ULALE PEMA BALOZI MAHIGA, UPUMZIKE KWA AMANI JAJI AGUSTINO RAMADHANI | Tarimo Blog

Charles James, Michuzi TV

NIMEZIMA Televisheni. Sitaki kuangalia tena, nimejikuta nachukia kwanini niliwasha data asubuhi na kukutana na taarifa zilizouumiza moyo wangu.

Kama Taifa tumeumaliza mwezi Aprili vibaya sana. Tumeuanza mwezi Mei kwa uchungu na vilio. Ni nini hiki tunapitia? Ndio zile nyakati za Dhiki kuu zilizoandikiwa na akina Ellen G White?. Maumivu hakika.

Tazama. Leo asubuhi Rais Dk John Magufuli ametangaza kifo cha Mwamba wa Diplomasia, Kachero wa Kimataifa na Balozi wetu wa kudumu kunako Umoja wa Mataifa, Dk Augustino Mahiga.

Dk Mahiga amefariki akiwa njiani kuwahishwa Hospitali baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo. Huzuni!

Mahiga amefariki akiwa ni Waziri wa Sheria na Katiba..kabla ya hapo Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Kwa miaka zaidi ya 40 amekua ni mtumishi haswa wa serikali. Mtumishi wa Nchi hii.

Katika umri mdogo wa miaka 36 alikahimishwa madaraka ya kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Kwa umri wake kuteuliwa na Mwalimu Nyerere kushika nafasi hiyo maana yake Mahiga alikua ni kichwa kweli kweli.

Leo amefariki. Pumzi yake imekata, haongei tena, hanyanyuki tena. Hatotumwa na UN kusuluhisha migogoro sehemu mbalimbali duniani. Amekwenda. Hatutomuona tena. Inauma.

Huyu ndie ametufanya tuuanze mwei Mei kwa uchungu na majonzi. Rais, Mawaziri, Wabunge na makachero wenzake wanalia. Dunia inamlilia pia.

Nakukumbusha kuhusu Aprili. Hii nayo imetuacha na majonzi mioyoni mwetu. Tumepoteza watu wengi mashuhuri na wenye nafasi kwenye maisha ya watanzania wengi.

Jaji Mkuu Mstaafu, Agustino Ramadhani ndiye ambaye amesababisha nizime TV mchana huu. Nilikua natazama akiagwa kwenye viwanja vya Karimjee. Jaji Agustino hatutomuona tena.

Nimejaribu kuvuta kumbukumbu nani ambaye nimewahi kusikia sifa zake kama Jaji Agustino nimekosa kabisa.

Sikiza. Anazikwa leo akiwa ni Jaji Mkuu Mstaafu, Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi na zaidi akiwa ni Mchungaji wa kiroho. Mwanaume wa namna gani huyu Jaji Agustino?!.

Maneno machache ya kusema ni Kwamba huyu alikua mmoja wa binadamu wachache nchini waliogusa maisha ya watanzania kwa asilimia kubwa sana.

Huyu anaondoka akiwa amehudumia Taifa hili kwenye kada mbalimbali. Ametugusa akiwa Jeshini, ametugusa kwenye haki mahakamani na kubwa kuliko ameokoa mioyo ya wengi kwa huduma yake ya kiroho kama Mchungaji.

Hakika Jaji Agustino ni mwanaume wa kukumbukwa nchini.

Sijasahau kama Mama Gertrude Rwakatare amefariki pia Aprili Mwaka huu. Mwanasiasa, Mfanyabiashara Tajiri na Mchungaji ambaye Kanisa lake la Mlima wa Moto lilikua kimbilio la wengi wenye shida.

Amewatetea watanzania kwa hoja zake mbalimbali bungeni, akatoa elimu bora kwa mamilioni ya watanzania kutokana na uimara wa shule zake za St Marys. Bado akawapa huduma za kiroho maelfu ya watanzania kanisani kwake.

Sijasahua kifo cha Mbunge wa Msemvu, Richard Ndasa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Mmanda. Hawa wote wamefariki April Mwaka huu.

UNAKARIBIA KUNIELEWA

Nataka kusema nini? Hiki ni kipindi ambacho kama wanadamu tunapaswa tujitafakari maisha yetu na utumishi wetu hapa duniani.

Usivimbe kichwa kwa madaraka uliyonayo, umaarufu wako hauna faida yoyote duniani kama hutendei wenzako mazuri. Haina maana ya kuwa na mamlaka yoyote kama utaonea wenzako.

Tazama leo watu wanazikwa na idadi inayopangwa na serikali kwa sababu ya hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona. Tena idadi ya watu 10 tu.

Kama siyo Corona leo pengine Karimjee pasingetosha wakati Jaji Agustino akiagwa. Viongozi wazito, majaji wenzake, wageni wa Kimataifa na waumini wake wangejazana kumuaga mpendwa wao.

Ni Corona iliyosababisha Mama Rwakatare aaagwe na watu 10. Tofauti na hapo msiba wake ungezungumzwa pengine kwa siku kadhaa kwa jinsi ambavyo ungejaza watu mashuhuri, maarufu na wale wenzangu na mimi.

Mbunge Ndassa amekua mbunge kwa miaka 25. Umri wa kijana mtu mzima mwenye mtoto. Lakini kaagwa na watu wachache mno. Wengi walitamani kumuaga mpendwa wao lakini haikuwezekana. Kwanini?

Corona imetupitisha sehemu ambayo hatujawahi kupita. Imetupa pia funzo zito na kubwa maishani mwetu. Imetukumbusha sisi ni binadamu na tunapaswa kuishi kama wote ni ndugu.

Haijalishi una fedha kiasi gani wala ni maarufu au tajiri kwa kiwango gani, tutendeane yale ambayo sisi tunapendaa kutendewa. Tusiumizane, tusitesane, sisi ni Tanzania moja.

0683 015145

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2