TABIA NA MITAZAMO IENDANE NA UBORA WA MAJENGO: JAJI MKUU | Tarimo Blog

Na Lydia Churi-Mahakama, Shinyanga
 
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kubadili tabia na mitazamo ili iendane na ubora wa majengo mapya na yenye vifaa vya kisasa yanayojengwa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini.
 
Akizindua jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga leo, Jaji Mkuu amesema Mahakama haitokani na majengo mazuri peke yake, bali huduma bora kwa wananchi ambapo pia amewataka watumishi wa Mahakama kuacha tabia zisizoendana na maadili mema wanapotekeleza wajibu wao.
 
“Maboresho makubwa tuliyofanya kupitia Mpango Mkakati, Programu ya Maboresho na uwekezaji mkubwa katika TEHAMA hayataboresha huduma za utoaji haki kama watumishi na viongozi katika ngazi zote za Mahakama hawatakuwa na mitazamo chanya ya kuwaheshimu na kuwathamini wanaofika mahakamani kutafuta haki” alisema Jaji Mkuu.

Alisema, nguvu na uwezo wa Mahakama kwa kiasi kikubwa unategemea imani ya wananchi kwa Mhimili huo na kuwa dhana ya sasa inayoongoza ujenzi wa majengo ya Mahakama ni kujenga majengo yanayotoa huduma jumuishi (Integrated Justice Centres), yaani kutoa huduma za zaidi ya ngazi moja ya Mahakama na pia wadau wanaotoa huduma mbali mbali kuwa katika jengo moja.

Jaji Mkuu alisema maboresho yatakuwa endelevu endapo watumishi wote
watayaelewa na kutambua Mahakama inaelekea wapi. “Nawaomba watumishi wa Mahakama tutekeleze dhana ya kumiliki maboresho na tutafanikiwa endapo kila mtumishi atafuatilia utekelezaji wake na kuyaelewa na kuwa tayari kuyafafanua kwa wananchi, wadau na hata kwa Mihimili ya Serikali na Bunge” alisisitiza.

Alisema maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama yanalenga mambo makuu mawili ambayo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za utoaji haki katika majengo bora yakiwa na vitendea kazi vya kutosha na kuwapunguzia wananchi umbali mrefu wanapotafuta huduma za Mahakama.

Jaji Mkuu aliwapongeza wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kupewa
kipaumbele katika kupatiwa huduma za Mahakama Kuu kwani mikoa ya
Morogoro, Pwani, Singida, Manyara, Njombe, Geita, Katavi, Lindi, Simiyu na

Songwe bado inasubiri kwa hamu kuwa na majengo yao ya kutoa huduma katika ngazi ya Mahakama Kuu.

Pamoja na kusogezewa huduma katika ngazi ya Mahakama Kuu; wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kupitia jengo lililozinduliwa wamesogezewa pia huduma za Mahakama ya Rufani. Kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe 24/7/2020, jengo la Mahakama Kuu Shinyanga, limetangazwa kuwa ni Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani.

Alifafanua kuwa tangazo hilo lina maana kuwa, Mahakama ya Rufani itafanya kikao chake cha kwanza Shinyanga kuanzia tarehe Agosti 10 hadi 28, 2020 ili kusikiliza jumla ya mashauri 29. Kila mwaka, Mahakama ya Rufani itakuwa na vikao katika jengo kanda ya Shinyanga.

Wakati huo huo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kubuni na kuendeleza mkakati wa ujenzi wa majengo ya Mahakama yenye ubora zaidi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kusogeza karibu na wananchi. Alisema kazi ya Mhimili wa Mahakama pamoja na Serikali ni kutoa huduma bora kwa wananchi ili wawe na furaha na amani.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi
amesema Mahakama ya Tanzania imejipanga kama mihimili mingine ilivyojipanga katika suala la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu. “Mahakama itasimama kwenye nafasi yake katika uchaguzi Mkuu”alisisitiza Jaji Kiongozi.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka
watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuyalinda, kuyaenzi na kuyaishi maboresho ya Mahakama ikiwemo majengo pamoja na matumizi ya Tehama.

Aliwataka watumishi kutenda haki na kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na uadilifu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru
alipongeza watangulizi wake Mahakama kwa ubunifu na usimamizi mzuri wa miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama likiwemo jengo la kanda ya Shinyanga lililozinduliwa.

Akizungumzia gharama za ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.9 ambazo ni fedha za ndani.
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu Mstaafu Dkt. Eliezer Feleshi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainabu Telack wakifunua pazia baada ya kukata utepe wa kuashiria uzinduzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.
Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga lililozinduliwa leo na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu Mstaafu Dkt. Eliezer Feleshi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainabu Telack wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2