KAMPUNI YA GGML YATOA SHILINGI BILIONI 1.6 KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI MAPAMBANO DHIDI YA VIRUSI VYA CORONA | Tarimo Blog

 Baadhi ya wananchi wanaozunguka mgodi wa kampuni hiyo wakinawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, vifaa hivyo vimetolewa na GGML kudhibiti maambukizi ya Corona katika mji wa Geita
Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Richard Jordinson akifafanua jambo

KAMPUNI  ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa Shilingi bilioni 1.6 kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona ambayo hadi sasa yamesambaa katika nchi 210 duniani Tanzania ikiwemo.

Pia GGML imezindua mikakati kadhaa ya kupambana na janga la virusi hivyo vinavyosababishwa ugonjwa wa Covid–19 katika eneo lake la kazi na kwa jamii zinazozunguka mgodi wake.

Akizungumza kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa  vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Wayne Louw amesema katika fedha hizo, Sh bilioni 1.1 zitaelekezwa kwenye  ngazi ya kitaifa kupitia Mfuko Maalum wa mapambano dhidi ya Covid – 19 ambao unasimamiwa na ofisi ya Waziri  Mkuu.

Amesema fedha zingine Sh.milioni 500 zitatumika kwa ajili ya kusaidia juhudi zinazofanywa katika ngazi ya mkoa na jamii, zitakazojumuisha ununuzi wa vifaa-tiba muhimu na vitendea kazi kama vile vifaa vya kujikinga, barakoa, mashine za kusaidia upumuaji pamoja na mambo mengine

Aidha, amesema kuwa GGML kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) imeweka matanki 10 ya maji yenye uwezo wa kubeba lita 1000 kila moja kwa ajili ya kuwezesha watu kunawa mikono.

Amesisitiza kwamba  jukumu la GEUWASA litakuwa ni kujaza maji katika matenki hayoambayo yamewekwa katika maeneo  yenye watu wengi mjini Geita na kuongeza kuwa GGML pia itatoa dawa aina ya Chlorine ili kutakasa maji hayo, na kwa hiyo hakutakuwa na ulazima wa kutumia  sabuni.

"Matenki mengine yanaendelea kutengenezwa kwa ajili ya Watoto na watu wenye ulemavu.Nia yetu ni kuendelea na shughuli zetu kama zilivyopangwa na tunatumaini kwamba janga hili litakwisha hivi karibuni. Kwetu sisi, shughuli zetu zinajumuisha uzalishaji wa dhahabu na pia utekelezaji wa miradi ya kusaidia jamii  inayotuzunguka,” amesema.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya afya
mahali pa kazi, Dk. Kiva Mvungi amesema katika kujenga uelewa juu ya janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi, kampuni hiyo imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa  za virusi ndani na nje ya mgodi.

“Katika kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya uelimishaji kuhusu janga la Covid-19, GGML imeingia ubia na Rubondo  fm, ambacho ni kituo cha redio kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Chini ya ubia huu, Kampuni ya GGML inagharimia uandaaji wa tangazo, na kituo cha Rubondo fm kitatoa mchango wake kwa kurusha matangazo yanayohusu elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema Kituo cha Rubondo fm kilianzishwa kwa ufadhili wa GGML chini ya Mpango wa uwajibikaji kwa Jamii (Coroporate Social Responsibility) wa kampuni hiyo. “Tunafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali.

"Maofisa wetu wawili wameteuliwa na Mkuu wa Mkoa kuwa sehemu ya kamati maalum iliyoteuliwa kupambana na janga hili hapa Geita. Wawakilishi wetu hawa wanahakikisha kwamba mipango yetu ya kupambana na Covid – 19  inaendana na ile ya Serikali,” amesema Dk. Mvungi.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2