimtazama
katika namna ya kumshangaa. Lakini wakaelewa azma yake. Hakika alikuwa
amelipata jibu kwa vitendo.
MWISHO.
Post a Comment