SUMAYE:KIFO CHA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA KIMENISHTUA , ALIKUWA NA IMANI KUBWA NA MIMI | Tarimo Blog


*Atoa siri ya jinsi alivyomkatalia asiwe Waziri Mkuu wake
 
Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

BAADA ya kutangazwa kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa usiku wa kuamkilia leo Julai 24, 2020, Waziri Mkuu mstaafu katika Serikali hiyo Frederick Sumaye ameelezea kusikitishwa kwake na kifo hicho huku akieleza mzee Mkapa alikuwa hazina kwa Taifa, Afrika na Dunia kwa ujumla.

Sumaye ambaye amepata nafasi ya kuhudumu katika nafasi ya Uwaziri Mkuu katika miaka yote 10 ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiingozwa na Rais mstaafu Mkapa ameeleza namna ambavyo aliaminiwa na kufanya kazi zake bila kusumbuliwa na Mkapa.

Akizungumza zaidi kuhusu kifo cha mzee Mkapa leo asubuhi hii Sumaye ameenza kwa kueleza kwamba "kwa kweli taarifa ya kifo cha mzee Mkapa,Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu imekuwa ya kushtua kwa kila mtanzania kwasababu tunamfahamu mzee Mkapa vizuri.

"Lakini mimi ambaye nimefanya naye kazi kwa miaka 10 kama Waziri Mkuu wake kwa kweli imenigusa sana kwa sababu mzee huyu alikuwa hazina kubwa sana kwa Taifa letu , hazina kwa Afrika na hazina kwa Dunia
"Alijijengea heshima, aliijengea nchi yetu heshima wakati wa kipindi chake hakika alifanya kazi kubwa ambayo watanzania wote wanaikumbuka na wanaielewa , kwa hiyo mimi nilipata nafasi ya kufanya naye kazi kama Waziri Mkuu wake,"amesema.

Sumaye amesema kuwa Mkapa alimteua mara zote mbili ,kwa maana hiyo alikuwa na imani kubwa sana na yeye."Nilikuwa nafanya kazi kwa uhuru,kwa amani na kufanya kazi bila woga wowote.

MAJANGA KATIKA SERIKALI AWAMU YA TATU

Akimuelezea zaidi mzee Mkapa, Sumaye ambaye alikuwa akizungumza kwa njia ya simu na kituo cha redio cha Wasafi FM ambao walimpigia kwa ajili ya kupata maoni yake baada ya taarifa za msiba huo, amefafanua mambo mengi yakiwemo ya nyakati ngumu ambazo utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu ilizopitia.

Kwa mujibu wa Sumaye amesema katika utawala wowote kuna mambo mengi yanatokea. "Kama utakumbuka wakati wa utawala wake ndipo ambapo nchi ilikuwa inaingia kwenye mageuzi mengi, ni Mkapa ndio aliingiza nchi kwenye mageuzi mengi ya kiuchumi, ndio tulikuwa tunabadilisha sasa kuingia kwenye mfumo wa biashara huria.

"Tulifanya marekebisho ya utumishi wa umma kama mnakumbuka , watu wengi ilibidi wapunguzwe Serikali ili kupata idadi ya watu ambao inaweza kuwa sahihi, kuliwa na majali mengi yaliyotokea , kama ajali ya meli MV Bukoba, kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.

"Mambo mengi mengi yalitokea, kulikuwa na ukame sana kati ya mwaka 1997, hadi mwaka 1998 nabaadae ikafuatiwa na mvua na Elnino ,changamoto ya uchumi ilikuwa ngumu sana, hata mishahara ilikuwa haipatikani kwa watumishi wa umma, tulipambana na hayo hadi nchi ilvyokaa vizuri.Hivyo wakati anaondoka kwa kweli hali ilikuwa nzuri kiuchumi, kiusalama na kubwa zaidi nchi ilikuwa imetulia sana."amesema Sumaye.

SUMAYE AZUNGUMZIA UKALI WA MKAPA

Akimzungumzia utendaji kazi wa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, Sumaye amesema" Ukali wa mzee Mkapa nilikuwa naujua na nilikuwa naupenda kwasababu mimi mwenyewe niikuwa napenda kiongozi mkali kwa yale mambo ambayo yanaonekana sio sahihi.

"Ukali wa Mkapa haukuwa tu hauna mpangilio, kwa Mkapa kama unafanya kazi vizuri hamuwezi kugombana na wala huwezi kuuona ukali wake, lakini kama unafanya kazi vibaya mtagombana tu, kwa hiyo ni ukali mzuri , ukali ambao unarekebisha mambo, ukali ambao hauzuiii kufanya mazuri ambayo unataka kuyafanya katika nafasi yako ya utumishi,"amesema Sumaye.

SUMAYE ATOA SIRI YA KUUKATA UWAZIRI MKUU.

Wakati huo huo Sumaye amepata nafasi ya kuelezea namna ambavyo aliaminiwa na Rais mstaafu Mkapa kwa kumteua kuwa Waziri Mkuu wake kwa kipindi cha miaka 10.

"Kama nikitaka kueleza ukweli kabisa, sikuwa na mazoea naye ya karibu, sikutegemea kupata nafasi ya Waziri Mkuu, aliponiteua nilimkatalia na kumwambia ampe mtu mwingine lakini naye alikataa. 

"Baada ya kumalizika kwa miaka mitano na kujiandaa kwa awamu ya pili nilimuaga vizuri nikamwambia naomba safari ijayo umtafute Waziri Mkuu mwingine , nikamueleza changamoto zilizopo akanielewa, lakini tuliporudi tena akaniteua tena, lakini nikamwambia nilishakuomba mimi nisiwe Waziri Mkuu.

"Akanijibu lazima uendelee.Kwa hiyo mimi ni mtu ambaye utanaona anakuteua sio kwasababu mnafahamiana , au kuna mtu ameenda kukusemea, bali alikuwa anateua kwa jinsi yeye anavyokuona , kwa hiyo sikuwa na ukaribu naye wowote , sikuwa na mtu ambaye amekwenda kunisemea.Labda kwa kuwa nilikuwa bungeni kwa muda mrefu, nilikuwa Naibu Waziri na baadae Waziri labda aliona naweza kumsaidia kazi,"amesema Sumaye.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2