DKT KALEMANI AAGIZA VIJIJI 11 SINGIDA MASHARIKI KUWASHWA UMEME NDANI YA MWEZI MMOJA | Tarimo Blog






Waziri wa Nishati Medard Kalemani akizungumza kabla ya kuwasha umeme katika vijiji vya Matare na Nkuhi vilivyopo jimbo la Singida Mashariki,kulia kwake ni Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akizungumza katika ziara ya Waziri wa Nishati Medard Kalemani jimboni humo.



Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani akitoa maagizo kwa wakandarasi wa umeme akiwa katika ziara wilayani Ikungi ambapo aliwasha umeme katika vijiji viwili vya Matare na Nkuhi.



Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu akizungumza mbele ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Mkuu wa wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo.



……………………………………………………………………………………………….

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Nchini(TANESCO)Mkoa wa Singida kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanaweka umeme kwenye Vijiji 11 vilivyopo Jimbo la Singida Mashariki.

Aidha ameiagiza TANESCO Singida kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi aanze kusimika nguzo mapema katika Tarafa ya Mungaa Lighwa,Ntuntu,Misughaa na Kikio ili umeme uwashwe kwenye Vijiji kabla ya mwezi June mwaka huu

Dkt Kalemani ametoa maagizo hayo wilayani Ikungi akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya umeme ambapo amewasha umeme katika vijiji viwili vya Matare na Nkuhi.

“Nampongeza Sana Mbunge wenu Mhe Miraji Mtaturu, kwani anafuatilia sana miradi ya wananchi wake,tangu amechaguliwa na kuapishwa ni miezi mitano tu lakini mnaona mambo yalivyo, leo tu tumewasha vijiji viwili je angekaa miaka minne hali ingekuwaje?,”alihoji Dkt Kalemani.

“Ndugu zangu Ugonjwa huu wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona(COVID 19)usikwamishe kazi za kuunganishia umeme wananchi ila mfanye kazi kwa tahadhari,tutaendelea kukagua miradi ya umeme kila mahali kwa kuwa wananchi wanahitaji umeme na Rais Dkt John Magufuli ameidhinisha sh Bilion 40 kwa Mkoa wa Singida ili kutekeleza miradi hii hivyo ni lazima tuisimamie,”alisema Dkt Kalemani.

Pamoja na hayo Dkt Kalemani amesisitiza wananchi kutolipishwa nguzo na gharama za kuunganishiwa umeme amesema ni sh 27,000 tu na sio vinginevyo.

“Katika hili niagize hapa mkandarasi wa Cyba Contractors Ltd ya jiji Mbeya aliyelalamikiwa kuwatapeli wananchi baada ya kuchukua pesa zao na hajafanya wiring mpaka sasa atafutwe,”aliagiza Dkt Kalemani.

Awali akizungumza katika ziara hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo amesema katika kata 28 zilizopo wilayani humo,ni kata 18 tu ndio zimefikiwa na umeme hivyo kumuomba waziri aendelee kuwasaidia.

“Mh Waziri kwanza nikupongeze na kukushukuru kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya umeme,wilaya ya Ikungi tulipewa Vijiji 30 na vimeshaunganishiwa umeme,lakini waswahili wanasema kushukuru ni kuomba tena,mh waziri naomba uendelee kutusaidia wananchi wa Ikungi tupate umeme katika maeneo yote,”aliomba mkuu wa wilaya hiyo.

Amesema katika wilaya hiyo viongozi wa serikali,chama na wabunge wote wawili wanafanya kazi kwa ushirikiano hali inayopelekea kurahisisha upelekaji wa maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake mbunge Mtaturu amemshukuru
Rais Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kwani aliahidi kuwafikishia umeme wananchi na utekelezaji wa ahadi hiyo unaonekana.

“Sisi wananchi wa Singida Mashariki na Ikungi kwa ujumla tunatoa shukrani za pekee kwake,miradi mingi tunaiona inatekelezwa,na tunaahidi kumpa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu ujao,”alishukuru mbunge huyo.

Amempongeza Dkt Kalemani kwa kumsaidia Rais Magufuli kusimamia sekta ya Nishati kwani miradi inaenda vizuri nchi nzima.

“Pamoja na shukrani hizo mh waziri Tarafa ya Ikungi kwenye vijiji vya Manjaru,Tumaini,Ng’ongosoro, Matongo,Kimbwi,Unyang’ongo na Mbwanjiki vipo barabarani havina umeme kwa muda mrefu pamoja na miundombinu kuwepo jirani,”aliongeza Mtaturu.

Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa ameipongeza serikali kupitia Rais Dkt Magufuli kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya chama hicho vizuri na kuomba Vijiji vilivyosalia vikamilishiwe kuwekewa umeme.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2