Na Said Mwishehe,Michuzi TV
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam inamshikilia Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira wa Mtaa wa Tambukareli Kata ya Azimio kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume cha kifungu cha sheria namba 302 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akizungumzia kukamatwa na kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam Donacian Kessy amesema leo kuwa Januari 19 mwaka 2019 ofisi ya taasisi hiyo mkoa wa Temeke ilipokea malalamiko yanayomhusu Ally Mtiga ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa huo kwa kujifanya ni Ofisa ardhi na kisha kuomba rushwa ya Sh.200,000 kutoka mwa mwananchi( jina limehiafadhiwa) ili aweze kumsaidia kupata leseni ya makazi ya jengo lake.
"Uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kwamba Januari 26 mwaka 2019 ,Ally Mohamed Mtiga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Mtaa wa Tambukareli, Kata ya Azimio anayejifanya ni ofisa ardhi na akiwa katika ofisini kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya Tambukareli alipokea fedha hizo za mtego Sh.200,000 ili kumsaidia mwananchi mmoja kupata leseni ya makazi ya jengo lake,"amesema Kessy.
"Uchunguzi wa tuhuma hizo umekamilika na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote kuanzia leo na kisha kufunguliwa mshtaka kwa kosa la kujpatia fedha kwa njia ya udanganyifu,"amesisitiza.
Pia amesema TAKUKURU Mkoa wa Temeke inatoa mwito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi kwa namba ya bure 113 au kupiga 113 na kutoa maelezo au kufika ofisi za TAKUKURU iliyo karibu nawe,amesema Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment