Mkurugenzi wa Sheria kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation, Anitha Moshi akifungua Shampeni ikiwa ni sehemu ya kusherekea wiki ya Huduma kwa Wateja iliyoanza leo, Oktoba 5 ulimwenguni kote leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania, TTCL Corporation limehaidi kuendelea kutoa huduma bora, za uhakika na kwa gharama nafuu katika mazingira ya kiteknolojia ili kukidhi mahitaji ya wateja wanaotumia huduma za Shirika hilo kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa ulimwenguni kote kwa malengo ya kutoa shukrani kwa wateja kwa kuendelea kutumia huduma zao, Mkurugenzi wa biashara kutoka TTCL, Vedastus Mwita amesema katika maadhimisho ya mwaka huu, Shirika hilo litaongezaa kasi zaidi katika Kuhakikisha wateja wao wanapata huduma bora zaidi na kwa wakati.
"Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Dream Team"...Timu ya ushindi kwetu sisi inaakisi kwa kuonesha umuhimu wa kushirikiana katika kutoa huduma bora kwa wateja wote kwa kuzingatia weledi, kujali wateja na kuhakikisha wateja wanapata zaidi ya wanachohitaji na daima tunatambua mchango wa wateja kupitia huduma tunazotoa katika na uchangiaji wa ukuaji wa Shirika letu na maendeleo ya Taifa kwa ujumla." ameeleza Mwita.
Mwita amesema kuwa, kwa kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu Wakurugenzi wa Shirika hilo na Mameneja wa Mikoa ya kibiashara jijini Dar es Salaam watatembelea vituo vya huduma kwa wateja ili kuwahudumia wateja, kukutana nao kusikiliza maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha zaidi huduma zitolewazo na Shirika hilo.
Vilevile amesema, katika kuendelea kuhakikisha kila mteja wa TTCL anaendelea kupata huduma kwa wakati, Shirika hilo limeendelea kubuni njia mbalimbali ambazo wateja wanaweza kutoa maoni na kero mbalimbali zinazojibiwa na kuhudumiwa kwa wakati.
"Wateja wetu sasa wanaweza kutembelea kituo chetu cha huduma kwa wateja kwa kupiga namba 100, website yetu na mitandao ya kijamii ambapo mteja anaweza kueleza changamoto zake na kuhudumiwa wakati wowote" ameeleza.
Aidha, kwa niaba ya Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL Mwita amewashukuru wateja wote wa ndani na nje ya nchi wakiwemo kutoka Rwanda, Kenya, Uganda,Burundi, Zambia na Malawi kwa kuendelea kuwaamini na kutumia huduma zao.
"Wiki hii tutaendelea kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja wetu, tunashukuru kwa kuendelea kutuamini na kutumia huduma zetu, TTCL ni timu ya ushindi....Rudi Nyumbani Kumenoga!." Amesema.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment