AHSANTE DK.JOHN MAGUFULI KWA KUWAPA HESHIMA WASANII WETU...WANAOBEZA KAZI WANAYO OKTOBA 28 | Tarimo Blog

 


Na Said Mwishehe, Michuzi TV


LEO nataka kuzungumzia umuhimu wa wasanii wetu nchini na mchango wao katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kijamii  na kisiasa.


Kabla ya kuendelea kuelezea kuhusu wasanii naomba nimshukuru Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo , tunamshukuru kwa kuendelea kutupa afya njema, tunakushukuru kwa kuendelea kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi.


Mungu wetu tunakushukuru kwa kuamua jinsi ambavyo umeamua kuliweka taifa hili katika mikono yako miwili.Tunasema ahsante Mungu kwa kuendelea kuwafanya Watanzania kuwa wamoja kadri siku zinavyokwenda licha ya kuwa na dunia ambayo imejaa wabaya na wasioitakia mema Tanzania yetu.


Baada ya shukrani kwa Mungu sasa tunaendele na mazungumzo kuhusu wasanii wetu.Ukweli wasanii wamekuwa na mchango mkubwa kwa nchi yetu.Hata takwimu zinaonesha kuwa sekta ya sanaa ni miongoni mwa sekta ambazo zinamchango mkubwa katika pato la taifa.Sekta ya sanaa inashika nafasi ya tatu. Ndio!


Sekta ya sanaa imefanikiwa kuajiri makundi kwa makundi ya vijana wa Tanzania, wameamua kuwekeza katika sanaa na maisha yao yanakwenda , hawana tatizo na mtu.Wanaishi, wanasomesha, wanahudumia familia zao na wategemezi wao.


Ukitaka kujua hili vizuri kamuulize Ally Salehe Kiba a.k.a Ali Kiba. Ukitaka kujua umuhimu wa sanaa na wasanii kamuulize Nasseb Abdull a.k.a Diamond.Na ukitaka kujua umuhimu wa wasanii katika nchi yetu na mchango wao muulize hata Rajab Kahali a.k.aHarmonize a.k.a Tembo a.k.a Jeshi.


Kuna wasanii wengi tu ukiwauliza watakuwa na majibu kuhusu umuhimu wa sanaa na ilivyobadilisha maisha yao.Hata Masanja Mkandamizaji na Mpoki watakwambia.


Tunafahamu sekta ya sanaa ambavyo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua, wanatumia sanaa yao kuhamasisha Watanzania kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.


Kwa bahati mbaya wakati wasanii hao wakiendelea kushiriki kwenye ujenzi wa nchi yao, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwabeza, wamekuwa wakiwakejeli na  wamekuwa wakiwachafua bila sababu za msingi.


Chakufurahisha wakati kuna watu wakiwabeza wasanii Rais Dk.John Magufuli yeye ameamua kuonesha umuhimu wa wasanii, thamani ya wasanii, mchango wa wasanii na hata kile ambacho Serikali inapata kutokana na uwepo kwa wasanii hao.Ahsante Rais Magufuli ambaye kwa sasa unaendelea na mikutano yako ya kusaka kura.Hongera kwa kutambua wasanii na mchango wao katika nchi yetu.


Inasikitisha sana kuona baadhi ya wanasiasa wakiwabeza wasanii, lakini nafarijika kuona Rais wetu unavyoelezea umuhimu wa wasanii na mchango wao.Naona fahari unavyowajali na kuwathamini wasanii wetu.Umekuwa ukiwapa heshima hadharani.Upendo wake kwa wasanii sote tunaufahamu, tunaona na kubwa zaidi unaonesha kwa vitendo.Huenda wanaowasema vibaya wasanii ni kwasababu wanaona wengi wako kwenye kampeni zako.Wako kwako kwasababu wanastahili kuwepo.


