Serikali imeunga mkono mpango wa benki ya NBC kuwasafirisha wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa sekta ya madini nchini katika mataifa yanayofanya vizuri kwenye sekta madini ikiwemo Zimbabwe, Ghana na Msumbiji ili wakajifunze na kutafuta namna bora zaidi ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kiwango cha kimataifa.
Akizungumza wakati alipotembelea banda ya benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayoendelea mkoani Geita, Waziri wa Madini Bw Doto Biteko alisema serikali ipo tayari kushirikiana na benki hiyo katika kufanikisha ziara hizo ikiwa ni pamoja na kushauriana na wadau wote wakiwemo wachimbaji hao ili kuongeza tija katika safari hizo.
“Ili safari hizi ziwe na tija zaidi kwa walengwa Serikali ipo tayari kushirikiana na pande zote wakiwemo wachimbaji ili kufahamu nchi sahihi ambazo zimefanya vizuri kwenye sekta hii ili walengwa wapate wasaa wa kujifunza mambo ambayo yatawasaidia zaidi…hivyo nawapongeza sana benki ya NBC kwa mpango huu,’’ alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke alisema mpango huo umekuja kufuatia mafunzo maalum ya siku tatu yaliyotolewa na benki hiyo kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali katika sekta ya madini yaliyofanyika kwenye maonesho hayo.
“Malengo ya safari hizo haswa ni kutusaidia sisi sote yaani benki ya NBC na wateja wetu kwenye sekta ya madini ili kwa pamoja tukabadilishane uzoefu na wenzetu ambao pia wanafanya vizuri kwenye sekta hii. Kupita safari hizo tunatarajia makundi haya mawili wachimbaji yatajifunza namna mpya na bora zaidi ya kuendesha biashara zao ikiwemo namna ya kulifikia soko’’ alibainisha.
Alisema kupitia mafunzo hayo, benki hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wamebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wadau hao na hivyo kuwajengea uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto hizo wao wenyewe huku pia benki hiyo ikiahidi kutumia changamoto hizo katika kubuni huduma mahususi zinazolenga kuziondoa kabisa.
“Aidha kwasasa benki ya NBC ipo kwenye hatua za mwisho kuzindua huduma maalum kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini nchini ambayo kwa kiasi kikubwa inalenga kujibu changamoto zilitojwa na wachimbaji wadogo pamoja na wajasiriamali wakati wa mafunzo yetu,’’ alisema
Kwa mujibu wa Bw Masuke, wakati huduma hiyo mpya kwa wadau wa sekta ya madini ikiwa katika za mwisho kabla ya kuzinduliwa benki hiyo imeendelea kuwahudumia wadau hao kupitia huduma zake mbalimbali ikiwemo huduma ya Klabu ya Biashara, internet Banking na mikopo isiyo na dhamana ili kuwajengea uwezo wa kifedha wanapoendesha shughuli zao.
“Kupitia Klabu ya biashara tumekuwa tukiandaa safari za ndani na nje ya nchi ikiwemo China ambapo wateja wetu wamekuwa wakikutanishwa na wawekezaji mbalimbali na hivyo kuanzisha mahusiano ya kibiashara ambayo yamewaletea tija kubwa kwenye shughuli zao,’’ aliongeza.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo pamoja na kuishukuru benki hiyo walisema kupitia mafunzo hayo wameweza kufahamu namna bora ya kuweka mipango na mikakati ya kukuza biashara zao, namna ya kutafuta masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi, mambo yanayoangaliwa na mabenki kabla ya kupatiwa mkopo pamoja na kufahamu sababu zinazosababisha biashara zao zife.
Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke (Kulia) akimkaribisha Waziri Madini Bw Doto Biteko ( Kushoto) kwenye banda la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayoendelea mkoani Geita.
Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo wadau wa sekta ya madini nchini. Anaemsikiliza ni Waziri wa Madini Bw Doto Biteko (Kulia)
Waziri Madini Bw Doto Biteko (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke (Kushoto).
Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje (kushoto) akifafanua kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wadau wa sekta ya madini nchini kwa Waziri wa Madini Bw Doto Biteko (Kulia) wakati waziri huyo alipotembelea banda ya benki hiyo lililopo kwenye maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayofanyika mkoani Geita. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel.
Waziri wa Madini Bw Doto Biteko (katikati) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (Kulia kwake) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke (Kushoto kwa Waziri) wakati viongozi hao walipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayofanyika mkoani Geita.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa
KUBOFYA HAPA
Post a Comment