WATOTO WAMJIA JUU BABA YAO MZAZI BAADA YA KUTAKA KUUZA ARDHI YAKE ILIYOKO ENEO LA KIJENGE JIJINI ARUSHA | Tarimo Blog


Na Woinde Shizza ,ARUSHA

MGOGORO wa kugombea mali ikiwemo ardhi na majengo umeibuka katika familia ya Mzee  Saimon  Kamakia mara baada ya watoto wa mzee huyo kumtuhumu baba yao kutaka kuwapora ardhi ambayo waliachiwa urithi baada ya marehemu mama yao,  kufariki dunia.

Kuibuka kwa mgogoro huo umeonekana umevuta hisia za wakazi wa eneo la Kijenge na ndani ya Jiji la Arusha na umesababisha kuvuruga amani ndani ya familia hiyo.

Baadhi ya watoto wa Mzee Kamakia akiwemo Nusin Kamakia walidai hatua ya baba yao kutaka kupora maeneo yao imekuja baada ya mama yao kufariki dunia miaka mitano iliyopita ambapo baada ya mazishi baba yao alianza mipango hiyo kwa kuleta watu mbalimbali katika maeneo yao kwa kulenga kuwauzia ardhi yao.

Mtoto mwingine wa Mzee huyo aliyetambulika kwa jina la Bella Kamakia alidai kabla ya mama yao kufariki dunia baba yao alikuwa akiishi wilayani Loliondo na mwanamke mwingine na pindi baada ya mazishi ya mama yao ndipo matatizo yalipoanza.

Alieleza maara walipomzika mama yao baba yao alianza kuleta watu mbalimbali wakiwemo wanajeshi kwa lengo la kununua ardhi waliyoachiwa kama sehemu ya urithi wa mama yao.

"Marehemu mama yetu alipofariki baba alikuja kuhudhuria mazishi kutoka Loliondo na pindi tulipomaliza kumzika ndipo baba yetu akaanza kuleta watu wa kutaka kununua ardhi yetu ambayo tuliachiwa kama sehemu ya urithi wa mama yetu," amesema Bella

Hata hivyo,Henry Kamakia alidai wanaiomba Serikali kuingilia kati suala hilo kwa kuwa limesababisha usumbufu wa Mara kwa Mara ndani ya familia yao.

Akijibu malalamiko hayo Mzee Saimon Kamakia amesema kuwa ardhi inayolalamikiwa na wanawe ni mali yake kwa kuwa alitafuta kwa nguvu zake na hajawahi kutoa urithi kwa mtu yoyote.

Mzee huyo alifafanua jambo lililomchukiza mpaka kutofautiana na wanawe ni kitendo cha wao kushindwa kuhudhuria harusi ya mke wake mwingine baada ya mke wake wa awali kufariki.

"Wale watoto hakika wamenivua nguo kabisa kitendo cha wao kukataa kuja kwenye harusi yangu walinichukiza kabisa na wamenivua nguo," alisema Mzee huyo na kuongeza suala la yeye kutuhumiwa kuuza maeneo na wanawe si kweli kwa kuwa yeye anauza ardhi ambayo ni mali yake kihalali na endapo watoto hawafurahishwi na uamuzi wake wana haki ya kwenda kutafuta ardhi yao kwani wameshakuwa watu wazima.
Picha ikionyesha mzee Saimon Kamakia akiwa na mke wake mdogo siku ya harusi yao.
 Picha ikionyesha mzee Saimon Kamakia akiongea na waandishi wa habari
 
 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2