WARIDI LA MAPENZI
(Kutokana na Kisa cha Kweli)
Tukusuma Mpoki alikuwa amesimama
kwenye baraza la nyumba yake, uso wake ukiwa umekunja ndita, jasho
likimtiririka, na macho yake yakiwa yanabubujikwa na machozi. Alikuwa
amejifunga kanga moja tu kati ya eneo la kifuani na kiunoni na hivyo kuonesha
mapaja yake yaliyonawiri vizuri na hivyo kulidhirisha kwa kadamnasi umbo lake
lake la nyigu. Chini ya kanga hiyo alikuwa amevaa chupi ya rangi nyekundu.
Licha ya upepo wenye joto la jiji hilo la bandari salama kumpulizikia bila
kukoma Suma aliendelea kusimama kwenye baraza la nyumba hiyo.
Hakujali watu
waliokuwa wamesimama upenuni wakimshangaa binti huyo wa Kinyakyusa akiwa katika
hali ya hasira na aliyekuwa akipaza sauti yake akimtukana mumewe bila kufunga
breki. Mkono wake wa kushoto uliokuwa umevikwa bangiri za rangi ya dhahabu
ulikuwa umekunjwa kwenye kiwiko na kuegeshwa kama gari la kijapani kwenye kiuno
cha binti huyo kilichokuwa kimehifadhi vyema mviringo wa makalio yake uliokuwa
kama vitunguu maji vinavyolimwa kule Tukuyu.
Mkono wake wa kulia ulikuwa umeinuliwa
juu, huku kidole cha kati kikining’inia hewani utadhani kimepigiliwa msumari
katika staili ya kumzodoa mtu. Kucha zake ndefu zilizopakwa rangi nyekundu
inayong’ara zilionesha ni jinsi gani Suma (kama alivyozoea kuitwa mtaani)
alivyokuwa anajijali. Nywele zake ndefu zilizosukwa kwa mtindo wa rasta
zilining’ia mabegani kama nywele za simba jike. Suma alikuwa amekasirika, na
hasira yake ilionekana wazi siku hiyo. Hakuna aliyewahi kuhisi kuwa dada huyo
anaweza kuweza kumpaka mtu hadharani namna hiyo.
“Toka hapa, unadhani mwanamme peke
yako” Alifoka binti huyo huku sauti yake yenye lafudhi ya mbali ya kinyakyusa
ikipasua anga la eneo hilo la Chang’ombe.
“Yaani kukupenda wewe ndio imekuwa
nongwa, mwanamme gani huridhiki, kama penzi langu hulitaki si uende huko huko
ulikolala jana, firauni mkubwa, kama unafikiri huyo malaya wako anaweza
kukupenda kama nilivyokupenda sasa mbona umerudi hapa?” Aliendelea kubwata bila
hata ya kumeza mate. Sauti yake ikiwa kavu na isiyoonesha kujali nani
anasikiliza au nani anamuangalia. Watu walifurahia sinema hiyo ya bure.
Hatua kama kumi hivi toka mlango wa
nyumba yake ambayo ilikuwa ni ya mwisho ikipakana na nyumba za Polisi za
Chang’ombe alikuwa amesimama Sospeter Mkiru, mdomo umemdondoka utadhani
amemuona mzee Ole wa Usiku wa Balaa, na mkononi akiwa bado ameshikilia shati la
lilikuwa limechanika mgongoni baada ya Suma kulishindilia kucha za uhakika.
“Jamani Suma nisamehe mpenzi sitarudia
tena” Alisema Sosi huku maneno yake yakitoka kwa kukwamakwama kama maji
yanavyotoka kwenye mpira wa kumwaligia maua. Soni zilimshika. Alijikaza
kisabuni huku akibembeleza apewe nafasi nyingine.
“Nikusamehe mara ngapi nyang’au mkubwa
we!” Dada Suma utadhani ametiwa ufunguo aliendelea kumpaka. “Jamani hata
uvumilivu una mwisho. Mimi sasa basi, nenda huko unakokwenda kila siku
utanletea magonjwa bure miye”
“Tafadhali Suma nisamehe mke wangu”
Sosper alianguka na kupiga magoti kwenye mchanga uliokuwa unajoto. Alijaribu
tena kumbembeleza binti huyo.
“Nenda kafilie mbali, hayawani mkubwa”
Suma alisema huku akimwelekeza Sosi kwa kidole kuondoka hapo. Hayo yalikuwa ni
maneno ya mwisho ambayo Sospeter aliyasikia toka kwa Suma Mpoki. Alimuona Suma
akigeuka na kuelekea ndani ya nyumba.
