WAGANGA WA TIBA ASILI WAPATA MAFUNZO KUJIKINGA NA CORONA | Tarimo Blog

Mratibu wa Tiba asili na tiba mbadala wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akiongea jana na waganga wa Tiba asili na tiba mbadala wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua dalili na kujikinga na ugonjwa wa Corona wakati wote wa shughuli zao kama moja ya makundi maalum yanayoaminika katika jamii.


Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya tiba asili na tiba mbadala wa wilaya ya Tunduru Mohamed Nandule akiongea na waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutoka kata ya Mbesa wilayani humo ambapo amewataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili yao.




Baadhi ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutoka kata ya Mbesa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wakimsikiliza jana mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wendy Robert(hayupo pichani)wakati wa mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo juu ya kutambua dalili na kujikinga na ugonjwa wa Corona mafunzo yaliyofanyika katika kijiji cha Mbesa.
Picha na Mpiga Picha wetu

…………………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu,Tunduru

ZAIDI ya waganga 50 wa tiba asili na tiba mbadala kutoka kata ya Mbesa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wamepata mafunzo ya kutambua dalili na kujikinga kuhusu ugonjwa wa Corona.

Pia mafunzo hayo yaliwahusisha viongozi wa dini na viongozi wa kimila ambao wana mchangao mkubwa katika kukabiliana na adui maradhi hasa baada ya kubainika kuwa zaidi ya asilimia sitini ya Watanzania wanaamini tiba asili na tiba mbadala.

Katika mafunzo hayo waganga hao mbali ya kufundishwa namna ya kujikinga wao wenyewe,pia jinsi ya kuwakinga wateja wao pindi wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku.

Mratibu wa tiba mbadala na tiba asili wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, Hospitali ya wilaya imeona ni vema kuwapa mafunzo waganga hao ili nao waweze kushiriki vema katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hasa baada ya kuona kuwa ni miongoni mwa makundi maalum yanayoaminika na jamii.

Alisema, tiba asili ina mchango mkubwa katika kukabiliana na adui maradhi ambayo ni changamoto kubwa kwa nchi maskini na zile zinazo endelea ikiwemo Tanzania.

KIhongolea amewataka waganga hao kuepuka mikusanyiko katika vilinge vyao kwani inaweza kuhatarisha maisha ya wateja na badala yake kuweka utaratibu utakaosaidia kuwakinga watu wanaofika na hata wao wenyewe.

Kihongolea ameagiza kila mganga kuweka ndoo ya maji yenye sabuni katika kilinge chake na kuacha kulaza wagonjwa kwani vibali vyao haviruhusu kufanya jambo hilo na Serikali haitosita kuchukua hatua dhidi ya mganga atakayekutwa analaza wateja katika kilinge.

Alisema, baada ya mafunzo hayo watapita kilinge kwa kilinge ili kujiridhisha na kuona ushiriki wa waganga katika vita dhidi ya Corona na amewataka kufuata sheria na taratibu pale wanapofanya kazi zao sambamba na kutokumbatia wagonjwa wanaohitji tiba za Hospitali.

Aidha,amewapongeza waganga hao kwa ushiriki wao katika kampeni ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuwaibua wahisiwa wanaofika katika vilinge vyao na kuwapa rufaa ya kwenda Hospitali kwa ajili ya vipimo na matibabu jambo lilio saidia sana wilaya hiyo kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Roberty alisema, waganga wa tiba asili wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuzuia uwezekano wa kupata Corona kutoka kwa watu wanaofika katika vilinge vyao.

Alisema, waganga wanatakiwa kuepuka kuwaweka wateja wengi sehemu moja kwani ni hatari kubwa wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona

Pia amewashauri viongozi wa Dini kuangalia namna wanavyoweza kuchukua tahadhari na kuwashauri waumini wao kwenda na vifaa vya kuswalia(miswala) ambayo muumini atatumia pekee yake na kurudi nao nyumbani badala ya utaratibu wa waumini kutumia mswala mmoja watu wengi.

Alisema, serikali kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya imeweka utaratibu wa kuwapima wanaotoka nje ya wilaya na wanaotoka nchi jirani kwa lengo la kuzuia kuleta na kueneza maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona.

Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya tiba asili na mbadala wilaya ya Tunduru Mohamed Nandule amewaonya waganga hao kujiepusha vinavyokiuka maadili ikiwemo utapeli,uesharati na ulaghai ambao umekuwa chanzo cha baadhi ya waganga kutopata wateja.

Alisema, baadhi yao wamekuwa watu wa ovyo na kusababisha hata mifarakano katika jamii na kuwataka kufanya kazi zao kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo ili kuepuka kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2