Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo Ztitto Kabwe, kutotoa na kutoandika maneno ya uchochezi kwa muda wa mwaka mmoja.
Zitto amehukumiwa leo mahakamani hapo baada ya kutiwa hatiani katika mashitaka matatu yaliyokuwa yanamkabili.
Hukumu hiyo imesomwa leo Mei 29, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi 15 wa upande wa mashtaka na kuzingatia utetezi wa Zitto pamoja na mashahidi wake saba.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Shaidi amesema, maneno aliyoyatoa Zitto hayana ukweli, makali na magumu mno ambayo yameshindwa kuthibitishwa kwenye utetezi.
"Maneno ambayo hayana ushahidi wa kutosha, hakuna palipothibitishwa kwamba askari wamemuua nani na ushahidi unaonesha tukio lilifanyika alfajiri muda ambao huwezi kusema nani alimuua nani....," Maneno yalikuwa strong maneno serious watu 100 kufa sio kitu kidogo mpaka kutaja watu wa kabila fulani ...ni sawa na kuwasha moto kwenye nyasi kavu..." amesema Hakimu Shaidi.
Hakimu Shaidi ameongeza kuwa, jamii inawatu wenye uelewa tofauti kutokana na uwezo wa kuchuja maneno hivyo kila mmoja anaweza kuchuja maneno kwa kadri anavyoweza.
Hivyo Hakimu Shaidi amesema anamtia hatiani Zitto na kumtaka asiandike wala kutoa maneno ya uchochezi kwa muda wa mwaka mmoja.
"Ieleweke kuwa sisi sote Watanzania ...tumlee mama yetu amani hata ninyi wanasiasa mnawajibu mkubwa wa kumtunza, mmezoe kusema kwenye mitandao kuwa Mahakama ya kisutu imegeuka TRA... Hivyo mimi nakuhukumu kutoandika wala kutoa maneno ya uchochezi kwa muda wa mwaka mmoja"
Aidha Hakimu Shaidi amesema, kama kuna upande haujaridhika na hukumu hiyo milango ya kukata rufaa ipo wazi.
Awali Wakili wa Serikali Mkude aliiomba mahakama kumpatia Zitto adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa wengine.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Frank Mwakibolwa ameiomba mahakama kutotoa adhabu kali kwa kuwa mshtakiwa ni baba wa watoto wadogo wanne na kwamba hajawahi kuwa na rekodi za jinai kwenye mahakama.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa takribani mwaka mmoja na nusu, upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka aliyekuwa akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, huku Zitto akitetewa na mawakili Jebra Kambole, Frank Mwakibolwa na Bonifacia Mapunda.
Hata hivyo hukumu hiyo imesomwa na kupokelewa na Wakili wa serikali Mkuu, Renatus Mkude pamoja na wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon.
Aidha wakati wa kipindi cha usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka uliwasilisha mahakamani hapo vielelezo vya nyaraka na video iliyodaiwa kurekodiwa na askari mpelelezi (Sajenti James kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 28, 2018.
Video hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo Desemba 4, 2019, na kupokelewa baada ya mabishano ambapo upande wa utetezi ulitaka video hiyo isipokelewa lakini mwisho wa siku mahakama ilipokea ushahidi huo na video hiyo ilioneshwa.
Katika kesi hiyo inadaiwa tarehe 28 Oktoba 2018, Zitto aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.
Mshtakiwa anadaiwa alitamka kuwa “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua’’
Katika shtaka la pili ilidaiwa Oktoba 28, 2018, mwaka juzi maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’ lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya.
“Taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, hajatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa.’’
Ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema “tumekuwa tukifuatilia kwa kila yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment