Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
TAASISI ya Furahika Education College inayotoa mafunzo ya ufundi, sanaa na elimu kwa wajasiriamali imetoa mkopo wa shilingi milioni 100 kwa wakulima wadogo wa parachichi kutoka Mkuranga, Kibiti na kata ya Ilala ili waweze Kuboresha kilimo hicho chenye soko la uhakika duniani.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalumu kwa wajasiriamali, wakulima na wafugaji Mkurugenzi wa Furahika Education College David Msuya amesema, katika kuunga mkono juhudi za Rais John Joseph Magufuli kituo hicho kimekuwa kikikutana na makundi mbalimbali na kuwezesha mbinu faafu za kujikwamua kiuchumi kupitia viwanda.
"Licha ya kutoa mafunzo ya ufundi na sanaa kwa vijana taasisi yetu pia inafanya kazi kwa ukaribu na makundi ya wajasiriamali, wakulima na wafugaji kwa kushauri, kusikiliza na kutatua na kutatua kero zinazowakabili ili waweze kufanikiwa kupitia shughuli wanazozifanya." Ameeleza.
Msuya amesema kuwa kwa wakati huu viwanda vingi vimeanzishwa hivyo ni vyema wananchi wakavitumia kama fursa ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuzitaka taasisi za aina hiyo kuwashika mkono wananchi katika kufanikisha hilo.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo kata ya Ilala Jemima Laizer amesema, kupitia mafunzo hayo wamebaini wajasiriamali wengi wanakupambana na changamoto ya masoko na pembejeo kwa wakulima na wafugaji na kuiomba serikali kuwasaidia katika utoaji wa pembejeo na rasilimali nyingine kwa kuwa maeneo ya kufanyia shughuli za kimaendeleo zipo.
Amesema kuwa kupitia kikao hicho wakulima, wafugaji na wajasiriamali wameomba kuwepo kwa maafisa masoko watakaosimamia masoko ya bidhaa pamoja na utangazaji wa bidhaa katika mitandao.
Mmoja ya wakulima waliohudhuria mkutano huo Omar Mtemamkano kutoka Mkuranga amesema;
"Licha ya kupata fedha za kujikimu na kusomesha bado magonjwa ya mifugo na mazao yanatutesa, tunaomba Serikali itusaidie kwa kutoa rasilimali fedha, maeneo yapo tukifanikisha hilo tutasonga mbele zaidi." Amesema.
Aidha amesema kuwa kupitia kikao hicho wamepata somo zuri kuhusu zao la parachichi ambalo uhakika wa soko ni mkubwa ulimwenguni na kuahidi kuwa watajiingiza katika kilimo hicho kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Ameeleza, Licha ya kujishughulisha kilimo cha uyoga, mihogo na ufugaji wa kuku wa kienyeji, fursa ya kilimo cha parachichi hakiwezi kumpita na amewashauri wakulima kufuata ushauri wa kilimo kwa kuzalisha mazao yenye ushindani sokoni.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment