DKT. MAGUFULI ATOA BILIONI 12.3 KUBORSHA SEKTA YA AFYA RUVUMA | Tarimo Blog




Na Muhidin Amri, Songea

SERIKALI imeupatia mkoa wa Ruvuma shilingi bilioni  12.3 kwa ajili ya
kuboresha huduma na kuimarisha miundombinu ya  Afya katika mkoa huo
katika kipindi cha miaka minne kutoka 2017 hadi 2020.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga, amesema hayo jana mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Magagura katika halmashauri ya wilaya ya Songea ambacho hadi sasa  ujenzi wake umefikia asilimia 90.

Dkt. Khanga amesema, kupitia fedha hizo mkoa wa Ruvuma umeweza kujenga
vituo 25 vya kutolea huduma  ya afya ikiwemo Hospitali 4  katika
wilaya ya Nyasa,Namtumbo,Tunduru na Songea, Vituo vya afya 16 na
zahanati 5 ambazo zimesaidia sana kuboresha  huduma za matibabu  kwa
wananchi.

Amesema, kati ya fedha hizo halmashauri ya wilaya ya Songea imepata
shilingi bilioni 3.5 ambazo zimewezesha kujenga vituo vya Afya 3  vya
Muhukuru, Magagura na Matimila kwa gharama ya shilingi bilioni
1.3, Zahanati 4 kwa shilingi milioni 400 na Hospitali ya
wilaya 1 inayojengwa katika kijiji cha Mpitimbi ambayo ujenzi wake
umetengewa shilingi bilioni 1.8.

Amesema, gharama ya ujenzi wa kituo cha Magagura ni shilingi milioni
400 ambazo zinahusisha majengo 4, ambayo ni maabara,jengo la mama na
mtoto,jengo la wagonjwa wa nje (OPD)  na upasuaji, lakini kutokana na
ushiriki mkubwa wa wananchi fedha hizo zimewezesha  kuongeza kujenga
choo cha wagonjwa wa nje, kichomea taka na shimo la choo.

Amesema, kujengwa kwa kituo cha Afya Magagura kimsingi itasaidia
kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hasa ikizingatia kuwa
wakazi wa kijiji hicho kwa muda mrefu walilazimika kwenda hadi
zahanati ya Misheni Chipole kufuata matibabu.

Dkt. Khanga, amewapongeza sana wananchi wa kata ya Magagura kwa
ushirikiano waliotoa wakati wote wa ujenzi wa kituo hicho na kuwataka
kuendelea kushirikiana na serikali yao katika ujenzi wa miradi mingine
inayolenga kuchochea maendeleo.

Amewataka watumishi watako pangiwa kwenda kufanya kazi katika zahanati
na vituo  vinavyojengwa kuhakikisha wanawahudumia wananchi na kwenda
kutoa huduma bora na ameonya kujiepusha  kutoa lugha mbaya kwa
wananchi watakaofika kupata huduma za matibabu.

Aidha, ametoa wito wananchi wa kata ya Magagura na mkoa wote wa Ruvuma
kwenda kupata huduma za  matibabu katika zahanati na vituo vya afya
vinavyoendelea kujengwa kwa kuwa serikali imeleta wataalam  na dawa za
kutosha kwa ajili yao.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliokutwa wakishiriki ujenzi  wa
kituo hicho wameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa juhudi kubwa
inayofanya katika kuboresha na huduma za afya hapa nchini.

Eliud Mtewele amesema, kujengwa kwa kituo cha afya Magagura
kutachochea mambo mengi ya maendeleo ambayo hapo awali  hayakuwepo kwa kuwa wakati mwingine wananchi walilazimika  kwenda hospitali ya rufaa
Songea mjini na hospitali ya St. Joseph Peramiho kufuata huduma za
afya.

Jenista Komba mbali na kuishukuru serikali kwa kujenga kituo cha afya
Magagura amesema, kituo hicho kitasaidia kuokoa maisha ya wanawake
wengi wajawazito ambao wanapohitaji kujifungua walilazimika kutumia
usafiri wa pikipiki na baiskeli kwenda hospitali ya Mkoa hivyo baadhi
yao kupoteza maisha wakiwa barabarani kabla ya kufika katika vituo vya
kutolea huduma.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2