Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MKURUGENZI Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo amehukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzuia askari kutekeleza majukumu yao kufuatia upande wa mashtaka kuthibitisha kesi yao dhidi yake.
Pia mahakama imemuamuru Melo kutokurudia kosa hilo ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Aidha, mahakama hiyo imemwachia huru mshtakiwa Mike Mushi aliyekuwa akishtakiwa pamoja na Melo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake na Hakimu Shahidi kusema kuwa Mushi alikuwa ni kama msindikizaji katika kesi hiyo.
Hukumu hiyo imesomwa leo Novemba 17,2020 baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao kwa kuleta mashahidi sita huku Melo akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.
Awali kabla ya kusomwa hukumu hiyo hakimu Shaidi aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo, Wakili wa serikali, Farajih Ngukah aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwani kitendo alichokifanya cha kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ni hatari kwa Taifa.
Katika utetezi wake Melo, kupitia wakili wake Bernedict Ishabakaki ameiomba mahakama kumpatia mteja wake adhabu ya faini kwani ana vijana ambao amewaajiri na wanamtegemea hivyo faini itakuwa fundisho kwake.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Shaidi amema mshtakiwa alionekana kuwa na makosa katika kesi ambazo zilifunguliwa awali na zote zilikuwa na makosa yanayofanana.
"Jeshi la Polisi liko kwa ajili yetu sote kazi yake ni kupeleleza na sisi ni wajibu wetu kushirikiana nalo, mahakama inaweza kukumbusha hilo."
Katika kesi ya msingi inadaiwa,kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 huko Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Melo na Mushi waliendesha mtandao ambao haujasajiwa kwa kikoa (domain) cha.tz na katika shtaka jingine walidaiwa kuzuia askari Polisi kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment