RAIS MAGUFULI: UWAZIRI MKUU SIYO KAZI YENYE 'GUARENTEE', MAJALIWA AMTANGULIZE MUNGU MBELE | Tarimo Blog

 
Charles James, Michuzi TV

UWAZIRI Mkuu hauna 'guarantee'! Ndiyo kauli ambayo Rais Dk John Magufuli ameitoa leo Ikulu Chamwino, Dodoma wakati akimuapisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo licha ya kumpongeza kwa uteuzi huo wa mara ya pili amemtaka kumtanguliza Mungu mbele na kuchapa kazi.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uapisho ambao amewaapisha pia mawaziri wawili aliowateua, Prof Palamagamba Kabudi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Dk Philip Mpango wa Wizara ya Fedha na Mipango, Rais Magufuli amewataka wabunge kuondoa presha ya uteuzi wa uwaziri badala yake wajikite katika kuwatumikia wananchi kwani ridhaa waliyoomba ilikua ni ubunge na wala siyo uwaziri.

Dk Magufuli amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni kiongozi mnyenyekevu, msikivu ambaye amefanya kazi kubwa katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya awamu ya tano lakini akamtaka kutokua na uhakika wa nafasi yake badala yake amtangulize Mungu huku akichapa kazi kwa bidii.

" Waziri Mkuu nikupongeze sana kwa nafasi hii, nilikua naangalia mawaziri wakuu wenzako waliopita muda waliokaa nikaona nikuteue haraka haraka sasa sijui nilipatia? Maana Nyerere alikaa mwaka mmoja, Kawawa mitatu, Sokoine mitatu, Msuya mitano, Sokoine akarudi akakaa mwaka mmoja tena, Dk Salim akakaa mwaka mmoja, Warioba mitano, Malecela minne na Msuya akarudi kukaa mmoja, Sumaye yeye ndio alikaa miaka 10 yote, Lowassa mitatu na Pinda saba. 
Hivyo ndugu zangu nataka muelewe kuwa nafasi ya uwaziri mkuu siyo ya 'guarantee' sana itategemea na ufanyaji kazi wake hivyo umuombe sana Mungu na wabunge pia mumuombee ili aweze kufikia rekodi ya Sumaye na Mama Majaliwa pia uelewe una kazi ya kumuombea mumeo," Amesema Dk Magufuli.

Akizungumzia nafasi mbili za uwaziri alizowateua Prof. Kabudi na Dk Mpango, Rais Magufuli amesema wala hakua na haraka ya kuchagua mawaziri kwa haraka lakini hao wawili ni kwa vile katika baraza lililopita walikua ni wabunge wa kuteuliwa na wakaenda kugombea majimbo wakashinda na walifanya vizuri pia kwenye baraza la mawaziri lililopita.

" Sikua na haraka ya kuteua safari hii tuna wabunge zaidi ya 350 bado wale 10 wa nafasi zangu, hawa wawili ni kwa sababu wabunge inabidi mlipwe mshahara na miradi mingine iendelee ndio maana nimechagua Waziri wa Fedha, lakini pia Wizara ya Mambo ya Nje ni lazima tuwe na Waziri wa kutusemea.

Wasaidizi wangu waliniletea ushauri niteue Waziri wa Mambo ya Ndani na wa Ulinzi sikuwajibu, nikanyamaza kwa sababu sikuona ulazima wa kufanya hivyo haraka, Mkuu wa Majeshi hata akiwa na shida hatoenda kwa Waziri atakuja kwangu, hivyo hivyo kwa IGP na Makatibu Wakuu wapo hivyo tuna haja ya kusubiri na wala hakuna haraka ya kuchagua baraza," Amesema Rais Magufuli.

Amewataka wabunge kuondoa presha walizonazo za uchaguzi na kuacha kwenda kwa waganga kuloga kwani watajitia nuksi na badala yake wajikite katika kazi ya kuwatumikia wananchi wao waliowachagua kwani ndio kazi waliyoiomba na kukabidhiwa Ilani ya CCM kwa ajili ya utekelezaji wake.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2