Kupongeza juhudi za Serikali dhidi ya Mapambano ya Mlipuko wa Maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona
Itakumbukwa kuwa katikati ya mwezi Machi mwaka huu Serikali ilitangaza mapambano rasmi dhidi ya maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona ambavyo hivi karibuni imekuwa ni janga kubwa duniani.
Serikali ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania kuanza kupata taarifa za uwepo wa wagonjwa wa maradhi hayo nchini na hivyo kuwataka Wananchi kuchukua tahadhari mbalimbali za kujikinga na maradhi hayo ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayotiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa Barakoa na kujiepusha na misongamano.
Kufuatia uamuzi huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inatambua na inaipongeza Serikali kwa uamuzi huo kwani ni hatua nzuri ya kulinda haki ya afya ya wananchi wake pia ni hatua muhimu katika kupunguza maambukizi ya maradhi hayo kwa jamii.
Kipekee kabisa Tume inaipongeza Wizara ya Afya na watendaji wake ikiwemo Madaktari, Manesi na Wahudumu wengine kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhamasisha, kuelimisha na kutoa huduma stahiki kwa wananchi ambao tayari wamepata maambukizi ya maradhi hayo.
Tume inatumia fursa hii pia kuwapongeza jumuiya za AZAKI na Wafanyabiashara waliojitokeza kuunga mkono kwa hali na mali jitihada za Serikali katika kupambana na maradhi hayo.
Aidha, Tume inaiomba jamii kutofanya mzaha na jambo hili, janga hili ni kubwa hivyo ni muhimu kuunga mkono jitihada za serikali kwa kufuata maelekezo sahihi yanayotolewa ikiwemo wale wote washukiwa wa maambukizi na wenye maambukizi kukaa Karantini kwa muda uliopangwa ili kuzuia maambukizi ya ndani yasiongezeke.
Mwisho, Tume inatoa ushauri kwa Serikali na jamii kama ifuatavyo:
1. Jamii iendelee kuzingatia maelekezo ya kujikinga yanayotolewa mara kwa mara na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
2. Tume inaomba wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya maradhi hayo.
3. Serikali iendelee kuchukua tahadhari hususani katika mipaka yetu ili kuzuia kuingia k
wa maambukizi mapya kutoka nje ya nchi.4. Tume inaiomba Serikali kuliangalia kipekee kundi la Watu wenye Ulemavu kwani wao wanahitaji msaada zaidi kukabiliana na mlipuko wa maradhi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kuwapatia taarifa sahihi kupitia njia sahihi, kwa mfano Viziwi wapatiwe taarifa kwa lugha ya alama na Watu Wasioona waandaliwe taarifa zao kupitia machapisho mbalimbali ya nukta nundu, kuwapa huduma bora za afya na kuwalinda dhidi ya unyanyapaa.
5. Tume inavishauri vyombo vya habari hususani Luninga vifuate mfano wa Shirika la Habari la Taifa (TBC) kwa kuweka kipengele cha msomaji wa habari wa lugha ya alama wakati wa kurusha matangazo yao ili Viziwi nao waweze kuelewa taarifa zinazorushwa na vyombo hivyo.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Jaji (Mst) Mathew Pauwa Mhina Mwaimu
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Aprili 16, 2020
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment