Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
RAIS Wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ameitisha kikao cha dharura kufuatia mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona (Covid -19) kuingia nchini humo kwa kuvuka mpaka kinyemela akitokea Korea kusini, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti tukio hilo leo.
Imeelezwa kuwa kisa hicho kinakuwa cha kwanza kuripotiwa nchini humo na tayari mshukiwa amefanyiwa vipimo na amewekwa karantini.
Kim ametangaza hali ya dharura nchini humo na kuagiza kuweka vizuizi katika mpaka kwenye mji wa Kaesong kwa tahadhari zaidi.
Imeripotiwa kuwa mshukiwa huyo alikuwa Korea kusini kwa miaka mitatu na alirejea nchini humo Julai 19 mwaka huu kupitia mpaka unaotenganisha nchi hizo mbili kabla ya kukutwa na dalili za Covid-19.
Korea Kaskazini imepokea maelefu ya vipimo vya Corona kutoka Urusi na mataifa mengine na ilifanikiwa kuweka vizuizi hasa mipakani lakini baadaye masharti hayo yakalegezwa.
Aidha Kim ameagiza uchunguzi kwa vyombo vya ulinzi katika mpaka ambao mshukiwa huyo alipita na kuchukua hatua muhimu ikiwemo adhabu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment