MGENI, MGENII MGENI HUYU MGENI, ANAUA WAZEE, VIJANA MPAKA WATOTO | Tarimo Blog

Charles James, Michuzi TV
MWANZONI mwa miaka ya 2000 Lejendi wa Muziki, Marehemu Kapteni John Komba na Bendi yake ya TOT waliingia 'booth' kurekodi ngoma waliyoipa jina la Mgeni.

Mgeni ulikua ni wimbo ambao ulimuelezea mgeni (Ukimwi) ambaye alikua ameingia kwa kasi nchini huku akiua watu kwa fujo. Wazee, Vijana hadi Watoto walikua wahanga wa mgeni huyu. 

Sogea hapa; Mwishoni mwa mwaka jana, Desemba 31, 2019 watu walikesha wakifurahia kuuaga mwaka huo na kuukaribisha mwaka mpya wa 2020.

Watu tukachinja Mbuzi, Jogoo, tukala Bia na bata vya kutosha tukijipongeza kuuona mwaka mpya. Kama ilivyo kawaida tukaongeza na hii, " This year will be my year," kwamba kila mmoja akisema huu ndio mwaka wake.

Mwaka wa mafanikio, mwaka wa kuoa na kuolewa, mwaka wa kumaliza shule. Mwaka wa kufungua biashara mpya. Hizo zote nilikua ni ndoto zetu. 

Lakini sasa mgeni ametuingilia, huyu siyo yule mgeni aliyemuimba Kapteni Komba. Huyu ni mwingine ambaye kaanzia huko Asia.

Mwanzoni tulimchukulia poa tukaona hawezi kuja Afrika. Tukatamba sana ooh Sisi Mafua ndo magonjwa yetu hayawezi kutuua. Kumbe huyu mgeni Corona alikua anatuchora tu.

Ghafla kaibuka nyumbani kwetu. Siyo kwa majirani tena tulipokua tunamuona kwenye Tivii..sasa upo kwetu, tunao nyumbani. Hali ni tete.

Mgeni huyu balaa sana mgeni hana adabu wala huruma. Mgeni roho yake mbaya hataki kutuona tukifurahi, hataki kutuona tukiabudu, anatufanya hata baadhi ya mikusanyiko ya kijamii tusiifanye.

Fikiria sasa hata uwanja wa Taifa hatuendi tena kumuona Meddie Kagere akizitesa nyavu za wapinzani wao, ni muda sasa hatujamuona Bernard Morrison akitembea juu ya mpira na jezi yake ya Yanga.

Shemeji zangu wa Lindi wananiambia wamemiss sana udambwi dambwi wa Lucas Kikoti na jezi yake ya Namungo FC. Ni purukushani tu, Ligi Kuu ya Tanzania imesimama. Raha iko wapi?

Tazama mashabiki wa Liverpool walivyo na wasiwasi, wanaumia haswa. Walibakisha alama sita tu watwae ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kitambo cha miaka 30 cha ukame wa kombe hilo.

Hawana amani tena mgeni ameingia England na ligi imesimamishwa. Uhakika wa ligi kurudi ni mdogo. Mgeni mbona 'mshenzi' hivi? Anataka watu walie?

Haya. Rafiki zetu wengine wanaoa mwaka huu, lakini hakuna sherehe, hakuna party kama watafunga Ndoa sherehe iwe ya kawaida ya watu wachache. Sasa raha iko wapi hapa? Hii yote ni vuruga za mgeni.

Misiba nayo tunazikana nje ya utaratibu wetu, watu wanaogopa kwenda kuzika wenzao maana mikusanyiko ndio inayosababisha pia maambukizi ya ugonjwa.

Tunakua wageni wa nani sasa? Maisha gani haya? Huyu mgeni si aondoke tu? Mwezi mmoja toka ameingia mateso yake kama miaka 10. Tumekoma Baba Corona tusamehe tunaomba uondoke.

Hebu angalia shughuli zinazohusisha wandishi wa habari visiwani Zanzibar zimepigwa marufuku. Kwa maisha yetu wandishi tunajuana bila press hali itakuaje? 

Huku bara hali ni kama hiyo tu, si tutaiepuka Corona halafu tufe na njaaa? 

Idadi ya watu wanaoenda kanisani imepungua maana masharti ya kitabibu ni kukaa umbali wa mita moja. Misikitini hali ni hiyo hiyo. Inamaana mgeni hataki Sisi tuzungumze na Mungu? Mgeni mbona roho yake mbaya hivyo?.

Wanafunzi wetu bado wataendelea kukaa nyumbani,hawaelewi lini watarudi shule maskini ya Mungu. 

Niwaombe wazazi wawasimamie tu vizuri huko majumbani na kuwaepusha na vishawishi vya Dunia. Maana mgeni huyu mgeni.

Kiukweli mgeni nshamchukia haswa, kwa sababu hata yeye mwenyewe hana upendo na sisi. Aende zake tu tushamchoka. Kitu gani linatunyima furaha?

Watu 88 mpaka sasa washatembelewa na mgeni, watu wanne washachukuliwa na mgeni. Hali ni mbaya ndugu zangu tufuate masharti ya kitabibu yanayotolewa na wataalam wetu wa afya.

Tufunge milango yetu kwa makomeo ya chuma ili mgeni asiingie ndani kwetu. Tuchukue tahadhari mgeni tayari yupo mitaani kwetu anaangalia mlango wa nani upo wazi aingie. 

Tuhakikishe tunanawa mikono yetu kwa maji yanayotiririka na sabuni au tutumie vitakasa mikono (sanitizer) tuepuke misongamano na mikusanyiko isiyo ya lazima ndugu zangu.

Tunapoona dalili zozote za mgeni basi tuwahi kituo cha afya haraka. Tusiishi kwenye mazoea ya kwenda dukani kununua panadol. Hali ni mbaya.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2