Tume ya Madini kupitia wataalam wake imeendelea kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za wachimbaji wa madini katika Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea katika Uwanja wa Kituo cha Uwekezaji Bomba Mbili Mjini Geita.
Taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Madini zinazoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Mgodi wa STAMIGOLD.
Akizungumza katika maonesho hayo Mtakwimu wa Tume ya Madini, Azihar Kashakara amesema kuwa kati ya changamoto zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli zao za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika mkoa wa Geita ni pamoja na migogoro kati yao wenyewe, kutosajili makubaliano yao(mikataba) katika mamlaka husika, uelewa mdogo wa sheria ya madini , kanuni na taratibu na uelewa mdogo juu ya masuala yanayohusu mazingira,afya na usalama migodini.
“Wapo wachimbaji wadogo walioonesha kushindwa kutofautisha kati ya hati ya kumiliki ardhi na leseni za madini hali inayopelekea migogoro kwenye shughuli zao za uchimbaji wa madini, tumewapa elimu ya kutosha,” amesisitiza Kashakara.
Katika hatua nyingine wataalam wa Tume ya Madini wameendelea na zoezi la kuwasajili wadau wa Madini kwenye mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao (online mining cadastre transactional portal (OMCTP).
Akielezea manufaa ya mfumo huo, Kashakara ameeleza kuwa ni pamoja na kuwawezesha wadau wa madini kuomba leseni za madini kupitia mfumo huo pasipo kufika kwenye ofisi za Tume ya Madini, kuongeza uwazi na kasi ya utoaji wa leseni za madini, wateja kupata taarifa za leseni na maombi yao kupitia mfumo huo.Ameeleza manufaa mengine ni pamoja na wateja kusimamia leseni zao pamoja na kuhuisha taarifa zao kupitia mfumo huo.
Wakati huohuo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Makolobela Mayigi ametembelea banda la Tume ya Madini na kupongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na waelimishaji.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment