BENKI YA DUNIA YATOA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 175,KULETA MAPINDUZI KATIKA ELIMU YA UFUNDI NCHINI | Tarimo Blog

  WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari.
 WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Benki ya Dunia imetoa mkopo wa  Sh. Bilioni 175 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuleta mapinduzi katika vyuo  vinne vinavyotoa elimu ya ufundi  hapa nchini.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo Juni 3, 2020  jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi magari manne kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambacho  ni miongoni mwa vyuo vinne vitakavyonufaika na mkopo huo wa Benki ya Dunia kupitia mradi wao wa Kuleta Mapinduzi kwenye elimu ya ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP).

Kuhusu mradi wa EASTRIP, alisema mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Ethiopia na Tanzania ambayo imebahatika kupata mkopo huo wa USD milioni 72 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 175.

Amevitaja vyuo vitakavyonufaika na mkopo huo na kusema fedha zitatolewa kwa chuo cha NIT ambacho kitapata Bilioni 49, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam  Campus (DIT DSM), DIT Campus ya Mwanza na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC). 

Amesema, malengo ya mradi huu ni kuvijengea vyuo hivyo vya ufundi uwezo ili viweze kutoa mafunzo bora na kuwapata wanafunzi wenye sifa stahiki ambazo zitawawezesha katika soko la ajira kwa kujajili ama kuajiliwa, pia fedha hizo za  mradi zitatumika katika kujenga miundombinu ikiwemo madarasa, mabweni, karakana, ofisi za wahadhiri pamoja na watumishi wengine. 

Ameongeza kuwa, magari hayo ambayo  NIT wamepatiwa ni sehemu ya mradi huo hivyo wanauomba uongozi wa chuo hicho kuhakikisha yanatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema mradi huo wa EASTRIP ni wa miaka mitano, ambao lengo lake ni kuongezea vyuo uwezo wa elimu ya ufundi na mafunzo  kutoa taaluma inayokidhi matakwa ya soko, kuongeza uwezo wa walimu pamoja na kuboresha miundombinu.

Amesema kiasi cha fedha cha Sh. Bilioni 49 ambacho NIT kitazipata kitatumika pia katika kuboresha utawala na Menejimenti katika kutoa mafunzo kama kituo cha umahiri, kuimarisha mahusiano kati ya chuo na wadau mbalimbali wa sekta ya anga na oparesheni za usafirishaji pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wasichana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo, Profesa Bavo Nyichomba amesema hatua ya chuo kununua magari hayo ni dhahiri kuwa imepata vitendea kazi madhubuti na ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Benki ya Dunia pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2