Ni wasanii wa Tanzania na sio dhambi kufanya kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM.Kuna msemo unaosema kwamba unayekata naye kuni porini ndiye unayastahili kuotea naye moto.Dk.Magufuli amekuwa karibu na wasanii katika kipindi chote cha uongozi wake wa miaka mitano.


Pia tunafahamu hata kabla ya kuwa Rais Dk.Magufuli amekuwa mshabiki mkubwa wa kazi za sanaa.Ni jambo la kawaida kumuona akipiga tumba, akicheza na hata kuimba.Huyo ndio Dk.Magufuli anayejua thamani ya sanaa na wasanii.


Kuna ubaya gani leo wakiwa kwenye kampeni zake. Hongereni wasanii wa Tanzania.Kwanza mnafanya kampeni za mtu sahihi kwa ajili ya nchi yetu.Watanzania tulio wengi tunaungana na Rais Magufuli kuwapongeza wasanii wetu.


Dk.Magufuli akiwa kwenye mikutano yake ya kampeni za kuomba ridhaa kwa Watanzania kuhakikisha wanamchagua itakapofika Oktoba 28 mwaka huu, amekuwa akitumia nafasi hiyo kuzungumzia wasanii na mchango wao.Akiwa Bukoba Mjini mkoani Kagera Dk.Magufuli ameeleza kwa kina kabisa na kwa utulivu kuhusu wasanii.Wakati anazungumzia wasanii Dk.Magufuli alisema hivi " Mtu anasimama anasema wasanii hawana umuhimu katika maendeleo , lakini ukweli wasanii ni watu muhimu katika kuelimisha ustawi wa jamii wa watanzania.


"Pia ni watu muhimu hata kwa kuburudika , hata kama mtu umechanganyikiwa ukitikisa kichwa mambo yananyooka, nani hapendi muziki? Hata Kanisani wanapiga muziki, hata msikiti kuna Kaswida, muziki ni heshima, muziki ni upendo, muziki unajenga umoja.


"Muziki unaondoa mawazo ya watu, nani hamjui yule mama Said Kalori anayechanganya kama karanga, tamathali za semi zinatolewa na wasanii ...mambo safi, kwa hiyo hawa wasanii , waigizaji na michezo yote kwa ujumla ni vitu muhimu katika kujenga uchumi wa nchi yetu,"anasema Dk.Magufuli.


Anasisitiza na ndio maana matatizo yao yameendelea kutafutiwa ufumbuzi na kubwa zaidi wameamua kuyaweka katika Ilani ya CCM ya ili yaweze kushughulikiwa, lengo ni kuwaweka watanzania wanaoshikamana kwa ajili ya kujenga Tanzania yao.


Dk.Magufuli wakati anafafanua zaidi kuhusu wasanii anasema wengine hawana Ilani za uchaguzi ambazo zinatambua wasanii , pamoja na kwamba sekta ya wasanii ndio ya tatu katika kukuza uchumi wetu kwa takwimu za mwaka jana ,ikiongozwa na utalii, ikafuata ujenzi na mawasiliano.


Kwangu maelezo hayo ya Dk.Magufuli kuhusu wasanii yanathibitisha dhamira njema ya Serikali ya CCM ambavyo inajua umuhimu wa wasanii wetu.Ukimfuatilia Dk.Magufuli kuhusu wasanii utoana namna ambavyo moyo wake umejaa upendo dhidi yao na haishii kwenye upendo tu bali anawaheshimu.


Ni mara kadhaa tumeshuhudia Dk.Magufuli kwenye mikutano yake ya kampeni ambavyo amekuwa akivua kofia ambazo amevaa yeye na kuwavisha wasanii mbalimbali.Hii ni heshima kubwa sana kufanywa na kiongozi wa nchi kwa wasanii wetu.Ni heshima ambayo ni kubwa na ya kiwango cha juu.


