Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akifanya mazungumzo na Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Chalinze, Enrico Shauri.
Na Mwandishi wetu, Chalinze
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametembelea na kufanya mazungumzo na Meneja na wafanyakazi wa Wakala wa barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Chalinze.
Awali akizungumza Meneja wa TARURA alisema wamejipanga vizuri kukarabati na kujenga Miundombinu ya barabara za Vijiji na Mjini ikiwemo Mji wa Chalinze japo iko changamoto ya ufinyu wa bajeti jambo ambalo Mh. Mbunge aliahidi kwenda kulishughulikia ikiwemo kushauriana na Madiwani wenzake kujenga hoja ili aongezewe mafungu.
Kwa upande wake Mbunge Ridhiwani Kikwete amemshukuru Mkandarasi na TARURA kwa ujumla kwa jinsi walivyojitahidi kujenga miundombinu pamoja na changamoto ya bajeti lakini pia alitumia ziara hiyo kujadili vipaumbele ambavyo wananchi wanahitaji Serikali yao chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli visimamiwe.
"Wana Chalinze wanahitaji miundombinu bora ya barabara TARURA mnajitahidi sana hongereni kwa hilo. Barabara korofi zote za Halmashauri zikiwemo zile za Kata ya Kimange, Miono, Mkange, Vigwaza, Ubena, Talawanda, Mandela, Mji wa Chalinze na maeneo mengine kama sehemu za kutolewa macho sana kutokana na shughuli za kimaendeleo na kuchangia uchumi katika Halmashauri yetu." Ameeleza Ridhiwani Kikwete.
Aidha, Mbunge amehaidi ushirikiano zaidi ili kufikia malengo makubwa waliyopanga kuyasimamia kwa pamoja wakishirikiana na Wananchi.
Mbali ya TARURA, tayari Mbunge ameshatembelea DAWASA-Chalinze kujionea miradi mikubwa ya maji inayoendelea kujengwa ilikuondoa kero ya maji jimboni humo.
Ziara ya Kata kwa Kata anaitarajia kuanza siku ya Jumatatu ya tarehe 30 Novemba ambapo atakagua miradi ya Maendeleo na kuzungumza na Wananchi kwa kusikia kero na matarajio waliyonayo kwa Serikali yao inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment