Charles James, Michuzi TV
WANAWAKE wanaweza, Rais Dkt. John Magufuli amesema serikali ya awamu ya tano itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi kwani wameonesha ni jinsi gani wanaweza wakiaminiwa.
Dkt. Magufuli ameitoa kauli hiyo jijini Dodoma ambapo anazindua Bunge la 12 sambamba na kulihutubia Taifa kupitia bunge hilo Novemba 13, 2020.
"Nipende kuwaambia wanawake kuwa serikali yangu itaendelea kuwaamini na kuwapa nafasi mbalimbali za kiuongozi wanawake maana nimeona ni jinsi gani mnachapa kazi na ndio maana hata Makamu wa Rais ni Mwanamke na pia nikupongeze na Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuendelea kuwa Naibu Spika." Amesem Rais Magufuli.
Akizungumzia huduma za jamii, Rais Magufuli amesema wataendelea kuimarisha sekta hizo ikiwemo ya Afya ambayo miaka mitano iliyopita vifo vya akina Mama wajawazito vimepungua kutoka vifo 11,000 kwa mwaka hadi kufikia vifo 3,000 na kwamba wamepanga kupunguza kabisa.
Amesema miaka mitano ijayo ujenzi wa vituo vya afya na zahanati utaendelea katika maeneo ambayo havipo lakini pia kuboresha bima za afya pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vya afya.
" Tumeona katika janga la Corona, miaka mitano ijayo maduka ya dawa asili ama mbadala yataruhusiwa, ikiwezekana watu kutoka nje ya nchi waje kutibiwa nchini na kimsingi wameshaanza kuja.," Amesema Dkt.Magufuli.
Kuhusu sekta ya elimu Rais Magufuli amesema serikali yake itaendelea kutoa elimu bila malipo, kuboresha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha miundombinu ya elimu.
"Tutaendelea kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na tutajenga shule moja kila mkoa kwa ajili ya masomo ya sayansi kwa ajili ya watoto wa kike, lakini pia tukitilia mkazo elimu ya ufundi." Amesema Rais Magufuli.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment