COSOTA YAKABIDHIWA RASMI WIZARA YA HABARI | Tarimo Blog




Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO.



Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA) leo kimekabidhiwa rasmi kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kilipokuwa awali.

Hafla ya makabidhiano ya Chama hicho imefanyika jijini Dar es Salaam baina ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo mbili na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya sanaa wakiwemo viongozi wa taasisi za Serikali, wasanii wa muziki, filamu, sanaa za maonesho na waandishi wa vitabu pamoja na miswada na wengineo.

Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa tukio hilo ni matunda ya uamuzi makini wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli uliofanywa kwa wakati muafaka ambapo nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kipato cha kati.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kufanya uamuzi mgumu wenye manufaa kwa wasanii wa Tanzania kwa kuwa anatambua sanaa ina umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu hivyo wasanii wetu hawapaswi kuwa maskini,” alisema Dkt. Abbasi.

Pia Dkt. Abbasi alieleza kuwa uamuzi wa kuihamisha COSOTA ulitekelezwa ndani ya saa 24 baada ya tamko la Rais Magufuli alilolitoa Julai 12 mwaka huu akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na yeye kuahidi kuwa ataendelea na kanuni hiyo ya saa 24 za maajabu ya kiutendaji.

“Nawaahidi kuwa ndani ya saa 24 zijazo kuanzia muda huu mambo mawili yatatokea, kwanza nitakutana na Bodi ya COSOTA na kusikiliza mipango yao katika kutekeleza kivitendo COSOTA mpya yenye kupigania haki za wasanii, pili ndani ya saa 24 hizi nitakutana na menejimenti na wafanyakazi wote wa COSOTA kuona tena mikakati yao ya kumfanya msanii awe tajiri kwa kunufaika na kazi zake”, alieleza Dkt. Abbasi.

Aidha kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe alibainisha kuwa COSOTA ni taasisi muhimu katika kutunza na kulinda maslahi ya wasanii hivyo wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa chama hicho muda wowote itakapohitajika kwa ajili ya maendeleo ya wasanii na taifa kwa ujumla.

Naye Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Bi. Doreen Sinare alieleza kuwa wanajivunia uongozi makini wa Rais. Dkt. John Pombe Magufuli kwani ndani ya miaka mitano ya uongozi wake chama hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa Bodi ya COSOTA pamoja na kuhamishiwa kwenye wizara inayohusika na wadau wa sanaa.

“Tunaahidi kuendeleza mazuri yote tuliyotoka nayo Wizara ya Viwanda na tunatarajia Wizara ya Habari itatupatia ushirikiano zaidi ili kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo kwa wasanii wa Tanzania,” alisema Doreen.

Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA) kiliundwa mwaka 1999 kupitia Sheria namba 7 ya Hakimiliki na Hakishiriki (The Copyrights na Neighbouring Rights Act).

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe (kulia), akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi(kushoto), nakala ya uthibitisho iliyosainiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli ya kuihamisha COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

  Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akikabidhi vitendea kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi(kushoto),  baada ya Chama cha Hakimiliki (COSOTA) kuhamishiwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi akionesha vitendea kazi kwa watalaam wa Sanaa (hawapo pichani) baada ya Chama cha Hakimiliki (COSOTA) kukabidhiwa Wizara hiyo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye Hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi akifuhia jambo na Msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Khamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA kwenye Hafla  ya makabidhiano ya COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda kuja Wizara ya Habari iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi, akizungumza na Watalaam wa Sanaa (hawapo pichani), katika makabidhiano ya Chama cha Hakimiliki (COSOTA) ambayo ilikuwa Wizara ya Viwanda na Biashara na sasa imelejeshwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia leo Julai 15, 2020.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na Watalaam wa Sanaa (hawapo pichani), katika makabidhiano ya Chama cha Hakimiliki (COSOTA) ambayo ilikuwa Wizara ya Viwanda na Biashara na sasa imelejeshwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia leo Julai 15, 2020.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Hakimiliki (COSOTA), Bi. Doreen Sinare akizungumza na Watalaam wa Sanaa (hawapo pichani), katika makabidhiano ya COSOTA ambayo ilikuwa Wizara ya Viwanda na Biashara na sasa imelejeshwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia leo Julai 15, 2020.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2