HDT YATOA WITO KWA MABENKI NA TAASISI ZA KIMATAIFA KUSAMEHE MADENI | Tarimo Blog

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Health Promotion Tanzania (HDT,) Peter Bujari akizungumza na waandishi wa habari juu ya kampeni ya kuomba kusamehewa madeni kutoka Taasisi mbalimbali za Kimataifa na mabenki.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

SHIRIKA lisilo la kiserikali la health Promotion Tanzania (HDT,) limetoa wito kwa mabenki na Taasisi za Kimataifa zilizoikopesha Tanzania kusamehe madeni  ya mikopo hiyo kama sehemu ya muitikio wa kupunguza madhara ya ugonjwa wa COVID-19 ulioikumba dunia nzima na badala yake fedha hizo zitakazosamehewa au kuondolewa riba zielekezwe katika sekta ya afya ili kuimarisha mifumo ya afya nchini.

 Mkurugenzi Mtendaji wa HDT, Dkt. Peter Bujari ameyasema hayo leo Octoba Mosi, 2020 alipokuwa akizungumza na waandishi habari juu ya kampeni wanayofanya ya kupaza sauti, Tanzania kusamehewa madeni wanayotakiwa kulipa.

Amesema kuwa ni muhimu Mabenki hayo yatafakari kuhusu suala hilo katika vikao wanavyotaraji kukaa siku zijazo, baadhi ya mabenki yanayoikopesha Tanzania ni pamoja na IMF, World Bank, Bank ya Afrika, pamoja na benki ya Korean Exim

"Wito wetu ni kwamba wale waliotukopesha, kama vile, IMF, World bank, bank ya Afrika, BADEA bank pamoja na benki ya Korea Exim bank wafikirie kutusamehe madeni au kuondoa ile riba ambayo tunailipa ili fedha hizo niweze kutumika kwa ajili ya kuiwekeza kwenye mifumo yetu ya afya ili kufanya nayo iwe tayari kupambana na changamoto au milipuko ya magonjwa yatakayotokea badae". Amesema Bujari

Aidha Mkurugenzi Bujari ametoa wito kwa serikali endapo itasemehewa ni vema wakaiwekeza kwenye sekta ya afya kwa kuimarisha mifumo ya afya na kujiweka tayari kupambana na milipuko ya magojnwa itakayojitokeza.

Amesema wito huo ni kuunga mkono wito wa Rais wa Jamuhuri ya Muunganonwa Tanzania, John Pombe Magufuli alioutoa Mapema Aprili 2020 Aidha ametoa wito kwa serikali kuwa iwapo fedha hizo zitapatikana, sekta ya afya ipewe kipaumbele ili iwe tayari kupambana na changamoto zozote za magonjwa  ya mlipuko yanayoweza kutokea.

Amesema, madeni hayo yakisamehewa na fedha zikapelekwa kwenye sekta ya afya itakuwa ni sehemu mojawapo ya muitikio wa kupunguza madhara ya COVID-19 ambayo yamepatikana dunia nzima.

Bujari ameongeza kuwa, makadirio yanaonyeasha kuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 uchumi wa nchi unaonekana utapunguza makusanyo yake na hivyo uwezo wa nchi kulipa madeni utapungua pia.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2