*Awaahidi makubwa,awaambia Tabora ni mkoa wenye historia kubwa
*Asema amebakia na deni la kuhakikisha anapelekea maendeleo
Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Tabora
WAMEVUNJA rekodi!Ndivyo unavyoweza kuzungumzia maelfu ya wananchi wa mkoa huo ambao wamejitokeza kumsikiliza Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ambaye leo amefanya mkutano wake wa kampeni mkoani hapa.
Akizungumza leo Septemba 21,2020 mbele ya wananchi hao, Dk.Magufuli amesema mapokezi ambayo ameyapata Tabora yamefunika kwani ni makubwa na yanamfanya abaki na deni kwa wananchi hao.
"Mkoa wa Tabora unahistoria kubwa, katika historia hata ya kutafuta uhuru Mkoa wa Tabora ulihusika, najisikia raha kweli. Tabora naifahamu , Tabora ya miaka ile sio ya sasa, nyumba nzuri zimejengwa kila mahali, Tabora imebadilika kweli kweli, hata barabara za lami zimeongezeka.
"Tabora ndio ilikuwa ni Mkoa wenye kilometa chache za lami, ilikuwa ni hapa tu mjni, leo mabadiliko makubwa, tumetoka mbalimbali na tuko mbali.Wasione vyaelea vimeundwa.Mwaka 2015 niliahidi mambo mawili, kutatua changamoto ya maji , pili miudombombinu,"amesema Dk.Magufuli.
Kuhusu maji amesema kuwa yametoka Ziwa Victoria kuja Tabora na kisha kupelekwa katika wilaya nyingine za Mkoa huo na kwamba yametoka Ziwa Victoria kwenda Nzega kwa Sh.bilioni 600."Leo watu wa Tabora wameanza kupata maji kutoka Ziwa Victoria.Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 92, vijiji zaidi ya 500 vitanufaika kwenye maeneo ambayo bomba linapita.
"Mradi utakapokamilika utamaliza tatizo la maji Mkoa wa Tabora, sambamba na mradi huo tumetekeleza miradi mingine 50, mradi wa gombe hadi Kaliua uliogharimu zaidi ya Sh.bilioni 19. Katika miaka mitano tumepanga kutekeleza mradi wa maji . tunataka kufikisha maji kwa asilimia 95 kwa Mkoa wa Tabora,"amesema Dk.Magufuli.
Kuhusu miundombinu ya barabara , amesema waliahidi kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa huo na kwa sehemu kubwa wamefanikiwa kutekeleza na kwamba kupitia mradi wa kuendelea miji 18 wamefanikiwa kujenga barabara nyingi za lami katika Mji wa Tabora pamoja na kuweka taa za barabarani na sasa mkoa huo umekuwa kama Toronto.
"Ni kazi ya CCM, ndugu zangu tumeendelea na programu ya kuhakikisha Mkoa wa Tabora unaunganishwa na barabara pande zote, Tabora nilikuwa nakuja nikiwa Waziri wa Ujenzi, wafadhili hawakutaka kutoa fedha kwa ajili ya mkoa wa Tabora, wakati wa Mkapa , na wakati wa Kikwete(marais wastaafu) tuliamua kufanya mageuzi.
"Ukitoka hapa kwenda Nzega ilikuwa vumbi, ukitoka Tabora kwenda Itigi mpaka Manyoni ilikuwa vumbi imejaa, tumefanya makubwa, barabara ya kutoka Nzega hadi Tabora ni lami, Tabora kwenda Kaliua lami, na tunaendelea sasa twende mkapa Kigoma, mpaka Nyakanazi.
"Ndio tuliamua Sh.bilioni 567 zikatengneze lami, Tabora , Sikonge mpaka Katavi wakandarasi wamejaaa, wasione vyaelea vimeundwa.Tumefanya haya kwasababu tulikuwa na sababu ya kufanya, mlituchagua kwasaababu ya kufanya kazi.
"Zaidi ya hapo tumefanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege Tabora, mwaka 2017 nilikuja kuzindua mradi huo na sasa tunataka kuanza ujenzi wa jengo la abiria, tumepanga kufanya upanuzi wa eneo la ndege kuruka na kutua, hiyo itachochea shughuli za utalii.Kama mnavyofahamu kuna Hifadhi ya Kigosi na hifadhi ya mto Ugala.
"Tunataka watalii wawe wanakuja Tabora, wanacha dola ,wanaacha fedha kama wanavyofanya Kaskazini.Sambamba na hayo kuhusu miundombinu ya usafiri tunaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa, kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, na kisha Dodoma kuja Tabora.
"Na baada ya hapo Tabora Mwanza na ikifika hapo nyingine inakwenda Kigoma na pale Isaka itakwenda mpaka Kigali.Lengo ni kuhakikisha Tabora inajengwa kiuchumi, uchumi wa kweli, uchumi wa kisasa,",amesema.
Dk.Magufuli ambaye amefika kwa wananchi hao kwa ajili ya kuwaomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, amesisitiza Tabora kuwa Sh.bilioni 39.66 zimetumika kwa ajili ya kujenga na kuarabati miundombinu ya elimu.Wakati Sh.bilioni 42.5 kwa ajili ya elimu bila malipo.
" Mlituchagua ili tufanye kazi, tumejitajidi kufanya kazi, katika miaka mitano iliyopita tumejenga hospitali za kanda tatu,bajeti ya dawa imeongezeka.Tumefanya mambo mengi na wabunge wameeleza mambo yaliyofanywa katika maeneo yao.
"Naamini wananchi wa Tabora mnafahamu yaliyofanyika kwenye maeneo yote, tunasimama hapa kwa upendo mkubwa kuwaomba kura.Nataka kuwakikishia watu wa Tabora mkitupa ridhaa tutafanya mambo makubwa sana,"amesema Dk.Magufuli.
Ameongeza nchi yetu wakati wa miaka mitano ilikuwa ikihesabika nchi yenye umasikini wa kutupwa lakini leo hii imeingia uchumi wa kati, uchumi unakuwa kwa kasi kubwa."Naomba mtuamini, najua kwa umati huu bado mnatuamini, mnataka tukafanye kazi kubwa. ndio maana nasimama hapa kuomba mturudishie na mbunge wa hapa.
"Katika kampeni huwa kuna mambo mengi, ndani ya CCM kuna michakato yetu ya kutafuta mgombea ubunge au udiwani, hata kwenye urais mwaka 2015 tulikuwa 42 lakini amebaki mmoja.Umati wa watu waliohudhuria hapa ni mkubwa sana, kwani mimi nani, sina cha kuwalipa. tukaendelee kujenga umoja wetu."
Wakati huo huo Dk.Magufuli amesema amesikitishwa na kitendo cha fedha ambazo alichanga Sh.milioni 10 na Sh.milioni tano ambazo zilichangwa huko nyuma kwa ajili ya Kituo cha Afya Uyui zimeliwa.
"Nimesikitika leo miaka kadhaa nilichangia Shilingi milioni 10 na mbunge alichangia Sh.milioni tano, Uyui kwa ajili ya kituo cha afya.Hata hivyo napongeza kwa kuanza kuwachukulia hatua watu waliohusika kula hizo fedha, hata CCM mafisadi yapo na ndio maana napongeza uongozi wa Mkoa na Wilaya husika kwa kuchukua hatua kwa waliohusika, wako watatu, hayo ndio majipu, sitaki kuingilia mambo ya Mahakamani,"amesema Dk.Magufuli.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment