Wajumbe wa Baraza la Maadili wafanya Ziara Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma | Tarimo Blog

Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst) Harold Nsekela ( wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Maadili walipofanya ziara yao katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu Dodoma hivi karibuni kwa lengo la kujifunza. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji (Mst) Ibrahim Mipawa akifuatiwa na Immaculate Ngwalle na kushoto kwa Kamishna, Peter Ilomo.Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst) Harold Nsekela akitoa neno la ukaribisho kwa Wajumbe wa Baraza la Maadili waliotembelea Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma makao makuu Dodoma hivi karibuni. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na watendaji wengine wa Sekretarieti ya Maadili.Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Harold Nsekela ( wa pili kushoto waliokaa) na Watendaji wengine wa Sekretarieti ya Maadili wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Maadili wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji (Mst) Ibrahim Mipawa (kushoto kwa Kamishna) mara baada ya kuhitimisha ziara yao ya siku moja katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jijini Dodoma.
KAMISHNA wa Maadili, Jaji (Mst.) Harold  Nsekela amewatambulisha rasmi  Wajumbe wapya wa Baraza la Maadili  kwa Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili  ya Viongozi wa Umma mapema mwezi huu.
Wajumbe  hao wapya  wa Baraza la   Maadili waliteuliwa hivi karibuni na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ni pamoja na  Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Ibrahimu Mipawa, Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Bibi Immaculate   Ngwalle na Katibu Mkuu Mstaafu, Peter Ilomo ambao ni Wajumbe wa Baraza hilo.
Jaji Harold  Nsekela katika  hotuba yake ya utambulisho wa wajumbe hao kwa Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alisema  kuwa hili Baraza ni la awamu ya tatu tangu kuundwa kwa Baraza la Maadili ambapo Awamu ya kwanza ya Baraza   Mwenyekiti wake alikuwa ni Mhe. Jaji (Mst) Damian Lubuva na wajumbe wake ambao walikuwa ni Mhe. Jaji (Mst) Balozi  Msumi na Gaudius Tibakweitira na Awamu ya pili ya Baraza ilikuwa ni ya Mwenyekiti, Jaji (Mst) Balozi Hamisi Msumi  na Wajumbe wake ni Hilda Gondwe na Bibi. Selina Wambura.  
Nsekela aliendelea kufafanua kuwa Jukumu kuu la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ili kuhakikisha kwamba tabia na mienendo ya Viongozi wa Umma waliotajwa katika Fungu la 4(1) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na pia Misingi ya Maadili iliyoainishwa katika Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu ya Sheria hiyo vinazingatiwa.
“Misingi ya Maadili na Maadili yaliyotajwa katika Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu ya Sheria, inatoa miongozo ya tabia na misingi ya Maadili inayopaswa kuzingatiwa na Kiongozi wa Umma wakati anaingia madarakani, wakati awapo madarakani na anapoacha madaraka, alifafanua Nsekela.”
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, Jaji (Mst.) Ibrahim Mipawa alishukuru kwa  kupata mafunzo kuhusu Muundo na utendaji kazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Nashukuru kwa elimu tuliyoipata kuhusu Muundo wa Taasisi hii.  Natoa wito kwa Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na kuepuka mihemko mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Mipawa.
Baraza la  Maadili linaundwa  kwa Mujibu wa kifungu  cha 26(1) kinachosema kuwa  “kwa madhumuni ya Sheria hii  ya Maadili ya Viongozi wa Umma  Baraza litakuwa na watu watatu watakaoteuliwa  na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka  miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na  wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu na wengine wawili watachaguliwa  kwa ushauri wa Kamishna”.
Kazi ya Baraza la Maadili ni kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyowasilishwa mbele yake na Sekretarieti ya Maadili.
Aidha,  Baraza litafanya uchunguzi wake  hadharani, ila tu linaweza kuwazuia   waandishi wa habari, baadhi yao au wote  ikiwa linaona kuwa ipo haja ya kufanya hivyo  kwa ajili ya kulinda na kudumisha amani, utulivu  kwa uendeshaji bora wa mwenendo wa uchunguzi au kwa  sababu nyingine yoyote.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2