Tunakumbuka Dk.Magufuli akiwa katika kampeni zake za kuwania urais za mkoani Mwanza alimpa kofia yake Diamond na hakuishia hapo akawa akiendelea kugawa kofia kama heshima maalum  anayoitoa kwa wasanii.


Amemvisha kofia Harmonize, amemvisha kofia Ally Kiba, amemvisha kofia Linex Sanda maarufu kwa Linex Mjeda , amemvalisha kofia Kala Jeremiah , amemvalisha kofia Stamina, amempa kofia mwanadada Snura Mushi na wasaii wengine kibao.Huyu ndio Dk.Magufuli, kofia ambazo anazitoa kama heshima  kwa wasanii inathibitisha kutambua na kuthamini mchango wao.Heshima ambayo anaionesha Dk.Magufuli kwa wasanii ni kubwa kuliko hata pesa.Ndio ukweli huo.


Pia naomba tuzungumze kitu hapa tena cha msingi kidogo.Fuatilia kwa makini, iko hivi kwa kuwa wasanii wengi wako CCM na wanazunguka na mgombea urais wa CCM Dk.Magufuli , wapo wanaobeza kuwa mikutano ya CCM inajaa kwasababu ya kuwepo kwa wasanii.Hizi ni hoja za kitoto sana na zinazoonesha kuishiwa kwa hoja.


Kwanza ni kweli mikutano ya kampeni ya Dk.Magufuli kuna wasanii na wapo kwasababu maalum nayo ni kuwa sehemu ya Watanzania kama walivyo wengine kushiriki katika kampeni hizo ambazo tunatafuta kiongozi sahihi kwa ajili ya Taifa letu.Hata hivyo kujaza kwa mikutano ya Dk.Magufuli moja kwa moja inatokana na mapenzi waliyonayo Watanzania kwake.


Kuna mikutano mingi ambayo inafanywa na Dk.Magufuli haina wasanii lakini bado idadi ya watu wanaojitokeza ni maelfu kwa maelfu.Ukitaka ushahidi fuatilia, nilikuwepo mkutano mkubwa wa Kasulu, Kibondo na hata uliofanyika jana Itigi.Hakukua na wasanii lakini idadi ya watu ilikuwa kubwa.


Tena kubwa sana.Watanzania wana mapenzi makubwa sana na Dk.Magufuli na wanaposikia kuna mahali atakuwepo wanajaa.Kwa kifupi Dk.Magufuli anapendwa sana na Watanzania na wasanii nao ni Watanzania na wanatamani kuwepo kila alipo.


Niwaombe wasanii , endeleeni kufanya kazi yenu, endeeleeni kufanya kampeni za mgombea urais wa CCM Dk.John Magufuli, mnafanya jambo jema.


Nyimbo zenu wasanii, maigizo yenu na kila mnachokifanya katika kipindi hiki cha kampeni kinawafurahisha wengi ukiondoa watazania wachache wenye roho mbaya na za kichawi wanaoshindwa kutambua thamani yenu.


Kwa kukumbusha tu wasanii hao nao ni wapiga kura, hivyo Oktoba 28 watakuwa na maamuzi yao juu ya nani ambaye wanaona anafaa kuongoza nchi ya Tanzania.Wasanii katika nchi hii wako wengi sana idadi yao ni kubwa, hivyo wakiamua kupiga kura kwa Dk.Magufuli unapata picha ya nini kinakwenda kutokea .


Wasanii hao hao wana familia zao, wana ndugu zao, wana marafiki zao, wana mashabiki wao ambao siku zote wanafanya kile ambacho wasanii wanakifanya.


Pata picha ya hao ambao wako nyuma ya wasanii halafu wewe endeelea kuwabeza tu.Kwa bahati nzuri wengi wameshaamua kura yao ni kwa Dk.Magufuli.Unaowabeza wasanii kazi wanayo Oktoba 28, mwaka 2020.

Mgombea Urais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi,Rais Dkt John Pombe Magufuli


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2