UKATILI WA KISHENZI WA BINADAMU USIFANANISHWE NA TABIA ZA WANYAMA | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

WIKI Moja sasa imepita toka Askari wa Zimamoto na Uokoaji, Denis Minja alipomuokoa mtoto ambaye alikua ametupwa kwenye shimo la Choo cha Shule ya Msingi Murgwanza wilayani Ngara, Kagera.

Nikukumbushe mtoto huyo alikua na umri wa mwaka mmoja na miezi sita na inasadikika alitupwa na Mama yake katika shimo hilo lenye urefu wa futi 30.

Fikiria Binadamu aliezaliwa bila kutupwa na wazazi wake yeye anakuja kumtupa mtoto mdogo kiasi hiko kwenye shimo la choo. Lengo lake bila kupepesa maneno lilikua ni kumuua mtoto huyo.

Tazama mtoto ameokolewa, akapelekwa Hospitali kwa ajili ya matibabu na sasa amepona. Sijui aliemtupa huko alipo anajitazamaje na roho mbaya yake.

Mara ngapi umewahi kusikia visa vya namna hii hapa nchini na duniani kwa ujumla. Simulizi za akina Mama kutupa watoto wao chooni, barabarani au kwenye dampo ni za kila siku.

Hazina tofauti na stori za Baba kumkana mtoto wake mwenyewe, kukimbia ujauzito au kutoa fedha ili mwanamke akatoe mimba. Huu wote ni ukatili.

Uswahilini kwetu kusikia Mama kamchoma mwanae na pasi mwilini kwa sababu ya udokozi wa nyama jikoni au mtoto kaiba Sh 200 sasa limekua jambo la kawaida.

Kabla hujafikiria kumchoma mtoto kwa pasi tu kwa sababu ameiba lazima ujifikirie wewe kama Mzazi unatosha kuitwa Baba au Mama?

Maana haiwezekani utoshe kwenye nafasi ya Baba au Mama halafu mtoto awe mwizi au mdokozi. Hii inaonesha wazi haumpi malezi mazuri na kumlea mtoto kwenye maadili bora.

Sasa kwanini tusikuchome kwanza wewe Mzazi na pasi kabla ya kumchoma mtoto maana tatizo limeanzia kwako kwa kushindwa kumlea vizuri na kupelekea kuwa na tabia za udokozi.

Ni kama ambavyo kila nikifungulia Radio na kusikia visa vya mauaji ya kutisha kwenye Mikoa ya Kwanda ya Ziwa. Hasa Mara na Shinyanga.

Leo utasikia Mume amemchinja Mke wake kisa kamnyima Samaki, kesho utasikia stori ya Mke kumchoma kisu mumewe kwa wivu wa mapenzi.

Usiniambie hujawahi kusikia matukio ya mauaji ya vikongwe na ndugu zetu wenye Ualbino kwa sababu tu za imani za kishirikiana. Washenzi wanamuua Bibi kizee wakimhisi mchawi tu eti macho yake ni mekundu.

Yaani vijana wenye nguvu zao wanamuua Albino ili wakate kiganja chake wakipeleke kwa mganga kwa minajili ya kupata utajiri. Huu ni ushenzi na ukatili wa kiwango cha juu sana.

Ni kama ambavyo wale Askari 'washenzi' kule Marekani walivyomuua George Floyd kwa makusudi kabisa baada ya kumtembezea kichapo kikali hadi kupelekea mauti yake.

Kesi za Watu weusi kuulia na Polisi nchini Marekani zimekua ni nyingi na sasa siyo stori tena. Limekua kama jambo la kawaida. Ubaguzi wa kishenzi huu.

Haya yote yakitokea tunauficha ubinadamu wetu kwenye unyama. Utasikia hawa wauaji wana roho ya kinyama sana. Hawa wauaji makatili kama wanyama.

Utadhani Simba, Nyati, Tembo wana ukatili tulionao sisi. Utafikiri kuna siku Simba amewahi kuonekana akimtupa mtoto wake kwenye bwawa la maji ili afe.

Lini umeona Mbwa akimuua mtoto wake mwenyewe? Wanyama porini wamegawanyika kwenye aina mbili.Wale wanaokula nyama na wale wanaokula majani. Simba kumla Nyati siyo ukatili kwa sababu ndio kitoweo chake. Chui kumla Swala siyo ukatili ndio kitoweo chake.

Hivyo ukatili wetu tusiiufananishe na unyama, tusiwape ubaya wanyama kwa roho mbaya zetu. Fikiria tunavyotoa kafara kwenye familia zetu ili tupate utajiri, angalieni tunavyofanyiana hila kwenye siasa ili tupate madaraka. Wanyama na unyama wao hawana ukatili huo.

Tunazo imani za kidini, tunaenda makanisani na misikitini, tunajifunza mashuleni lakini elimu zote mbili tunazozipata bado hazitusaidii. Ukatili wetu uko pale pale.

Hapa tu sheria za Nchi zinatubana lakini laiti ingekua kuua siyo makosa basi tungeuana sana mitaani huku.

Yote hayo ni kwa sababu mioyo yetu imekosa upendo, imekosa imani, mahusiano yetu na Mungu ni ya hovyo kiasi kwamba kuua watoto wetu kwa kuwatupa chooni, kuchinja binadamu wenzetu kisa mali tunaona ni kawaida.

Ukatili wa binadamu haufikii hata robo unyama wa Wanyama licha ya sisi kupewa akili na maarifa kuwazidi wao.

0683 015145

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2