Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida . Denis Nyiraha akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wagombea kutojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, George Silindu (kulia) akizungumza katika mkutano huo.
Mkutano na Wanahabari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida umewataka wagombea nafasi za udiwani na Ubunge kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020.
Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Umoja huo mkoani hapa Dkt. Denis Nyiraha wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Niwaombe wagombea wote kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa kufanya hivyo itasababisha chama chetu kupata viongozi ambao hawatakuwa na sifa stahiki" alisema Nyiraha.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wameibuka watu wakitaka kugombea nafasi za udiwani na ubunge huku wakiwa hawayajui hata hayo majimbo wanayotaka kugombea wala mipaka yake lakini kwa kuwa wana fedha wanaamini watashinda kwa kutumia rushwa.
" Natoa maagizo kwa wenyeviti wangu, makatibu wangu, makatibu hamasa wote kuanzia ngazi ya wilaya hadi kata kuwa mgombea yeyote mwenye mawazo hayo na anayekuja kwa utashi huo asifikiri ubunge ni bidhaa anayokwenda kununua sokoni kama nguo sh.milioni 2, milioni 3 na kuondoka nayo napenda kuwaambia ubunge wa Singida unahitaji watu wenye weledi, wanaojua shida za watu na mipaka ya jimbo. Kwa mantiki hii natuma salamu kwa wale wote wanao fikiri kutumia fedha kupata ubunge wa Singida itakuwa ni ndoto" alisema Nyiraha.
Alisema wagombea wote wapimwe kwa uwezo na kuthubutu kwao na kujitolea na si kwa fedha na kama kuna mgombea wa namna hiyo kwa mkoa wa Singida hana nafasi labda aende sehemu nyingine na huko pia anaamini hawezi kuipata.
Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata zote 136 na majimbo 8 kwenye mkoa huo kitashinda kwa kishindo na hakutakuwa na kura hata moja itakayo haribika.
Alisema wagombea watakao letwa na chama hicho watakuwa safi,wasio na kashifa, ambao ni hitaji la wananchi na wanaweza kwenda kwenye medani za ushindani katika mikoa mingine, bungeni na hata katika halmashauri zetu.
Nyiraha alisema uchaguzi wa mwaka huu hali itakuwa nzuri na nyepesi kwani Mgombea wao Rais Dkt. John Magufuli amefanya kazi iliyotukuka ya kuleta maendeleo chini ya mihimili mitatu, Bunge, Serikali na Mahakama kwa kushirikiana na wabunge na madiwani.
Alisema Rais Magufuli ametekeleza kwa kujenga barabara, maji, umeme, Hospitali na Zahanati na miradi mingine mingi ya maendeleo na mambo yameenda bamubamu.
Katika hatua nyingine Nyiraha amewataka vijana wa chama hicho wenye uwezo na sifa za kuwatumikia wananchi kujitokeza kuchukua fomu za kugombea uongozi.
"Mimi kama Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida nawasihi vijana mkoani hapa wajitokeze kwa wingi kugombea katika majimbo hayo kwani tunaamini katika vijana na Rais wetu Dkt. John Magufuli ana waamini na amekuwa akitoa fursa kwao kwani tumeona wakuu wa mikoa na wilaya vijana, makatibu Tawala na Makatibu Tarafa vijana. Kama Rais anavyotoa fursa hizo nami nawaomba vijana wenzangu wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za ubunge na udiwani. Mkoa wa Singida una kata 136 wajitokeze kugombea ili kuongeza ushindani wa utendaji kazi katika halmashauri zetu " alisema Nyiraha.
Alisema vijana wakiwa katika nafasi hizo wataweza kusogeza maendeleo ya Serikali yetu mbele kuanzia pale alipoishia Rais wetu kwa kuifikisha nchi yetu kwenye uchumi wa kati hivyo nawahamasisha vijana wote wa mkoa huu kujitokeza kugombea nafasi hizo." alisema.
Nyiraha alisema ameacha kwenda kugombea nafasi ya ubunge sio kwamba haupendi bali amefanya hivyo kwa ajili ya kuwatetea kwani ana wajibu wa miaka mitano kufanya hivyo kwani walimuamini kwa kumchagua kwa kura nyingi anaona ni vema awasimamie na kuwahamasisha wajitokeze kugombea nafasi hizo." alisena Nyiraha.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment