Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepandikiza kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) nje ya Taasisi hiyo bila ya kutumia mtambo wa Cathlab.
Mgonjwa aliyewekewa pacemaker alipata ajali iliyosababisha uti wa mgongo kupata shida na kusababisha baadhi ya viungo vya mwili kupoteza uwezo wa kufanya kazi ikiwemo mishipa ya damu inayoratibu uwezo wa moyo kutengeneza mapigo yake (Sympathetic Waves System).
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaama daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Yona Gandye alisema kutoka na tatizo alilolipata mgonjwa mara baada ya kupata ajali mapigo ya moyo yalishuka hadi kufikia 30 kwa dakika na mgonjwa kuonesha dalili za ukosefu wa mahitaji muhimu ya mwili yanayosambazwa na mapigo ya moyo ambayo ni oxygen , virutubisho, madini na chakula.
“Mgonjwa huyo alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na alihitaji huduma ya haraka ya kuwekewa kifaa kisaidizi ambacho kinausaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) ili mapigo yafikie 60 hadi 100 ambayo ni mapigo ya kawaida ya moyo”.
“Kutokana na mazingira ya mgonjwa kutoweza kuhamishika kutoka MOI na kuletwa JKCI ilibidi tumfuate kumwekea Pacemaker. Tulitumia vyumba vya upasuaji vya kawaida kutumia mashine tofauti na yetu ambayo yao inajulikana kwa jina la C-ARM”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema huduma hiyo wameitoa kwa mara ya kwanza nje ya Taasisi hiyo na kuifanya bila ya kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambao ni maabara ya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na tiba
Alimalizia kwa kusema ushirikiano wa JKCI na MOI na utayari wa JKCI kuhudumia wagonjwa nje ya Taasisi hiyo ulisaidia kufanyika kwa huduma hiyo kwa haraka. Aliziomba Hospitali kuwasiliana na JKCI kama watapata mgonjwa mwenye matatizo ya moyo ambaye hawezi kuhamishika ili waone namna ambavyo wataweza kumsaidia mgonjwa huyo kwa kumfuata mahali alipo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment