Benki ya NBC, Ofisi ya Mkoa Geita waendesha mafunzo ya biashara na ufanisi kwa wajasiriamali na wachimbaji wadogo Geita.
Geita: Septemba 17, 2020: Wajasiriamali na wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita wameanza mafunzo maalumu yanayolenga kwa kuwajengea uwezo wa kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kwa viwango shindani vya kimataifa, shukrani zikielekezwa kwa Benki ya NBC pamoja na wadau wengine kwa kuratibu na kuendesha mafunzo hayo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamezinduliwa rasmi leo mkoani Geita na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel kwenye maonesho ya dhahabu na teknolojia yanayofanyika mkoani humo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mhandisi Gabriel ametoa wito kwa wafanyabiashara na wachimbaji wadogo mkoani humo kuzingatia kanuni za utunzaji wa fedha na heshima ya matumizi ili kulinda na kukuza mitaji yao huku akiipongeza benki ya NBC kwa kuwewezesha utolewaji wa mafunzo hayo.
“Ninaomba sana wajasiriamali na wachimbaji wa dogo kupitia mafunzo haya muweze kubadilika na mtoke kwenye mfumo wa kufanya shughuli zenu kwa mazoea na badala yake muhamie kwenye mfumo wa kisasa unaoheshimu ushauri wa wataalamu wakiwemo wataalamu kutoka taasisi za fedha ikiwemo benki ya NBC na mamlaka nyingine zinazosimamia biashara nchini.” Alisisitiza.
Alisema iwapo wadau hao watatumia vizuri rasilimali madini hususani dhahabu ni rahisi kwao kufanikiwa huku akitolea mfano mabadiliko ya kisera na kiutendaji yalivyoongeza mapato yanayopatikana kutokana na madini katika mkoa huo.
Alitaja baadhi ya mada muhimu kwenye mafunzo hayo kuwa ni pamoja na taratibu bora za uchimbaji madini, umuhimu wa ulipaji kodi na taratibu za kufuata, matumizi sahihi ya taasisi za kifedha na upatikanaji wa mitaji, umuhimu wa kuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na matumizi sahihi ya kemikali katika shughuli za uchimbaji madini.
“Mwisho wa mafunzo haya tunaamini walengwa watapata kufahamu namna bora ya kuweka mipango na mikakati ya kukuza biashara zao, namna ya kutafuta masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi, mambo yanayoangaliwa na mabenki kabla ya kumpa mfanyabiashara mkopo, sababu zinazosababisha biashara nyingi zife na tabia za muhimu kwa mfanyabiashara,’’ alisema.
Kwa upande wake Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje alisema pamoja na kuzitambulisha fursa za huduma na bidhaa za kibenki ikiwemo huduma ya Klabu ya Biashara, internet Banking na mikopo isiyo na dhamana kutoka benki hiyo, mafunzo hayo pia yatawasaidia walengwa hao kuzitambulisha fursa za kibiashara ambazo wajasiriamali na wachimbaji wadogo hususani wa mkoa wa Geita na mikoa ya jirani wanaweza kunufaika nazo.
“Benki ya NBC tumekuja na mkakati huu mahususi wa mafunzo kwa wafanyabiashara kutokana na matokeo ya tafiti za kitaalamu zinazoonesha kuwa, takribani zaidi ya asilimia 70 ya biashara zote zinazoanzishwa hufa na kupotea kabisa ndani ya mwaka mmoja, na hili linatokana na sababu kadhaa ikiwemo kukosekana kwa mbinu za uongozi mzuri wa biashara ’’ alitaja.
Alitaja sababu nyingine zinazoathiri biashara za wajasiriamali hao kuwa ni kukosekana kwa utaalamu katika maeneo muhimu ya biashara na Kukosekana kwa uelewa mzuri wa mambo ya kifedha katika kuziendesha biashara.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo pamoja na kuwashukuru waratibu wa mafunzo hayo ikiwemo benki ya NBC, walisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo wa kuziendesha biashara zao kwa ufanisi na kwa faida.
“Kupitia mafunzo haya tunatarajia kunufaika katika maeneo tofauti yakiwemo kujua namna ya kutunza kumbukumbu za biashara, Ubora wa bidhaa na huduma kwa wateja, Uongozi wa kibiashara, na namna ya kutangaza biashara zetu,’’ alisema mmoja wa wajasiriamali hao Bi Neema Matta.
Mbali na Benki ya NBC mafunzo hayo yanaendeshwa na wataalamu mbalimbali kutoka TANTRADE, Tume ya Madini, TRA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, GST, SIDO, NEMC, TBS, OSHA, NEEC, na taasisi nyingine za kifedha.
Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel (katikati) akizungumza na wajasiriamali pamoja na wachimbaji wadogo (hawapo pichani) wakati akizundua mafunzo maalumu ya siku tatu kwa wajasiriamali hao yanayofanyika kwenye maonesho ya dhahabu na teknolojia mkoani humo. Wengine ni pamoja na Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje (Kulia) ambapo benki hiyo ni mdhamini mkuu wa mafunzo hayo.
Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.
Meneja Benki ya NBC tawi la Geita Bi Hilda Bwimba, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.
Baadhi ya wajasiriamali na wachimbaji wadogo mkoa wa Geita wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje (kushoto) akimsindikiza Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel mara baada ya kufungua mafunzo hayo.
Meneja Mahusiano wateja binafsi benki ya NBC Tawi la Mwanza Bi Mariam Benjamin akimhudumia mmoja wa wateja alietembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye maonesho ya dhahabu na teknolojia mkoani humo Geita.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa
KUBOFYA HAPA
Post a Comment