WAZIRI MPANGO: PPRA WANAFANYA KAZI NZURI, WAELIMISHE UMMA ZAIDI | Tarimo Blog


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) mara baada ya kutembelea banda hilo katika maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane na kueleza kufurahishwa na utendaji kazi wa Mamlaka hiyo, leo Mkoani Simiyu.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa. Florens Luoga alipotembelea banda la PPRA, kwenye maonesho ya Nanenane yaliyoadhimishwa kitaifa mkoani Simiyu.

Na Ripota wetu, Michuzi TV

WAZIRI Wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, leo Agosti 8, 2020 ametembelea banda la Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwenye Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane, yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Akiwa bandani hapo Waziri Mpango amesema kuwa anatambua kazi nzuri inayofanywa na PPRA na amewataka kuongeza wigo wa kutoa elimu ya ununuzi wa umma kupitia vyombo vya habari. 

Aidha, Waziri huyo amesema kuwa anasoma ripoti za ukaguzi unaofanywa na PPRA, na amewataka kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo wanayoyaibua.

“Mnafanya kazi nzuri sana, ripoti zenu nimezisoma vizuri sana na mnaniandikia vizuri lakini, msiishie kwenye kuibua matatizo tu, muwe pia sehemu ya kuyatatua,” amesema Waziri Mpango.

Akizungumzia maagizo ya Waziri Mpango, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Mahusiano kwa Umma, Bi. Winifrida Samba, amemshukuru  Waziri Mpango kwa pongezi alizozitoa kwa Mamlaka hiyo na kuahidi kufanyia kazi maagizo yake. 

Agosti 7, 2020, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga alitembelea banda hilo na kueleza kuwa anatambua kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi nzuri na wasipunguze kasi kutokana na kufisiwa. 

“Kweli kazi yenu tunaiona, mnafanya kazi nzuri. Zamani kidogo kulikuwa na changamoto, lakini kwa sasa kazi yenu tunaiona na tunaitambua, kwa hilo ‘we commend you’ (tunawapongeza),” alisema Profesa Luoga. 

Viongozi wengine waliotembelea banda la PPRA na kuwapongeza ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani, Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagin, Katibu Tawala wa Wilaya ya Busega, R. Rutagumirwa, Katibu Tawala wa Meatu, A. Rutaihwa. 

Wadau na wananchi mbalimbali walipewa elimu na kuhamasishwa kuwa sehemu ya usimamizi wa ununuzi wa umma, kwa kutoa taarifa PPRA pale ambapo wataona kuna dalili za uvunjifu wa sheria.

Mwisho.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2