Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza
na waasisi wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake wa nchi huru za Afrika
(PAWO) jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto – akiwa katika picha ya pamoja na waasisi wa Umoja wa Jumuiya
za Wanawake wa nchi huru za Afrika (PAWO) jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake wa nchi huru za
Afrika (PAWO) Leah Lupembe akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu wakati wa mkutano na waasisi wa
Umoja huo Jijini Dar es salaam.(Picha zote na kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW.)
Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John
Jingu amewataka waasisi wa Jumuiya za wanawake wa nchi huru za Afrika
PAWO kuendelea na mapambano ya kuwakomboa wanawake kiuchumi, kijami na kiutamaduni.
Akizungumza na waasisi hao jijini Dar es salaam Dkt. Jingu amesema
PAWO imetoa mchango mkubwa katika bara la Afrika wakati wa harakati za
kuondokana na ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa wakoloni lakini bado
mapambano yanaendelea ambayo ni kujikomboa kiuchumi katika nchi na mtu
mmoja mmoja.
Ameongeza pia, Serikali kupitia Wizara ya Afya – Idara Kuu ya
Maendeleo ya jamii imeweka kipaumbele suala zima la kuwakomboa
wanawake kiuchumi kwa kutambua kuwa, mwanamke akiwezeshwa kiuchumi
ataweza kujitegemea kwa mambo mengi hivyo kuepukana na unyanyasaji
unaotokana na uchumi duni.
“Katika shughuli zetu zote tumeweka suala la kuwawezesha wanawake
kiuchumi kuwa kipaumbele, tunafanya hivyo kwa sababu tunajua mwanamke
akiwezeshwa kiuchumi mambo mengine yote yanaweza kufunguka”amesema
Jingu.
Katibu wa Umoja huo hapa nchini Marie Shaba amesema, tangu kuanzishwa
kwake umoja huo Pamoja na shughuli nyingi walizofanya waasisi,
wameamua kuendelea kupambana kwa kufanya kampeni kuibua mambo ambayo yatafanya jamii iweze kubadili fikra na tabia katika ngazi zote
ikiwemo mila na desturi.
Kwa upande wake mwanasheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Charles Mpaka amewashauri waasisi hao kufuata sheria na
taratibu za usajili wa mashirika na kuwa, Ofisi ya Msajili ipo tayari
kuwapa ushirikiano.
Umoja huo ulianzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kuwaunganisha wanawake
wa nchi za Afrika ili kutoa msukumo wa kushirikishwa kiuchumi na
kijamii ambapo kwa sasa umoja huo unaingia hatua ya kuwa shirika
lisilo la Kiserikali kuendeleza majukumu yake
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment