Mgombea Ubunge Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA), Rehema Mkoha, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kupekuliwa na polisi usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake eneo la Mandewa akidaiwa kumiliki silaha za moto na kushambuliwa na askari hao. Kulia ni Aneth Joel akiwa amefunga bandeji mguuni kwa madai ya kipigo cha polisi.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Singida, Mutta Adrian akizungumzia tukio hilo. Wengine waliosimama nyuma ni vijana waliokuwemo nyumbani mwa mgombea ubunge huyo
Mgombea Ubunge Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA), Rehema Mkoha, akizungumzia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Unyakumi, Mossy Athumani, akizungumzia tukio hilo.
Baadhi ya wanachama wa Chadema wakisikiliza wakati wa kuelezea tukio hilo.
Nyumba ya mgombea ubunge huyo iliyofanyiwa upekuzi.
Aneth Joel akisimulia tukio hilo. Kushoto ni Bathromayo Chiza mmoja wa vijana aliyekuwa kwenye nyumba hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Singida
JESHI la Polisi Mkoani Singida limefanya upekuzi nyumbani kwa Mgombea Ubunge Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rehema Mkoha na kumkamata na watu wengine 10.
Mkoha alikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kuwa nyumba anayoishi anamiliki silaha za moto kinyume cha sheria.
Tukio hilo limekuja siku chache tangu chama hicho kizindue kampeni zake za uchaguzi ngazi ya mkoa uliofanyika kiwanja cha Bombadia zamani Peoples na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi na wafuasi wa chama hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbert Njewike akizungumza kwa njia ya simu, alikiri kukamatwa kwa mgombea huyo na watu wengine na kisha kuachiwa baada ya kuhojiwa ambapo watatakiwa kuripoti tena polisi kesho (Ijumaa).
Kamanda Njewike alisema kabla ya kuwakamata walifanya upekuzi ndani ya nyumba ya mgombea huyo baada ya polisi kupata taarifa kuwa anamiliki silaha za moto.Hata hivyo majina ya watu wengine waliowakata hakuyataja.
"Tulipomkamata mgombea huyo na vijana wengine wanaoishi ndani ya nyumba hiyo tuliwaachia kwa dhamana na tunaendelea na uchunguzi tumewaambia waje leo kwa mahojiano zaidi," alisema Kamanda Njewike.
Awali mgombea ubunge huyo alieleza kuwa usiku wa kuamkia juzi saa 8.30 usiku wakiwa na kama saa 1.30 waingie kulala baada ya kumaliza kikao chao cha kujipanga kwa ajili ya kuendelea na mikutano ya kampeni alishutuka kusikia milango ikigongwa kwa nguvu huku wakiamliwa wafungue milango.
Alisema alitoka chumbani kwake na vijana wake na kumuona mtu akiwa ameshika mtutu wa bunduki hivyo wakawa wanajiuliza wafanyeje kwani kwa jinsi walivyo ni lazima wataingia ndani na hawakuwa na uwezo wa kupambana nao.
" Wakati narudi chumbani kwangu watu hao walifanikiwa kubomoa mlango wa mbele na kuingia ndani na moja kwa moja walipitiliza kwenye vyumba mbalimbali na walipofika kwenye chumba changu walikuta nimefunga mlango ili niweze kutoa taarifa kwa watu wengine na wakati napiga simu ndipo walipouvunja mlango wa chumba changu," alisema Mkoha.
Alisema wakati huo yeye alikuwa amejificha bafuni ambapo walimkamata Aneth Joel waliyekuwa naye chumbani na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi.
Alisema baada ya hapo walimkamata huku mmoja wao akimuelekezea mtutu wa bunduki na mwingine akimshambulia mara nne kwa kutumia gongo na baadae walitolewa na kuwekwa sebuleni ambapo walianza kuwahoji na kujitambulisha kuwa ni askari polisi na kwanini walipokuwa wakigonga mlango hawakuwafunguliwa.
Katika kundi la askari hao alikuwepo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Unyakumi waliyemtaja kwa jina la Mossy Athuman ambapo walichukua maelezo yao na walipo muuliza yeye ni nani alisema ni mgombea wa ubunge kupitia Chadema.
Alisema askari hao waliwaambia kuwa wamefika hapo kwa kujihami na kufanya upekuzi baada ya wasiri wao kuwaeleza wanamiliki silaha za aina mbalimbali.
Baada ya hapo askari hao walimwambia kuwa wanataka kufanya upekuzi ambapo alimuita mmoja wa jirani yake awe shuhuda wa tukio hilo.
Alisema baada kufanya upekuzi huo askari hao walichofanikiwa kupata panga moja la matumizi ya nyumbani na kifaa kimoja kidogo kama nyundo, kisu, bisibisi na kifungulio cha soda (opena ambavyo walivichukua kama ushahidi.
Alisema baada ya upekuzi huo waliwachukua hadi kituo cha polisi kwa hatua nyingine ambapo pia waliambiwa wajiwekee dhamana lakini walikataliwa kupewa PF3 ili wakatibiwe kutokana na majeraha waliyopata kutokana na kipigo cha askari.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa eneo hilo Mossy Athumani alisema alipigiwa simu na mmoja wa askari polisi aliyemtaja kwa jina moja la Yasini kuwa watakuwa na kazi ya kupekua nyumba moja katika eneo lake inayodaiwa kuhifadhiwa silaha za moto na walipofika katika nyumba hiyo hawakukuta silaha zozote zaidi ya panga na kifaa hicho chenye bisibisi.
Kufuatia tukio hilo, Chadema kimelaani tukio hilo ambalo wamelihusisha na masuala ya kisiasa na wakaliomba Jeshi la Polisi lisitumike kisiasa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment