WADAU WA MAZINGIRA WAHIMIZWA KUONGEZA MCHANGO WAO WA KUCHAKATA NA KUCHAGIZA NISHATI JADIDIFU KWA MAENDELEO YA TAIFA | Tarimo Blog



 Mkurugenzi wa Can Tanzania Dk. Dr. Sixbert Mwanga(wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa mazingira kutoka asasi mbalimbali waliokutana kujadili na kuweka mbinu mpya za kuihamasisha jamii ili iendelee kutumia nishati jadidifu.

Wadau wa mazingira waliokuwa kwenye mkutano huo wakiwa wamesimama kabla ya kufanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kuuchangamsha mwili.

Mratibu wa Miradi kutoka Forumcc Henry Kazula akiwa kwenye mkutano huo akiandika jambo.
Ofisa Miradi Can Tanzania Jophillene Bejamula akiwa makini kufuatilia majadiliano baada ya kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Can Tanzania Dk.Sixbert Mwanga.

 
Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WADAU wa mazingira nchini wametakiwa kuongeza mchango wao kuchakata au kuchagiza nishati jadidifu katika maendeleo ya Taifa hasa kwa kuzingatia nchi yetu tayari imeingia uchumi wa kati.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Can Tanzania Dk. Dr. Sixbert Mwanga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akifungua mkutano uliowashirikisha asasi za kiraia ambazo zinajihusisha na masuala yanayohusu nishati jadidifu pamoja na mazingira kwa ujumla.

Hivyo Dk.Mwanga ametumia nafasi hiyo kufafanua masuala yanayohusu nishati jadidifu pamoja na nishati safi katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa letu la Tanzania hasa kwa kuzingatia nishati jadidifu ikitumika vizuri inaweza kutoa mchango mkubwa wa kimaendeleo.

"Ushauri wangu kwa washiriki ambao tumekutana hapa tuanze kuhakikisha tunaongeza mchango katika nishati jadidifu katika kuchakata au kuchagiza maendeleo ya taifa letu.

"Hasa kwa kuzingatia nchi imeshaingia kwenye uchumi wa kati, hivyo bado tunayo safari ndefu ya kuhakikisha tunabaki kwenye uchumi wa kati bila kushuka maana inaweza tukashuka au kupanda zaidi,"amesema Dk.Mwanga.

Hata hivyo amesema asasi hizo ambazo zimekutana lengo kubwa ni kujadili na kuweka mbinu zinazoweza kuongeza tija ambazo zinafanywa na Serikali ili sote kwa pamoja wawe na mchango unaotambulika katika kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu.

Pia amesema Can Tanzania wamekuwa wakitekeleza mradi wa nishati jadidifu unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Hivos, hivyo kupitia mkutano huo wameangalia miradi waliyoitekeleza maeneo ya Kijiji cha Kidomole na Kata ya Makurunge ndani ya Wilaya ya Bagamoyo.

Kuhusu nishati jadidifu, Dk.Mwanga amesema anafikiri wakati wanaanza walikuwa wanakwenda tararibu lakini sasa hivi kuna muitikio mkubwa.

"Kwanza katika halmashauri, kuna muitikio katika vikundi kwa ngazi za vijiji , tunashuhudia kuna vikundi ambavyo vimeamua kutengeneza majiko banifu yanayotumia kuni mmoja kupika chakula kwa kutumia rasilimali zilizopo vijijini.

"Kwa hiyo naweza kusema watu wamehama na wamegundua kwanza kuni zimekwenda mbali na mkaa haupo karibu, lakini Serikali imekuwa macho katika kulinda misitu , mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri vitu vyote hivyo , kwa hiyo tunalazimika aidha tunapenda au hatupendi sasa tunaenda kule.

"Kwa hiyo tunachokifanya sisi kwa sasa ni kuongeza uelewa, lakini nikiri hatuko zero , tuko kwenye eneo la nishati jadidifu tumepiga hatua na kama tungekuwa tunasema ndege basi ingekuwa imeshaanza kutembea kuelekea kupaa,"amesema Dk.Mwanga.

Kwa upande wa baadhi ya washiriki kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Can Tanzania wametumia nafasi hiyo kueleza haja ya wao kuendelea kujenga uelewa kwa jamii kuhusu matumizi ya nishati jadidifu.

Wamesisitiza katika nishati jadidifu wamekubaliana kuendelea kuwa wamoja na kila mmoja mtu kuona umuhimu wa kutumia nishati hiyo na kwamba huenda uchumi wa kati utasaidia kuifanya jamii ya Watanzania kwenda pamoja.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2