*Ni kauli ya Dk.Magufuli alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi Geita, ataja maendeleo yaliyofanyika
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Geita
MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na Mwenyekiti wa Chama hicho Dk.John Magufuli amesema mkakati wa Serikali uliopo ni kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kupewa nafasi zaidi ikiwa pamoja na kuanzisha hifadhi nyingine za taifa za utalii katika kanda zote nchini.
Amesema hayo leo Septemba 9,2020 mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Geita alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ambapo amesema Geita mbali ya kunufaka na madini, imekuwa na eneo la utalii, hivyo imeanzishwa hifadhi ya Burigi Chato ambayo ni ya tatu kwa ukubwa, hivyo ni fursa kwa wana Geita kufanya maendeleo.
Dk.Magufuli ambaye ni Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesisitiza "Tunataka kila kanda kuwepo na utalii, zamani ilikuwa utalii ni Kaskazini tu lakini sasa tumeamua na tutakuwa tunaanzisha hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini kwetu.Kila mahali kuwepo na hifadhi za taifa za utalii, ndio maana tunajenja uwanja wa ndege wa kimataifa Mwanza, ili watalii wakija wanavuka daraja la Busisi wanakuja na huku.
"Tuanze kuchangamkia fursa, watu waanze kujenga nyumba za kulala wageni(Gesti) kwa ajili ya watalii.Tunataka fedha ambazo zinatokana na utalii ziongezeke, hata hili Ziwa Victoria ni utalii na kwa kuendelea kufungua milango ya utalii nchini kwetu tunaamini tutaweza kuleta maendeleo,"amesema Dk.Magufuli
Wakati huo huo Dk.Magufuli amezungumzia kuhusu kilimo, uvuvi na ufugaji ambapo amesema wametoa kipaumbele kikubwa kuendelea sekta hiyo na kwamba wanataka wakulima , wafugaji na wavuvi nao wafaide huku akieleza katika kipindi cha miaka mitano kuna hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa ikiwemo ya kufuta 114.
Pia amesema mkakati uliopo kwa Mkoa wa Geita ni kujengwa kwa machinjio ya nyama ya kisasa na ujenzi wake unatarajia kutumia Sh.bilioni saba."Tunataka nyama inayochinjwa hapa ikitoka hapa inakwenda moja kwa moja Ulaya. Masuala ya kilimo, ufugaji na uvuvi yamefafanuliwa katika ukurasa wa 33 hadi 56 ya Ilani ya Uchaguzi.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Dk.Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano barabara za lami zenye urefu wa kilometa 123.23 zimejengwa na kwamba wananchi wa Geita ni mashahidi kwani hata mji huo haukuwa na barabara za lami kama ilivyokuwa sasa hivi.
"Barabara za lami zimeanza kuchomoza katika maeneo mbalimbali , miaka mitano ijayo tutatengeneza zaidi ya ilivyo sasa. Kuna babarabara ya Nyahunga -Ushilombo yenye urefu wa kilometa 52, tumejitahidi kujenga barabara za lami na tutaendelea na tumepanga barabara ya Geita kwenda Kahama itajengwa kwa kiwango cha lam,"amesema Dk.Magufuli.
Kuhusu huduma za jamii, Dk.Magufuli amesema miaka mitano iliyopita huduma zimeboreshwa katika sekta ujenzi wahospital za rufaa, hospitali za kanda na hospitali ya rufaa ya Geifa, hospitali za wa wilaya nne pamoja na kuongezwa kwa watumishi wa umma ambako kwa Geita wameajiriwa watumishi wa afya 192.
Katika elimu amesema nako kazi imeendelea kufanyika kwa kuendelea kujenga shule za msingi, sekondari, kukarabati shule kongwe huku akielezea kujengwa kwa madarasa 1,539 na hayo ni katika mkoa wa Geita peke yake, sekondari 27, nyumba za walimu 162, na kiasi cha Sh.bilioni 35 .3 zimetumika kwa ajili ya elimu bila malipo katika mkoa huo.
Pia amezungumzia mafanikio ambayo yamepatikana kwenye sekta ya nishati ya umeme ambapo vijiji vingi vimepata umeme na vichache vilivyobakia vitamaliziwa.Ndio maana ndugu zangu naomba tena miaka mitano tukafanye majaabu katika nchi hii.
"Mambo ni mengi, tumetoka mbali na tunakwenda mbali. najua pamoja na utekelezaji wa mradi wa maji wa Sh. bilioni 36.5.Mji wa Geita kuna maeneo ambayo bado maji hayajafika maeneo mengine, kazi hiyo tutaifanya na Mji wa Geita uko katika miji 28 na Sh.bilioni 130 zimeshatengwa kwa ajili ya maji kwa Mkoa wa Geita,"amesema Dk.Magufuli.
Pamoja na hayo amewaeleza wananchi wa Geita kuwa Sh.bilioni 29 zimekwenda katika Mkoa huo kwa ajili ya kusaidia kaya masikini kupitia mfuko wa TASAF na kusisitiza Serikali itaendelea kusaidia kaya masikini kupitia mfuko huo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment