Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Chato
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Geita Vijijini mkoani Geita Joseph Kasheku ‘Msukuma’ amesema katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 , wananchi wa Chato wanatakiwa kupiga kura zote za ndio kwa Dk.John Magufuli.
Msukuma amesema hayo leo Septemba 14, 2020 wakati akitoa salamu kwa maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Chato na maeneo jirani ambao wamehudhuria mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM Dk.John Magufuli.
“Wananchi wa Chato ngoja niwaambie ninyi ndio ambao mnaongelewa sana bungeni, wananchi wa Chato ndio wanaosemwa sana , wananchi wa Chato ndio mnaongelewa nchi nzima.Siku hizi chochote kizuri kikifanyika hapa (Chato)tunazoewa,”amesema Msukuma.
Amefafanua inashangaza kuona kila ambacho kinafanyika Chato basi watu wanasema tu.”Hivi tunalaana gani kuwa na Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, tunalaana gani tukiwa na Uwanja wa Ndege Chato.Hiki ni kipindi cha maajabu kwa kuhakikisha kura zote zinakwenda kwa Dk.Magufuli,”
Msukuma amesema chini ya utawala wa Rais Dk.John Magufuli amefanya maendeleo makubwa katika maeneo mbalimbali nchini lakini cha kushangaza kukiwekwa taa za barabarani Chato watu wanaanza kuhoji kwanini zinawekwa taa wakati Singida anakotoka Tundu Lissu kuna taa za barabarani.
Hivyo amesema katika uchaguzi Mkuu mwaka huu wananchi wa Chato na Geita kwa ujumla wana kila sababu ya kuhakikisha kura zote zinakwenda kwa Dk.Magufuli na kamba isiharibike kura hata moja.
Amewataka wananchi kuomba kila mtu kwa dini yake ili kuhakikisha Dk.Magufuli anashinda kwa kura nyingi.”Kila mtu aombe kwa dini yake, siku hiyo kazi yetu iwe kura zote kwa Dk.Magufuli.”
Amesema kwa sasa wananchi wa Mkoa wa Geita wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa ambapo amekumbusha hapo zaman hata kwenye machimbo ya madini ya dhahabu walikuwa wanafukuzwa lakini hivi sasa wanaendelea na uchimbaji bila kusumbuliwa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment