SERA YA NYUMBA KUANDALIWA ILI KUWEZESHA UPATIKANAJI NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU | Tarimo Blog

 


Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA

WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya
Makazi Duniani leo tarehe 5 Oktoba 2020, Serikali iko katika hatua
mbalimbali za kuandaa Sera ya nyumba ili kukabiliana na changamoto
zilizopo kwenye sekta hiyo sambamba na kuwezesha mazingira ya
upatikanaji nyumba za gharama nafuu.

Akitoa salamu za Siku ya Makazi Duniani mwishoni mwa wiki mkoani
Iringa, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amesema, sera hiyo itatoa dira ya uendelezaji wa sekta ya nyumba
nchini.

Ameongeza kuwa, kupitia sera hiyo juhudi zitaelekezwa katika kubuni
mbinu mbalimbali za kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata
nyumba zilizo bora.

Aidha, Waziri Lukuvi amesema serikali imeanzisha miradi na mifuko
mbalimbali ya kusaidia kuwezesha maendeleo ya sekta ya nyumba nchini
na kubainisha kuwa, kupitia mradi wa mikopo ya nyumba mabenki na
taasisi za fedha zimekuwa zikipatiwa mitaji kwa ajili ya kutoa mikopo
ya nyumba. Kwa mujibu wa Lukuvi hadi sasa Serikali ya awamu ya tano
imetoa mikopo isiyopungua bilioni 438.58 na wananchi wapatao 5,460
wamenufaika na mikopo kwa utaratibu huo.

Sambamba na hilo, Lukuvi amesema serikali inafanya kazi kwa karibu na
taasisi mbalimbali za kifedha kwa kuimarisha vyama vya ushirika ili
kuhakikisha fedha zinapatikana kwa makazi ya watu wa kipato cha chini
na kubainisha kuwa mikopo midogomidogo imekuwa ikisaidia ujenzi wa
wamu kwa watu wa kipato cha chini.

‘’Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa Taasisi zisizo za kiserikali
(NGOs) katika kuboresha makazi na baadhi ya taasisi hizo zimekuwa
zikishiriki katika uboreshaji wa nyumba za makazi yasiyokuwa rasmi.’’
amesema Lukuvi.

Aidha, Lukuvi amesema Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI
itaendelea kutekeleza miradi ya urasimishaji nchini kwa kutambua
miliki hatua kwa hatua ili kuyaweka maeneo yenye makazi holela huduma
za kiuchumi na kijamii kupitia mpango shirikishi.

‘’Miradi hii itaendelea katika miji mbalimbali nchini kwa lengo la
kuboresha hali ya maisha ya makazi husika na kupunguza umasikini,
faida nyingine ni pamoja na kuongeza usalama wa miliki kwa kutoa hati
miliki za ardhi’’ amesema Lukuvi.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema, Wizara yake iko katika maandalizi
ya kufanya sensa ya nyumba ili kutambua idadi kamili ya nyumba na
kusaidia kubaini uhaba na hali ya nyumba na kusisitiza kuwa matokeo ya
sensa hiyo yatasaidia kuandaa mipango mikakati ya maendeleo ya nyumba.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila jumatatu ya kwanza ya mwezi
Oktoba ya kila mwaka ambapo Mataifa yote Duniani hujumuika kuadhimisha
siku hiyo ikiwa ni azimio namba 40/202 la Umoja wa Mataifa la mwezi
Disemba mwaka 1985.  Siku hiyo hujulikana kote duniani kama siku ya
makazi Duniani. Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya utaratibu
wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) huadhimisha siku hii kwa
njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafakatri hali ya makazi katika
nchi na changamoto zake husika na kupanga mikakati ya kukabiliana na
changamoto hizo. Ujumbe wa mwaka huu ni Nyumba kwa wote Miji bora ya
Baadaye.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2