* Huduma za Afya, Maji, Miundombinu na Umeme kuzidi kupewa kipaumbele zaidi.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MAKAMU Wa Rais na mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan amesema kuwa wanajipanga kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na hiyo ni kufuatia elimu bure inayotolewa katika shule za umma na kupeleka wanafunzi wengi kutoka shule hizo kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kampeni za Urais, Ubunge na udiwani katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 katika Wilaya ya Ilala na Temeke Mama Samia amesema kuwa;
"Katika kipindi cha miaka miaka mitano elimu imekuwa ikitolewa bure katika shule za Umma na wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri...tumejipanga kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ili vijana wanaotoka katika mazingira duni wasome hadi Chuo kikuu bila shida na kutimiza ndoto zao" ameeleza Mama Samia.
Awali Samia aliwasilisha salamu kutoka kwa Rais na mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dkt.John Joseph Magufuli ambaye amewashukuru Wana Dar es Salaam kwa ushirikiano mkubwa aliopewa na watanzania na amehaidi kuja kuongea na wakazi wa jiji hilo.
Samia amesema kuwa wana Dar es Salaam wamekuwa wanufaika wa miradi mbalimbali ikiwemo Flyover, madaraja, ndege zilizonunuliwa pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege wa wa kimataifa wa Julius Nyerere pamoja na miundombinu ya barabara.
Aidha amesema kuwa miaka mitano mitano ijayo wataimarisha miundombinu katika maeneo yanayoathirika na mafuriko ikiwemo jangwani, pamoja na ujenzi zaidi wa barabara za mwendokasi, na kuwataka wananchi wakiwemo wanachama wa chama hicho kuchagua Serikali ya CCM ili kuleta maendeleo zaidi.
"Bakora tuliyojipiga miaka ile isijirudie kwa kuwa hakuna Chama kinachoweza kuipiga CCM, katika miaka ijayo tunaahidi kufikisha huduma ya umeme katika kila eneo ili kujenga uchumi wa viwanda, vijiji 9500 vimepata umeme miaka miwili ijao tatizo la umeme halitakuwepo, ndege zaidi zitanunuliwa zikiwemo za mizigo...tunajenga Tanzania ya maendeleo." amesema Mama Samia.
Vilevile katika kipindi cha miaka mitano ijayo kupitia ilani ya CCM amehaidi kujenga shule, mabweni na miundombinu mingine pamoja na kuboresha vyuo vya ualimu ili kutoa walimu bora wakiwemo wa sayansi, pamoja na kuimarisha mafunzo ya lugha ya kiswahili kimataifa.
Katika sekta ya Afya Samia amesema kuwa katika miaka mitano ijayo wataendelea kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto ambavyo ni vipaumbele, na hiyo ni pamoja na kuimarisha mifuko ya bima ya Afya na kuhakikisha kila mwananchi anamiliki bima ya afya, na wataanza ujenzi wa vituo vya afya katika kila Halmashauri, wakimaliza mhula kila kata nchini ina kituo cha afya.
Pia katika sekta ya Utalii Samia amesema kuwa mikakati zaidi ya kuongeza watalii nchini itazingatiwa na hiyo ni pamoja na kuandaa vipindi vya utalii vitakavyorushwa nje ya nchi pamoja na kuweka mikakati ya kukomesha ujangili nchini.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa ufunguzi wa kampeni za Urais,Ubunge na Udiwani katika Wilaya ya Ilala, leo jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais na mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia tiketi ya CCM Samia Suluhu Hassan akihutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Ilala waliojitokeza kusikiliza sera kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi, Samia amesema kuwa kwa mhula uliobaki changamoto za maji, umeme na afya zitakuwa zimetatuliwa na huduma hizo zitakuwa zimefika kwa kila mwananchi, leo jijini Dar es Salaam.
.Makamu wa Rais na mgombea mwenza wa kiti cha Urais kupitia tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na mmoja wa wahamasishaji wa kampeni ya "Mama Ongea na Mwanao" Tausi Mdegela mara baada ya kuwasili katika viwanja wa Tabata shule kwa ajili ya kuzindua kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani katika Wilaya ya Ilala, ambapo amehaidi neema kubwa kwa watanzania kwa mhula wa miaka mitano ijayo, leo jijini Dar es Salaam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment