KIWANDA KURUDISHA SHUKRANI KWA RAIS MAGUFULI KWA KUGAWA CHAKI BURE ...DC JOKATE MWEGELO ATOA NENO | Tarimo Blog


Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo(aliyevaa nguo nyekundu),Katibu Tawala wa wilaya hiyo Tella Mwampamba(kulia) wakiwa na baadhi ya wafanyakazi na viongozi wa kiwanda cha kutengeneza chaki cha Mkongoma General Supply Ltd wakishuhudia taa zikiwaka baada ya Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) wilayani humo kupeleka umeme katka kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Mkongoma General Supply Ltd Geoffrey Mkongoma (kulia) akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo(katikati) kuhusu shughuli zao za uzalishaji baada ya kupelekewa nishati ya umeme.Kabla ya umeme kiwanda hicho kilikuwa kinatumia Sh.milioni tano kwa ajili ya kununua mafuta ya dizeli kwa mwezi na sasa wanatumia Sh.400,000 kwa mwezi.
Katibu Tawala Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Tella Mwampamba(katikati) akielezea jambo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo(hayupo pichani) baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza chaki cha Mkongoma General Supply Ltd baada ya kiwanda hicho kupelekewa nishati ya umeme ili kukiwezesha kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Meneje wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mhandisi Nyanda Mlagwa(katikati) akifafanua jambo kuhusu kiwanda cha Mkongoma General Supply Ltd ambacho kwa sasa kinatumia nishati ya umeme baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo kutembelea kiwanda hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani (kulia) akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha Mkongoma General Supply pamoja na baadhi ya wananchi kuhusu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyodhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kuhakikisha inaondoa changamoto zinazoweza kuwa kikwazo katika shughuli za uzalishaji.Pia ametoa pongezi kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa jinsi ambavyo wamebeba maono ya Rais Dk.John Magufuli ya Tanzania ya Viwanda na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza chaki cha Mkongoma wakiwa katika kiwanda hicho baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo kutembelea kiwandani hapo kushuhuhudia shughuli za uzalishaji baada ya kupata nishati ya umeme.
Sehemu ya chaki zikiwa zimehifadhiwa katika makasha maalumu katika kiwanda cha Mkongoma General Supply Ltd.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Mkongoma General Supply Ltd Geoffrey Mkongoma akitoa shukrani zake kwa Serikali ya Awamu ya Tano baada ya kiwanda hicho kupatiwa nishati ya umeme.


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

BAADA kiwanda cha kutengeneza chaki cha Mkongoma General Supply Ltd kilichopo wilayani Kisarawe kupatiwa nishati ya umeme na kusababisha kupunguza gharama za uzalishaji kutoka Sh.milioni 5 kwa mwezi hadi Sh.400,000 kwa mwezi, uongozi wa kiwanda hicho umesema umepanga kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli kwa kugawa chaki bure kwa shule za Wilaya ya Kisarawe, Kibaha na Ilala.

Uongozi huo umesema wameteseka kwa miaka sita ya uzalishaji wao kwa kutumia mafuta ya dizeli lakini chini ya Serikali ya Awamu ya Tano hatimaye wamepata umeme na kwao wanaona kama maajabu huku wakiahidi kufanya kazi zaidi ya uzalishaji ya ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo, wakati wa sherehe za kufurahia kupata nishati hiyo ya umeme , Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Geoffrey Mkongoma amesema kuwa kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2014 katika kata ya Msimbu lakini kwa kipindi chote cha uzalishaji walikuwa wakitegemea genereta linalotumia kiasi kikubwa cha mafuta ya dizeli.

"Kuunganishwa kwa nishati hii ya umeme katika kiwanda chetu, tunachoshuhudia ni maajabu kwani gharama zimeshuka kwa kiwango kikubwa sana.Tulikuwa tunatumia Sh.milioni tano kwa mwezi lakini sasa tunatumia Sh.400,000 tu kwa mwezi.Hivyo tumeamua kurudisha shukrani zetu kwa Rais Magufuli kwa kugawa chaki kwa baadhi ya shule zilizopo Kisarawe, Kibaha na Ilala.

"Tumefurahi sana na tunaahidi tutaendelea kuchapa kazi kwani Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa makini katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wawekezaji wakubwa, wakati na wadogo.Nasisitiza tutagawa chaki bure kurudisha shukrani kwa Rais,"amesema Mkongoma na kuongeza umeme huo sasa utasaidia kuongeza kasi za uzalishaji na hata kuongeza ajira.



Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye amefika kiwandani hapo kuona shughuli za uzalishaji, amempogeza mwekezaji wa kiwanda hicho kutokana na jitihada zake za kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinafanyika licha ya kuwa na changamoto ya kukosa umeme na ni matumaini kwa sasa ataongeza kasi ya uzalishaji.

Pia amesema amefurahishwa na muwekezaji huyo kijana kwani ni wazi amebeba maono ya Rais Dk.John Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda inayochagizwa na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu. "Tunatoa pongezi kwa muwekezaji wa kiwanda hiki kwa uwekezaji huu ambao ameufanya.Ni matumaini yangu sasa ataongeza uzalishaji lakini pia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo haya."

Hata hivyo Jokate amefafanua changamoto kubwa iliyokuwa inawasumbua Kisarawe ni maji na umeme lakini Serikali imeamua kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inawasaidia wawekezaji hasa vijana. "Hatuwezi kuwaacha vijana wanaojitokeza kufanya uwekezaji kama huu wakisumbuliwa na changamoto hizi ndio maana tunaweka mazingira wezeshi ili kurahisisha shughuli zao za kila,"amesema Jokate.

Wakati huo huo Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Wilaya ya Kisarawe Mhandisi Nyanda Mlagwa amesema mpango uliopo ni kuunganisha umeme katika maeneo yote ya kimkakati ikiwemo kwenye viwanda.

Kuhusu vijijini Mlagwa alisema eneo lake lenye vijiji 84 kufikia Oktoba mwaka huu vitabaki vijiji 13 ambavyo havijaunganishwa na itakapofika Juni mwakani vyote vitakuwa vimepata umeme.

Amewaomba wawekezaji kuwekeza wilayani Kisarawe maana umeme upo na wataendelea kuboresha miundombinu ili huduma zote muhimu ziweze kupatikana kwa uhakika.

Ametumia nafasi hiyo kuwahakikisha wananchi wa Kisarawe kuwa umeme utafika maeneo yote kikubwa ni wananchi kujiandaa kuunganishiwa umeme na kwamba fomu za kuomba umeme ni bure ila gharama ya kuunganisha umeme ni sh.27000 tu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2