Sosi alijua kuwa safari hii amevurunda
kweli kweli. Uchungu ulianza kumpanda pole pole na donge la hasira ya kumpoteza
waridi lake na mpenzi wake wa toka shule lilimkaba shingoni. Alijihisi kuwa
amejidhulumu penzi na anastahili adhabu hiyo kali. Alitamani amkimbilie Suma na
kujiangusha miguuni mwake na kumwomba radhi huku akijigaragaza. Akili yake
ilianza kwenda kwa kasi akijiuliza ni shetani gani lilimwingia hadi kumfanya
kwenda kulala na mwanamke waliyekutana kilabuni na kumuacha mpenzi wake wa
damu? Alijihisi kizunguzungu. Kama mtoto mdogo Sosi aliunganisha vidole vya
mikono yake kichwani huku shati lake akilibeba begani. Watu waliokuwa wamesimama
kushuhudia tukio hilo walianza kujipangua taratibu huku wengi wakimuonea huruma
Sospter na wengine wakisema wazi kuwa “amejitakia” mwenyewe.
Wachache
hawakuficha dhihaka yao kwani walimcheka hadharani na kumuona kweli huyo jamaa
wa kuja. Sospeter aliapa hatarudi tena mitaa hiyo kwa aibu aliyoipata
Chang’ombe. Akiwa haangaliki anakokwenda, Sosi alijikuta yuko katikati ya
barabara ya Chang’ombe huku magari yakijaribu kumkwepa, na watu wakimrushia
matusi ya kila aina hata matusi yasiyosajiliwa. Gari aina ya Fuso ambalo
lilikuwa limeshehena mashabiki wakitoka uwanja wa Taifa lilijitahidi kufunga
breki na kumkwepa kwa ustadi mkubwa. Sauti ya breki zake ziliumiza masikio ya
watu.
Mlio wa mshtuko wa watu ulitanda angani, huku watu wakishika vichwa vyao
na wengine kufumba macho wasione kile kilichokuwa kitokee.. Sospeter hakupata
nafasi ya kukwepa Fuso hilo, kwani alirushwa juu kama kopo tupu la kimbo.
Alipotua kwenye lami yenye mashimo mashimo, mwili wake ulikuwa hauna ishara
yoyote ya uhai ndani yake. Watu walikimbilia hapo kuangalia kilichotokea, huku
kina mama wakipiga kelele ya kilio wakiwaficha watoto wao wasishuhudie jambo
hilo.
Bila kusogea hata sentimeta moja, Suma
alijisemea moyoni “Ukome!” Suma aligeuka kwa haraka huku akiangua kilio
alichokuwa amekizuia kwa muda na kuingia ndani ya nyumba ambayo alikuwa anaishi
na wadogo zake. Mwili wote ulikuwa unamtetemeka huku hisia ya furaha ya kisasi
na hatia ya uovu vikimkaba rohoni. Moyo wake ulikuwa umejeruhiwa kwa mapenzi na
kumbukumbu ya mapenzi ilimuumiza mtima. Alijihisi amepoteza muda mrefu na
kijana Sospeter ambaye walikuwa wakiishi kama mume na mke. Alijidharahau na
kujiona kweli “amepatikana” kwa kukubali penzi la kijana huyo chakaramu. Aliapa
moyoni mwake kuwa hatopenda tena, kwani wanaume ni kama mbwa. Aliendelea kulala
kitandani huku ameukumbatia mto huku moyo wake ukipaza sauti ya kilio chake
mbele za Mungu. Aliendelea kulia hadi alipopitiwa na usingizi huku akiwaza
jinsi alivyokutana na Sosi kwa mara ya kwanza.
* * *
Ilikuwa mwaka 1992 kwenye mashindano
ya Umoja wa Michezo ya Sekondari Tanzania ngazi ya Mkoa ambayo kwa mara ya
kwanza yalikuwa yanafanyika kwenye shule ya Sekondari ya Karatu iliyopo
pembezoni mwa barabara iendayo mbuga maarufu ya Serengeti nje kidogo tu ya mji
wa Karatu. Wakati huo mji wa Karatu ulikuwa bado ni Wilaya ndogo katika mkoa wa
Arusha. Shule karibu ishirini za Sekondari kutoka kila kona za mkoa wa Arusha
zilikuwa zinawakilishwa kwenye mashindano hayo ambayo hatimaye yangeteua timu
ya mkoa ambayo ingewakilisha mkoa wa Arusha katika mashindano ya UMISETA
yaliyokuwa yanafanyika baadaye mwaka huo huko Morogoro.
