Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Morogoro
MHAHADHRI Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(SUA) Profesa John Jeckoniah ametoa mwito kwa waandishi wa habari nchini kuhakikisha wanaandika habari zinazohusu usimamizi wa misitu ya jamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Amesema katika shughuli zozote za kijamii ni vema kukawa na usawa wa kijinsia ili kuhakikisha jamii yote inakwenda pamoja na hakuna anayeachwa nyuma kwasababu zozote zile zikiwemo ya kijinsia au jinsi.
Profesa Jeckoniah ameyasema hayo wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka kwa vyombo vya habari mbalimbali nchini yanayohusu masuala ya jinsia ambayo yameandaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) pamoja na Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania ((MJUMITA).
"Kama waandishi wa habari wakijengewa uwezo katika eneo hilo watakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa taarifa au kuandika habari zenye tija na ambazo hazitakuwa na upotoshaji wa taarifa.Habari zinazohusu masuala ya jinsia au jinsi yanahitaji umakini , hivyo ni matumaini yangu mafunzo haya yanakwenda kuongeza tija kwa waandishi wa habari na yatakuwa chachu ya wao kuandika zaidi.
"Uwiano wa masuala ya kijinsia nchini bado upo chini na sio kwetu tu Tanzania bali katika nchi nyingi duniani, hivyo njia sahihi ya kufanikiwa katika eneo hilo ni kuwajengea uwezo waandishi ili wawe na uwanja mpana katika kuripoti hasa kwenye USMJ,"amesema.
Aidha amesema katika eneo la maendeleo nchini uwiano wa kijinsia bado haupo vizuri pamoja na ukweli kuwa wanawake wanaweza kufikia rasilimali ila uamuzi wa mwisho kuhusu matumizi ya rasilimali inabakia kwa wanaume jambo ambalo linapaswa kupingwa na wadau wote huku akifafanua sababu mojawapo ni kuendelea kuwepo kwa tamaduni ambazo jamii inaona iko sawa lakini kwa jicho la kijinsia sio sahihi.
Ameeleza kumekuwepo na juhudi mbalimbali zinazoendelea kwa lengo la kubadilisha jamii kuhakikisha wanatambua na kuzingatia umuhimu wa masuala ya kijinsia katika shughuli zao za kila siku."Hata mkakati wa kuwa na uwiano wa 50 kwa 50 katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vyombo vya uamuzi unalenga kuweka usawa."
Amesisitiza Serikali imekuwa ikifanya jitihada kwa kuandaa sera, sheria na miongozo ila tatizo kubwa lipo ngazi ya chini za utekelezaji, hivyo wanawake kuwa waathirika wakubwa na njia ya kutoka hapo ni waandishi kutumia nafasi zao kubadilisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo amesema mafunzo hayo kuhusu msuala ya jinsia ambayo yanatolewa kwa waandishi wa habari ni ni moja ya mkakati wao kwenye Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) ambao umechochea mabadiliko makubwa kwenye USM.
Wakati huo huo Meneja Mradi kutoka TFCG Charles Leonard ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina kuhusu miradi mbalimbali ambayo inaendelea kutekelezwa na shirika hilo katika maeneo ya mradi na kubwa zaidi wanahimiza kuzingatiwa kwa usawa wa kijinsia.
Amefafanua awamu ya kwanza na ya pili wamefanikiwa kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwenye hekta 130,000.Pia wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuchochea uhifadhi wa misitu kwenye vijiji, ambavyo vimekuwa na mradi wa usimamizi wa misitu ya asili.
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG)Emmanuel Lyimo(wa kwanza kulia) akiwa na washiriki wengine katika semina iliyoandaliwa na shirika hilo mkoani Morogoro kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari namna ya kufahamu vema na kuzipa nafasi habari zinazohusu masuala yanayohusu jinsi na jinsia katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa umma kutoka TFCG Bettie Luwuge (wa kwanza kushoto) akiwa na washiriki wengine wa semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya jinsi na jinsia ambayo inafanyika mkoani Morogoro.
Mhadhiri kutoka Chuo cha Kilimo Sokoine(SUA)Profesa John Jeckoniah ambaye amebobea katika masuala ya jinsia akifafanua jambo wakati alipokuwa akitoa mada inayozungumzia kwa kina kuhusu tofauti ya jinsi na jinsia na majukumu yao katika jamii.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika semina hiyo wakifuatilia mada zinazotolewa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG)Emmaneul Lyimo akizungumza alipokuwa akifungua rasmi semina ya mafunzo ya masuala ya jinsia ambayo yameandaliwa na shirika hilo kwa ajili ya kuwajengea uwezo na uelewa waandishi wa habari kutambua mambo yanayohusu jinsia na jinsi katika shughuli mbalimbali zikiwemo za ushiriki wa wanawake na wanaume katika usimamizi wa misitu ya asili nchini.
Baadhi ya washiriki ambao wanatoka shirika la usimamizi wa misitu ya asili wakifuatilia mada zinazotolewa kwenye semina hiyo.
Meneja Mradi kutoka TFCG Charles Leonard akielezea mikakati ya shirika hilo katika kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu usimamizi wa misitu ya asili nchini na namna ambavyo wamejipanga katika kuendeleza miradi iliyoanzishwa katika maeneo ya miradi kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika pamoja na Serikali.
Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa makini kufuatilia mada wakati wa semina hiyo ikiendelea.
Mmoja ya wafanyakazi kutoka TFCG akigawa majarida kwa washiriki wa semina hiyo.Majarida hayo yanaeleza kwa kina shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment