Mwanamfalme wa Uingereza, Prince William amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikishwa katika shughuli za uhifadhi wa maliasili kwa kupatiwa elimu zaidi ya masuala ya uhifadhi ili isaidie katika mapambano dhidi ya ujangili nchini.
Mwanamfalme huyo ambaye yupo katika ziara nchini ametoa wito huo leo alipotembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi ambako ameelezea kufurahishwa na vivutio vilivyoko katika hifadhi hiyo na kuridhishwa na jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuishirikisha jamii kwenye shughuli za uhifadhi na kupambana na ujangili.
Mwanamfalme William amewasili katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi leo mchana na kulakiwa na wenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Same, Mh. Rosemary Senyamule, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Dk. Allan Kijazi, Mkurugenzi wa Mradi wa Faru – Mkomazi, Tony Fitzjohn, na Mkuu wa Hifadhi ya Mkomazi, Abel Mtui.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Dk. Kijazi amemweleza Mwanamfalme William kwamba TANAPA imeweka mkazo katika kushirikisha jamii zinazozunguka hifadhi katika uhifadhi wa maliasili kwa kutoa elimu ya uhifadhi, kushirikiana katika kuanzisha na kuimarisha huduma za kijamii kwa kuangalia vipaumbele vya jamii husika na pia kuwaunganisha na mamlaka mbalimbali katika kutatua changamoto zao katika masuala mtambuka.
Aidha, Dk. Kijazi amemweleza Mwanamfalme William juu ya ongezeko la idadi ya hifadhi za taifa nchini kutoka 16 zilizopo sasa hadi 21. Hifadhi hizo zilizopo mkoani Kagera zipo katika mchakato wa kurasimishwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mh. Rosemary Senyamule amesema wilaya yake ipo kwenye mchakato wa kutengeneza mpango mkakati wa kutangaza utalii wa maeneo ya wilaya ya Same ambapo Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Mkomazi ni sehemu ya maeneo hayo.
Mwanzilishi mwenza na Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Faru - Mkomazi Tony Fitzjohn ambao unafadhiliwa na Tusk Trust ya Uingereza ambayo Mwanamfalme William ni mlezi wake, amesema idadi ya wanyama hasa Faru katika hifadhi ya Mkomazi inaongezeka kila mwaka kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau katika kuboresha mazingira ya hifadhi hii.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi amitaja moja ya changamoto inayoikabili Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuwa ni ukame unaosababisha upungufu wa maji, hatua inayosababisha wanyama kukimbilia nje ya hifadhi kutafuta maji na kuwa na mwingiliano na shughuli za binadamu.
Mwanamfalme William anatembelea Tanzania kwa mara ya pili ambapo mara ya kwanza alitembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na Pori la Akiba Selous miaka 20 iliyopita na amesema atatembelea Serengeti siku za usoni.
Post a Comment