Sospeter alikuwa ni
golikipa namba moja wa timu ya Soka toka shule ya sekondari ya Singe iliyoko
Babati. Sifa zake zilienea kwenye mashindano hayo kwani aliokoa penati tano
katika mechi mbalimbali ambazo ziliifanya timu yake kushiriki katika mashindano
hayo. Hata hivyo sifa hizo hazikumfanya awe anajipendekeza au kujiona yeye bora
zaidi. Nje ya uwanja alikuwa ni kijana mcheshi, mwenye kupenda utani, lakini
anayeheshimu kila mtu. Akiwa kwenye lango alikuwa ni tishio kwa timu ya ugeni
kwani alikuwa na manjonjo ya Juma Pondamali na udhibiti wa goli wa Idi Pazi.
Alikuwa na mbwembwe golini kiasi cha kuwafanya washambuliaji wa timu ya ugeni
kupenda kujaribu mashuti ya mbali kwani wakimsogelea huwa anawazogoa na
kuwatania kiasi cha kuwafanya wakasirike na hivyo kushindwa kutilia mkazo
ufungaji magoli. Kwa mtindo wake huo watu walimfananisha na aliyewahi kuwa
golikipa wa Coastal Union, Duncan Mwamba.
Upande mwingine kulikuwa na timu ya
Netiboli toka shule ya Sekondari ya Kilutheri ya Dongobesh wilayani Mbulu. Kati
ya shule zote zilizowakilishwa kwenye mashindano hayo timu ya Dongobesh ndiyo
ilionekana kutoka mbali zaidi na wachezaji wake kuonekana ndio washamba zaidi.
Hata hivyo watoto wengi wa wakubwa ambao walikuwa watundu huko mijini walitupwa
huko kwenye shule hiyo ya bweni iliyozungukwa na kijiji cha kale cha Dongobesh.
Timu yao ya Netiboli ilikuwa inacheza vizuri lakini sifa kubwa ilikuwa
inatokana na dada aliyekuwa akicheza nafasi ya senta, alikuwa ni gumzo hapo
Karatu.
Kwanza kwa sababu ya uzuri wake na umbo lake la kimalaika. Wenyewe
walimpachika jina la Angel hadi wengine walidhania ndio jina lake halisi.
Alikuwa na mvuto wa ajabu kwa wavulana na wasichana. Lakini pamoja na sifa zake
zote Suma alikuwa anaakili darasani na tangu aingie shule ya Dongobesh hajawahi
kushika nafasi chini ya pili. Alikuwa akipishana na kijana mmoja ambaye baadaye
alijulikana kwa kazi yake ya uandishi, hadithi, na utunzi mbalimbali kwenye
mtandao wa kiintaneti.
Dongobesh walikuwa wanacheza mechi ya
mwisho dhidi ya timu ya Madunga ambayo ilikuwa ni mpinzani wa jadi. Sospeter
kwa kuitikia mwito wa rafiki zake waliokuwa wanamsifia Suma aliamua kwenda
kuangalia mechi hiyo, siyo kwa ajili ya kuona nani atashinda bali kuona kama
kweli hizo sifa za Suma zilikuwa ni za kweli au ni porojo tu za kwenye Umiseta.
Alipofika na kumuona jinsi binti huyo alivyokuwa anapendeza katika mavazi yake
ya netiboli ambayo yalimfanya aonekana kama amepotea toka Mbinguni na wanamtafuta,
Sosi alijikuta akimkodolea macho dada wa watu utadhani ameona hazina ya mfalme
Solomoni.
Sosi hakutaka kuangalia kitu kingine chochote na alijikuta anaungana
na wadau wengine kushangilia kila Suma alipokuwa akitoa pasi na kudaka mpira.
Mara mbili alijikuta anagonganisha macho yake na Suma ambaye na yeye alianza
kumwangalia na kila akidaka mpira basi anaweka madoido kidogo kumlingishia Sosi
(kama ilikuwa kweli au hayo ni mawazo ya Sosi tu miye sijui).
Mechi iliisha kwa timu ya Dongobesh kushinda na furaha kubwa
ilitawala upande wa mashabiki wa Dongobesh wakiongozwa na shabiki
aliyejipachika Sospeter Mkiru. Ilikuwa ni furaha kubwa kwani timu ya Dongobesh
haijawahi kuifunga Madunga kwa miaka mitano mfululizo hivyo ilikuwa ni furaha
kwa mwalimu wa Michezo Michael Tluway wa shule hiyo. Aliyekuwa na furaha zaidi
ya Sosi alikuwa ni matroni wao Vera Akonaay. Wakiwa katika shamrashamra za
kusherehekea Sospeter alitembelea kumwelekea Suma aliposimama mbele yake
alijikuta ananyosha mkono wa pongezi kwa kapteni huyo wa Dongobesh.
“Hongera Sana kapteni” alisema Sosi huku moyo ukimwenda kasi
utadhani aliyefukuzwa na simba mwenye njaa.
