MGOMBEA URAIS CCM DK.JOHN MAGUFULI AINGIA KWA KISHINDO MKOANI KAGERA... | Tarimo Blog

*Atoa ahadi kutatua changamoto katika zao la kahawa, kupeleka neema Kemondo

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-KAGERA

AMEINGIA kwa kishindo Kagera!Ndivvyo unavyoweza kumuelezea Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu Dk.John Magufuli ambaye leo ameingia mkoani Kagera akitokea mkoani Geita huku akitumia nafasi hiyo kuzungumzia mikakati iliyopo katika kutatua changamoto ya zao la Kahawa ambalo ni la kimkakati.

Pamoja na mambo mengine Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kuelezea maendeleo ambayo yamefanyika katika maeneo mbalimbali ya Kagera na mikoa mingine nchini kwa ujumla na alipokuwa eneo la Kemondo aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali katika miaka mitano imefanya kazi kubwa ya kuboresha usafiri wa meli katika Ziwa Victoria na mkakati ni kuendelea kuboresha zaidi usafiri huo.

Dk.Magufuli kabla ya kuanza kuelezea mipango iliyopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi hao kuhakikisha katika uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Oktoba 28 kura zote wapeleke kwa CCM ili waendelee kupata maendeleo huku akiwataka kutochagua watu wasioaminika na watakaotawala kwa matakwa ya wengine.

Kuhusu zao la Kahawa , Dk.Magufuli amesema anajua kwamba kuna changamoto ambazo zinalikabili zao hilo na tayari wamelibeba kwa ajili ya kuanza kulifanyia kazi.

"Tumeanza kutatua changamoto katika zao hili la kahawa ambalo ni zao la kimkakati.Wiki mbili nimezungumza kwa simu na Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Waziri wa Kilimo ndio maana wakatuma makatibu wakuu waje huku Kagera."

Amesisitiza kuwa anataka kumaliza matatizo ambayo yapo kwenye zao hilo ili wakulima na wananchi wanufaike nalo huku akifafanua Serikali inatekeleza miradi mikubwa hivyo haiwezi kushindwa kutatua changamoto za zao hilo."Tunataka tumalize matatizo ya kahawa moja kwa moja".

Wakati akielezea zao hilo la Kahawa, Dk.Magufuli amewasisitiza wananchi katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wahakikishe wanamchagua yeye kuwa Rais kwa miaka mitano mingine pamoja na wagombea ubunge na udiwani wanaotokana na CCM."Maendeleo hayana Chama na ndio maana hata yeye anatekeleza miradi katika maeneo yote nchini.

Kwa upande mwingine Dk.Magufuli amezungumzia usafiri wa meli katika bandari ya Kemondo ambapo amesema bandari hiyo iliachwa na Mwalimu Julius Nyerere na imeleta utajiri mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na mkoa wa Kagera kwa ujumla.

"Wote tunakumbuka ni zaidi ya miaka 20 imepita tangu Meli ya MV Bukoba ilipopinduka na tangu wakati huo haijawahi kurudi tena na kusababisha watu wengi waliokuwemo siku hiyo kuiachia njiani. Hatukuweza kuleta meli nyingine,"amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza kwamba anamtanguliza Mungu ili anayopanga yakatimie na hivyo kuwaondolea machungu wananchi wa Bukoba na Kemondo.Amesema katika miaka mitano iliyopita amefanya yanayowezekana ikiwemo kuboresha meli .

"Tumefanya yaliyowezekana ili kupata fedha kwa ajili ya kuboresha usafiri wa meli na miundombinu katika Ziwa Victoria, tumebana mafisadi tukapata Sh.bilioni 152.Tumekarabati meli tano na hatukuishia hapo kwani tumenunua meli kubwa kuliko MV Victoria.

"Inauwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo, itaitwa MV Mwanza.Meli ya MV Victoria tumeinununulia injini mpya na itakuwa inakuja na hapa Kemondo,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza watabadilisha mazingira kwani wanataka iwe bandari kubwa ili watu kufanya biashara, tumeanza na meli na tutapabadilisha hapa.

"Nimekuja tena kuomba kura, nina sababu za msingi kuwaombea kura wabunge na madiwani ili tukaongee lugha moja tukamalize kazi.TulimrudishaMgombea Ubunge jimbo la Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza kwanza alishinda kura na pili ni Katibu wa wabunge. "Walipoondoka wabunge wa upinzani bungeni kwa kuogopa Corona, Rweikiza alisema wataendelea kubaki ili kupitisha bajeti ya kununulia meli na kuleta maendeleo. Ameniomba tulete gridi ya taifa nimeridhia. Siku nikishinda wanikumbushe hata Karagwe umeme unakatikatika hatuwezi kuishi maisha haya,"amesema Dk.Magufuli

Amesisitiza anataka umeme ukiwaka uwe unawaka moja kwa moja na ndio maana wameanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawati 2115 katika bwawa la Julius Nyerere na umeme utakaozalishwa hapo utasambazwa nchini kote.
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2