CCBRT YAUNGANA NA WADAU KUADHIMISHA SIKU YA MGUU KIFUNDO NYAYO ZA KUPINDA DUNIANI 3, JUNI 2020 | Tarimo Blog

 SIKU ya miguu kifundo au nyayo za kupinda ulimwenguni huadhimishwa kila  mwaka tarehe 3 Juni. Tarehe hii ilitokana na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Dk. Ignacio Ponseti, (1914-2009) Daktari aliyegundua njia ya kutibu ulemavu huo ujulikanao kwa lugha ya kingereza kama “Ponseti method”.

Lengo la Siku hii ya Mguu kifundo ni kukuza uelewa juu ya ulemavu huu na kuhamasisha utumiaji wa matibabu yake kwa kutumia njia ya Ponseti.

Miguu kifundo au nyayo zilizopinda nini?
Mguu kifundo au nyayo za kupinda kwa kitaalamu unajulikana kama “Congenital talipes equinovarus” ama “Clubfoot” ni aina ya ulemavu wa mguu au nyayo ambapo mguu mmoja au yote huelekea ndani na kwa kutazama chini. Hali hiyo inaathiri mifupa, misuli, ngozi na mishipa ya damu ya mguu/unyayo. Hili tatizo ni la kuzaliwa nalo, na huathiri watoto wa kiume zaidi kuliko wale wa kike .Sababu ya kuwaathiri watoto wa kiume kuliko wale wa kike bado haijajulikana na tafiti zinaendelea.

Ukubwa wa tatizo Ulimwenguni.
Tafiti zinaonyesha kuwa mguu kifundo au nyao za kupinda hutokea kwa mtoto 1 kati ya watoto 750 mpaka 1000 aliyezaliwa hai kila mwaka. Duniani kote takribani  watoto 813,000 huzaliwa na mguu kifundo kila mwaka na 80% ya hizi ni hutokea  nchi zinazoendelea hususani  Kusini mwa Jangwa la Sahara hii ni sawa na (22%).

Tanzania
Kwa mujibu wa tafiti watoto 2200 hadi 3000 wanazaliwa na mguu kifundo/nyayo za kupinda kila mwaka hapa nchini. Kwa mujibu wa Dokta Zainab Illonga daktari wa mifupa kutoka hospitali ya CCBRT Dar es Salam, hospitali hiyo huwaona watoto na hata watu wazima wapya wenye matatizo hayo takribani 400 kwa mwaka.

Ni nini husababisha ulemavu huu?
Hakuna sababu kubwa ambayo husababisha mguu kifundo/nyayo za kupinda  ingawa kuna sababu kadhaa ambazo huweza kuchangia mtoto azaliwe na mguu kifundo/nyayo za kupinda. Miongoni mwao ni, uhusiano wa kifamilia kama kuna mtu ndani ya ukoo/familia aliwahi zaliwa na aina hiyo ya ulemavu inaweza pelekea mtoto akazaliwa na ulemavu huu katika familia hiyo.

Sabu nyingine zinazochangia ni pamoja na:
Ukaaji wa mtoto kwenye mfuko wa uzazi, shida ya mfumo wa fahamu kama ugonjwa wa kupooza kwa ubongo na mgongo wazi Kiasi kidogo cha amniotic kinachomzunguka mtoto kwenye mfuko wa uzazi (oligohydramnios) wakati wa uja uzito yaweza kuwa sababu ya mtoto kuzaliwa na tatizo hilo.

Je! Kuna dalili gani za mguu kifundo?

Dalili za mguu kifundo ni:
Mguu kuonekana mfupi na mpana, kisigino huelekea chini wakati nusu ya mbele ya mguu (mguu wa mbele) hugeuka ndani.
Msuli kamba wa kisigino (Achilles tendon) unakaza na mfupi.
Kisigino kinaweza kuonekana chembamba.
Misuli ya mguu ni midogo ikilinganishwa na mguu wa kawaida.

Je! Mguu kifundo hutambuliwaje?
Mtoa huduma ya afya kwa mama na mtoto anaweza kutambua hitilafu ya nyayo za mtoto mara baada ya kuzaliwa na hivyo kushauri mahali pa kumpeleka kwa matibabu ya mapema.

Pamoja na hilo mlezi au mzazi anaweza tambua dalili hizo za mtoto mwenye nyayo za kupinda wakati wa malezi na makuzi ya mtoto. Vipimo vya x ray hua havihitajiki kugundua tatizo la mguu kifundo hata hivyo endapo motto atafikishwa kwenye huduma wakati muda umekwisha pita sana ama motto anamatatizo mengine ya ulemavu kama “Arthrogryposis” ama mengine kunaweza kuwa na ulazima wa kupiga mionzi (X ray) ili kubaini shida zaidi. 

Je! Mguu kifundo unatibiwaje?
Matibabu hutegemea dalili za mtoto, umri, na afya yake kwa ujumla. Pia itategemea jinsi hali ilivyo. Lengo la matibabu ni kunyoosha mguu ili uweze kukua na kuimarika na kuwa kawaida. Bila matibabu, mtoto atakuwa na shida kwenye kutembea.

Matibabu ni pamoja na:
Njia ya Ponseti (bila upasuaji mkubwa) (Dr Ignacio Ponseti, mvumbuzi wa mbinu ya Ponseti kwa ajili ya matibabu ya mguu kifundo) 
Hii kawaida hujaribiwa kwanza bila kujali ukubwa wa tatizo. Matibabu haya yanatumia utaalamu wa kunyoosha misuli kwa utaratibu maalumu kisha kufunga hogo kila baada ya wiki moja ili kurekebisha mguu hatua kwa hatua. Mara nyingi huchukua mwezi mmoja hadi miwili. Kisha mtoto anaweza akahitaji upasuaji mdogo wa kulegeza msuli kamba wa kisigino na kisha kufungwa hogo la mwisho. Baada ya hapo kwa sababu mguu kifundo huweza jirudia  mtoto atalazimika kuvaa viatu maalumu kwa miaka kadhaa ili kuzuia mguu usirudi tena. Mara ya kwanza, viatu hivi huvaliwa kwa masaa 23 kwa siku hadi miezi 3. Halafu huvaliwa usiku tu hadi miaka 5.

Mtoto mwenye tatizo hilo anaweza kuhitaji upasuaji mkubwa ikiwa matibabu mengine hayarekebishi mguu. Upasuaji maalum unategemea aina na kiwango cha hitilafu cha mguu na umri wa mtoto. 
Watoto wengi wachanga walio na mguu kifundo hawahitaji upasuaji. Watoto ambao huhitaji upasuaji huenda wakahitaji upasuaji zaidi ya mara moja kwa sababu hitilafu ya mguu yaweza kurudi kadri anavyokua.
Ni nini kinatokea ikiwa mguu kifundo/nyayo za kupinda imeachwa bila kutibiwa?
Ikiwa mguu kifundo haukutibiwa mtoto hataweza kutembea kawaida. Wakati mwingine inawezekana kutembea na mguu kifundo, lakini ni ngumu sana. Watoto ambao wana mguu kifundo hutembea kwa upande wa juu ya miguu yao. Hii inaweza kusababisha kovu kubwa na maumivu sugu.
Mtoto anapokua na kujitegemea kimaisha kuwa na mguu kivundo itamaanisha kuwa na changamoto katika shughulli zake za kila siku na hata uwezo wa kuzalisha kipato.

Je! Matibabu ya mguu kifundo  hutolewa wapi?
CCBRT na hospitali washirika hutoa matibabu hayo, kwa CCBRT matibabu  kwa watoto chini ya miaka mitano hutolewa bila malipo kwa kushirikiana na Tanzania Clubfoot Care Organisation (TCCO), Miraclefeet na Tigo Tanzania. Hospitali yetu ya CCBRT ina uzoefu wa kutoa matibabu ya aina hii kwa takribani miaka 19, “wito wangu kwa wazazi wenye matatizo ya aina hii wasiwafiche ndani wawalete CCBRT tuko tayari kuwapatia huduma bila malipo kwa wazazi wenye watoto wa ulemavu huu na ambao wako mikoani wanatakiwa kufanya utaratibu wa kupata malazi ya walau miezi miwili wakati wakiendelea na matibabu hapa Dar es salaam. Lakini pia wale wa mikoa ya karibu na Moshi wasisite kupeleka watoto wao katika kituo chetu cha CCBRT kilichopo Moshi.

Je! Athari ya COVID 19 ni nini katika utoaji wa huduma CCBRT?
Katika kuunga mkono juhudi za serikali dhidi ya Covid 19 na kuhakikisha kwamba tunapunguza kuenea kwa Covid 19 na kuwalinda wagonjwa na wafanyakazi, tumeweka utaratibu maalumu wa kuwahudumia wagonjwa wetu tunaowaona kwa siku, lakini pia tumeanza kutoa huduma siku za Jumamosi na kuongeza muda wa kuwaona wagonjwa siku za kawaida ili kupanua wigo wa huduma zetu.

Hivyo basi, wazazi wenye watoto wa miguu kifundo wanahimizwa kuleta watoto wao siku yeyote kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi
Je! Unaweza kushauri nini jamii kwa ujumla juu ya mguu kifundo?
Mguu kifundo unatibika na sio kurogwa wala laana. Wazazi wawapeleke watoto hospitalini kupata huduma mapema iwezekanavyo. Wakunga wawachunguze watoto wachanga na wale watakaobainika na mguu kifundo wawaelekeze kuja CCBRT Dar es salaam ama CCBRT Moshi au hospitali inayotoa huduma sahihi ya mguu kifundo.

Tunashauri pia wanasayansi na wanataaluma kujikita pia kufanya utafiti zaidi kuhusu mguu kifundo Tanzania. Pia tunatoa wito kwa wafadhili wajitokeze zaidi ili kuweza kuhakikisha hizi huduma zinaendelea kutolewa bure. 

Vyanzo vya TAKWIMU
1. Smythe T, Kuper H, Macleod D, Foster A, Lavy C. Birth prevalence of congenital talipes equinovarus in low- and middle-income countries: a systematic review and meta-analysis. Trop Med Int Heal. 2017;22(3):269–85. 
2. About Clubfoot - Tanzania Clubfoot Care Organization [Internet]. [cited 2020 Jun 2]. Available from: https://bit.ly/3gMF9g9

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2