Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga (pichani) amesema Tanzania kwa zaidi ya miaka 45 imekuwa na uh
usiano mzuri na nchi za umoja wa ulaya na kwamba bado wanaendelea kushirikiana katika mambo yanayohusu maendeleo.
Balozi Nyamanga amesema hakuna kikao chochote cha Bunge zima la Umoja wa Ulaya kilichoketi, kujadili na kuazimia kuizuia Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi za umoja huo na wala kujadili uchaguzi wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28 na kuwataka wananchi kupuuza uvumi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu umoja huo kuiwekea vikwazo Tanzania.
Hivi karibuni kumekuwa na uzushi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Umoja wa Ulaya na mashirika yake umeameadhimia kusitisha misaada na mikopo kwa Tanzania, taarifa ambayo Balozi Nyamanga amesema ni ya upotoshaji na kwamba Bunge la Umoja wa Ulaya halijaiwekea vikwazo Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi za umoja huo.
“Novemba 19 asubuhi hapa Ubelgiji kamati ya Bunge ya mambo ya nje ya umoja wa ulaya ilikutana katika kikao chake cha kawaida, moja ya masuala yaliyojadiliwa katika kamati hiyo ilihusu Tanzania na hali ilivyo baada ya uchaguzi mkuu kukamilika, huu ni utaratibu wa kawida kabisa wa Kamati ya Bunge la Umoja wa ulaya kujadili na kuweka majadiliano na nchi ambayo ni mbia wao wa maendeleo pindi tu uchaguzi unapokamilika katika nchi husika na hasa uchaguzi Mkuu” alisema Balozi Nyamanga
Alisisitiza “Kuna taarifa zinaenezwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii taarifa za upotoshaji na zisizo na ukweli wowote zikidai eti Bunge lote la Umoja wa Ulaya leo limeadhimia kusitisha misaada kwa Tanzania na Mikopo kutoka Umoja wa Ulaya na katika mashirika yake, taarifa hiyo ni ya upotoshaji inadai kwamba eti Bunge la Umoja wa Ulaya limeweka azimio la kuiwekea Tanzania Vikwazo na kwamba eti limeazimia kuzuia Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi za umoja wa ulaya, ni uongo mtupu”
Balozi Nyamanga amesema kikao kilichofanyika Novemba 19 kilikuwa ni cha kamati ya bunge ya mambo ya nje, na sio kikao cha Bunge lote la Umoja wa Ulaya kama ilivyonukuliwa sehemu ya taarifa ya upotoshwaji inayoenea kwenye mitandao ya kijamii na kwamba hata kikao hicho cha Kamati ya Bunge hakikutoa azimio lolote kuhusu Tanzania, huku akibainisha kuwa kilichofanyika ni kutoa nafasi kwa wabunge hao kujadili na kutoa mawazo yao kuhusu hali ya Tanzania ya uchaguzi ambapo ni wabunge watano tu waliotoa mawazo yao kati ya Wabunge 71 wa Kamati hiyo ya mambo ya nje huku Bunge lote la Umoja wa Ulaya likiwa na jumla ya Wabunge 705.
“Waliozungumza kwenye kamati ni wabunge watano tu na wametoa mawazo yao tofauti walivyoona, sio azimio, sio makubaliano na hakuna azimio lolote lililowekwa, kwa hiyo taarifa zinazoenezwa sio za kweli, ni za uongo na zinafanywa na watu wenye nia mbaya na Tanzania, eti taarifa hizo zinadai kwamba eti Bunge lote la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania Msaada wa Euro Milioni 626 na pia zinadai kuwa Tanzania inapewa fedha hizo na Umoja wa Ulaya kila mwaka, ni upotoshaji mkubwa sio kweli, kwanza umoja wa Ulaya hauipi Tanzania Euro 626 sawa na Trilioni 1.6 wanazodai kila mwaka, sio kweli na si kweli kwamba fedha hizo zimesitishwa, fedha hizo hazijasitishwa na utekelezaji wa miradi unaendelea tena unaendelea vizuri na hakuna azimio lolote la kusitisha fedha hizi.” Alisema Balozi Nyamanga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment