Mwakinyo, Paz kuzichapa jioni hii Next Door Arena kuwania mkanda wa WBF wa mabara | Tarimo Blog

  Bondia Hassan Mwakinyo anapanda jukwaani usiku wa leo kutetea  ubingwa wake wa Mabara wa WBF wa  uzito wa super welter dhidi ya bondia Jose Carlos Paz wa Argentina.

 Pambano hilo  la raundi 12 limeandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sport chini ya ukurugenzi na mwanzilishi, Kelvin Twissa na kuthibitishwa na Kamisheni ya ngumi za kulipwa ya Tanzania (TPBRC) na WBF.

 Mbali ya pambano hilo, leo pia kutakuwa na mapambano ambapo  bondia Hussein Itaba atazichapa na  Alex Kabangu wa  DR Congo ambapo  Fatuma Zarika wa Kenya ataonyeshana kazi na  Patience Mastara  wa Zimbabwe katika pambano la.ubingwa wa dunia wa uzito wa super bantam wa WBF na Mtanzania Zulfa Macho atazichapa na Alice Mbewe wa Zambia.

Mbali ya TPBRC, rais wa WBF Howard Goldberg atasimia pambano hilo huku mwamuzi maarudu duniani, Edward Marshall atawachezesha mabondia hao ambao wametambiana kila mmoja kushinda pambano hilo.

Akizungumza mara baada ya kupima uzito, Mwakinyo alisema kuwa anarajia kushinda pambano hilo  katika raundi za mwanzoni na kuwaomba mashabiki kuwahi kuingia.

“Nataka kufanya staili ya mabondia wa zamani kama Mike Tyson ambaye alikuwa anamaliza pambano huku mashabiki wakiwa katika foleni ya kuingia na wengine wakikata tiketi. Nawaomba mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini, kuwahi kukata tiketi na kuwahi kuingia ili washuhudia nikiweka historia nyingine,” alisema Mwakinyo.

Mwakinyo alisema kuwa  atahakikisha Paz anaachana na mchezo wa ngumi za kulipwa kutokanana kipigo alichumuandalia.

“Ninachoongea ndicho ninakimaanisha, nataka kuonyesha mimi ni bondia wa iana gani katika familia yetu ambayo mchezo wa ngumi na kickboxing ni moja ya shughuli zake, sina mchezo katika pambano hili,” alisema huku akisisitiza kuwa kamwe hata mdharau mpinzani wake.

Paz alisisitiza kuwa mikono yake ndiyo ‘itaongea’ ulingoni katika kuthibitisha ubora wake. “Najua Mwakinyo anaongea sana, ni kawaida, lakini mimi nitaonyesha vitendo na kuondoka na mkanda huu,” alisema Paz kwa kifupi.

Rais wa WBF, Howard Goldberg alisema kuwa  maandalizi ya pambano la jioni hii yamekamilika na endapo Mwakinyo atashinda pambano hilo, atapata nafasi ya kuwania ubingwa wa dunia dhidi ya bingwa mtetezi, Lasha Gurguliani wa Georgia ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

“Napenda kuwashukuru  kampuni ya Jackson Group Sport kwa kuandaa pambano hili na kurejesha thamani ya ngumi za kulipwa nchini.  Hii ni mara yangu ya saba kuja nchini, lakini sijawahi kushuhudia weledi wa aina hii katika kuandaa pambano,” alisema Goldberg.

Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema kuwa maandalizi yamekamilika na kwa mara ya kwanza Tanzania inawakutanisha mabondia kutoka nchi nyingine tano duniani na kuweka historia.

Twissa alisema tiketi zinaendelea kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh 3 Milioni kwa meza ya watu 10 na  Sh150,000 kwa kwa viti vya kawaida.


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jackson Group Sport Kelvin Twissa (katikati) akiwatambulisha mabondia Hassan Mwakinyo (kulia) na Jose Carlos Paz ambao watapambana leo Ijumaa Novemba 13, 2020 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay kuwania mkanda wa mabara wa WBF.

Bondia Hassan Mwakinyo akipima uzito tayari kwa pambano la leo Ijumaa Novemba 13, 2020 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oyesterbay

Bondia Jose Carlos Paz akipima uzito tayari kwa pambano la leo Ijumaa Novemba 13, 2020 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oyesterbay.
 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jackson Group Sport Kelvin Twissa (katikati) akiwatambulisha mabondia Fatuma Zarika kushoto) na Patience Mastara wa Zimbabwe ambao watapambana leo Ijumaa Novemba 13, 2020 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay kuwania mkanda wa Dunia wa WBF wa uzito wa bantam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2