“Asante sana” Alijibu Suma huku akijaribu kuachilia mkono wa
Sosi ambaye alikuwa kama amemng’ang’ania.
“Umecheza vizuri kweli” alijikuta akisema maneno yasiyo na
kichwa wala mguu.
“Ndiyo, ila kulikuwa na mtu ananikodolea macho utadhani
amepoteza kitu na mimi nimemfichia” Alisema Suma huku mikono yake akiifunga
pamoja kifuani. Sosi alishindwa kujizuia kuangalia kifua cha Suma ambacho kilikuwa
kimetuna kwa matiti yaliyolala kama paa nyikani na kama midomo ya hua wawili
chuchu zake zilionekana kwa mbali. Sosi alimeza fundo la mate kwa aibu.
“Wala usisema maana nilichopoteza nimekipata” Alisema huku
akijikaza. Waliweza kuona macho ya watu yakiwaangalia imekuwaje watu hao wawili
wazungumze. Na vijana wengi walishangazwa ni jinsi gani Sosi alikuwa na ujasiri
wa kuzungumza na binti mrembo kama huyo. Wengine walikiri kuwa kama kulikuwa na
mwanafunzi yoyote kwenye mashindano hayo ambaye angeweza kumsimamisha Suma basi
alikuwa ni Sospeter.
“Umekipata? Na ulipoteza nini?” alihoji Suma huku macho yake
yakimganda kijana wa watu. Moyoni alijisemea kuwa alikuwa ni kijana mzuri,
msafi, na jasiri maana vijana wengi walikuwa wanaogopa hata kumsalimia. Walijiona
hawafai mbele zake.
“Nimepoteza akili yangu baada ya kukuona, na nadhani nimepata
mke kwa maisha yangu yote” Kama mtu aliyepagawa pepo wa mahaba Sosi hakujua
maneno hayo yametoka wapi, maana yalibubujika kama chemchemi ifukayo maji ya
mapenzi.
“Wacha we!, yaani kuniona tu umeona na mke kabisa!?” Aling’aka
Suma huku akikunja uso wake kwa kushangaa na kwa kukutwa hakujiandaa kwa maneno
hayo. “Usiniambie umeshaona na watoto na wajukuu?” Aliendelea huku akiangua
kicheko.
“Tena watatu, wawili mapacha” Alisema Sosi huku akihesabu kwa
vidole vitatu kwanza, kisha viwili. Suma aliendelea kucheka huku akishikilia
mbavu zake kwani hajawahi kukutana na mvulana aliyejua anachotaka kama huyo.
Mara mmoja wa wanatimu wa Suma walimuita ili waende kubadili nguo na kujiandaa
kwa chakula cha jioni.
“Ungependa kula na mimi na tupige soga zaidi” Aliuliza Sosi
kabla Suma hajakimbia.
“ah..wenzangu wataningoja” alijibu Suma
“Hapana, tunaweza kwenda kijijini na kununua cha hotelini, mie
leo sili dona lao” alijibu Sospeter huku moyoni akiombea kwa miungu yake Suma
akubali.
“We, tutawezaje kutoka kambini si ni kujitakia matatizo? Huoni
geti kali?”Aliuliza kabla hajakubali baada ya ushawishi wa Sosi. Sospeter alimhakikishia
kuwa hawatagundulika na wakakubaliana wakutane saa moja baadaye kwenye lango
kuu la shule. Sospeter alianza kutafuta njia ya kuweza kutoka na kurudi jioni
hiyo bila kujiletea matatizo yeye mwenyewe na Suma.
Baada ya kuhangaika kufikiri nini cha kufanya aliamua kwenda
kwa mzee mmoja wa Kimang’ati aliyekuwa zamu kulinda lango la shule hiyo. Wala
hakumchelewesha alimpatia shilingi mia tano na kumuomba chonde chonde amruhusu
yeye na Suma waweza kwenda na kurudi kabla ya muda wa kulala ambao ilikuwa ni
saa nne kamili za usiku. Mzee wa Kimang’ati kumbe hizo zilikuwa zake.
Alizifinyanga hizo pesa kiupole na kuziweka mfukoni. Alimwambia akiwaona
wanakuja basi atajifanya anazunguka upande wa pili na geti atalisogeza upande
kidogo tu. Na kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Sosi na Suma walipofika hapo
majira ya moja za jioni wakati giza ndio limeanza kuingia kwa nguvu na
kunyamazisha sauti za ndege yule mlinzi alizunguka upande wa pili wa kibanda na
kujifanya hakuona kitu na pale tu walipotoka alifanya haraka kufunga geti kwa
kufuli. Alikaa kuwasubiri warudi.
ITAENDELEA.................................................

Post a Comment