WAZIRI MHAGAMA AITAKA CWT KUCHUKUA TAHADHARI YA KUJIKINGA NA CORONA KWENYE MKUTANO WAO | Tarimo Blog

Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amekagua maandalizi ya mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) utakaofanyika Juni 5 mwaka huu na kuwataka kuchukua tahadhari ya kujinga na Corona.

Mhe Mhagama ametembelea Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambao ndio mkutano huo utakapofanyika ambapo pia utatumika kuchagua viongozi wakuu kitaifa wa CWT.

Akizungumza baada ya kukagua maandalizi na kuzungumza na viongozi wa chama hiko, Waziri Mhagama amesema mkutano huo ni muhimu kwa CWT kwa sababu utakwenda kuleta viongozi wengine wa kitaifa kwa mfumo wa kidemokrasia.

Amesema ngazi zingine za Mikoa na Wilaya tayari zishafanya uchaguzi wa kupata viongozi wake na sasa kilichobakia ni uchaguzi wa viongozi wa juu na kuwataka Walimu ambao ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu kujitokeza kwa wingi ili kuchagua viongozi wanaoamini watakipeleka mbele zaidi chama chao.

Waziri Mhagama amesema kwa siku ya leo ameshauriana na wajumbe wa maandalizi wa mkutano huo namna nzuri ya kuendesha mkutano huo kwa hadhi ya Chama chenyewe pamoja na kuzingatia mazingira yaliyopo nchini kwa sasa kwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya Corona.

" Huu ni mkutano wa muhimu sana kwa mustakabali wa CWT na Ofisi ya Waziri Mkuu kama walezi wa vyama hivi tumefika hapa kukagua maendeleo na maandalizi yake ambayo tumeridhishwa nayo na tunaamini mkutano utafanyika kwa amani kabisa.

Kama serikali nimetoa maelekezo ya kuhakikisha pia tahadhari dhidi ya Corona inachukuliwa kwa kuweka vifaa vya kujikinga zikiwemo ndoo zenye maji tiririka kwa ajili ya kunawia mikono, Vitakasa mikono pamoja na hatua zingine muhimu, " Amesema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Rais wa CWT, Mwalimu Lea Ulaya amesema mkutano huo unatarajia kujumuisha Walimu 1200 ambao watatoka Mikoa yote Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine watachagua viongozi wapya watakaokaa madarakani hadi 2025.

Mwalimu Lea amesema mkutano huo umekuja baada ya kumaliza chaguzi zao za ngazi ya matawi, Wilaya na Mikoa na kilichobaki ni uchaguzi wa kuwapata viongozi wao wa kitaifa.

" Tunashukuru tayari uchaguzi katika ngazi za chini tumeshamaliza. Huu wa kitaifa ni wa kumpata Rais wa CWT, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Viongozi wanaotokana na makundi maalum kama kundi la Vijana, kundi la Walimu wanawake na wenye Ulemavu," Amesema 

Nae Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif ameahidi kuchukua maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa Corona.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama akitoa maelekezo alipofika kukagua maandalizi ya mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) utakaofanyika Juni 05 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama akikagua ratiba ya mkutano huo wa CWT utakaofanyika jijini Dodoma Juni 5 mwaka huu.
Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wakimsikiliza Waziri Jenista Mhagama alipofika kukagua maandalizi ya mkutano huo.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2