Charles James, Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi amepiga marufuku biashara zozote ndani ya wilaya hiyo ambazo hazina vifaa vya kujikinga na corona.
DC Ndejembi amewataka wafanyabiashara wote kuhakikisha wanaweka maji ya kunawa yanayotiririka, sabuni au vitakasa mikono ikiwa ni jitihada za kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu maarufu Corona.
Akizungumza katika mkutano wake na watendaji wa kata zote za wilaya hiyo, DC Ndejembi pia amewataka watendaji hao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ya namna gani ya kujikinga na ugonjwa huo.
" Sisi viongozi ndio wenye jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wetu, tuchukue hatua pia za kujua wageni wote wanaoingia ndani ya wilaya yetu ili kama akikutwa na maambukizi tujue tunaanzia wapi kujua watu aliokutana nao.
Tuna utaratibu wa kutambua mtu mgeni kuanzia ngazi ya nyumba kumi kumi, hivyo niwatake watendaji muwe makini na hilo, wageni wote wanaokuja kibiashara pia tuwajue, hatuzuia watu kuja kufanya biashara wilayani kwetu lakini ni vema tukachukue hatua muhimu za kujinga," Amesema DC Ndejembi.
Amewataka watendaji hao kutoruhusu pia mikusanyiko ya aina yoyote kwenye maeneo yao ili kujiepusha na maambukizi ya Corona.
" Hata nyie mnavyoenda kutoa elimu kwa wananchi siyo mnawakusanya eneo moja wote hakikisheni kunakua na umbali ili elimu mnayowapa ya kuepuka msongamano iakisi kwa vitendo, siyo unaenda kutoa elimu halafu unawajaza wananchi na kuwatarishia usalama wao," Amesema DC Ndejembi.
Pia ametoa maagizo kwa vyombo vyote vya usafiri vinavyofanya safari zake ndani ya wilaya hiyo kuwa na vitakasa mikono ili kila abiria anaeingia kunawa mikono yake.
Amewaagiza pia madereva wa bodaboda kuhakikisha wanakua na vitakasa mikono na 'mask' ikiwa ni njia mojawapo pia ya kujikinga na maambukizi hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi akizungumza na watendaji wa kata zote ndani ya wilaya hiyo katika mkutani wa pamoja wa kupeana maelekezo ya namna gani ya kuchukua hatua za kudhibiti maambukizi ya Corona.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment